5. Ramadhan

Tukiwa tunaelekea Ramadhan, tuijue Qur’an

Zimebakia wiki chache tu panapo majaaliwa kabla ya kuingia katika masiku matakatifu ya mwezi wa Ramadhan, mwezi wa Qur’an. Bila shaka Waislamu tupo katika hamkani za maandalizi ya kuupokea mwezi huu na kujivunia mengi ya kheri. Allah atufikishe Ramadhan.

Bila shaka Waislamu tunaelewa vyema mahusiano ya Qur’an na Ramadhan. Tunaelewa kwamba Qur’an kwa mara ya kwanza iliteremshwa ndani ya mwezi wa Ramadhan, na kwamba ilikuwa kawaida Jibril kuja kumsikiliza Mtume kila Ramadhan.

Mahusiano haya yanaelezwa kwa ufasaha katika kauli yake Allah: “Ni mwezi wa Ramadhan ambao imeteremshwa ndani yake Qur’an.” (Qur’an, 2:185).

Waislamu wamehimizwa kuisoma zaidi Qur’an tena kwa mazingatio katika mwezi mtukufu wa Ramadhan. Ni kwa ajili ya himizo hilo ndiyo maana utawaona wameshughulika zaidi humo na kitabu hiki kitakatifu.

Licha ya ukweli huo, inawezekana kabisa Muislamu huyu ambaye anaushika msahafu akiamini ndani yake mna maneno matakatifu ya Allah, hajui ilikuwaje kihistoria hadi Qur’an kushushwa na namna ilivyohifadhiwa mpaka ikaja kwa sura inayoonekana hivi leo.

Kwa sababu hiyo basi, tumeona ingekuwa vyema Muislamu kuyafahamu haya kwa ufasaha ili awe na yakini juu ya ukweli wa maneno haya na ili aweke kinga dhidi ya majaribio yanayofanywa na maadui kuwataka Waumini kukikanusha kitabu chao.

Makala yetu hii ina lengo la kumsaidia, na kumkumbusha mpendwa msomaji angalau kwa muhtasari namna Qur’an ilivyoteremka na kuhifadhiwa –kwa kiasi tunachokijua- kwa kupitia dondoo za fani ya Uluum-al Qur’an (elimu ya tafiti za Qur’an). Tunamuomba Allah atuwezeshe hilo.

Qur’an ilivyoteremka
Kuna tofauti moja kubwa baina ya Qur’an na vitabu vingine vya mbinguni. Vitabu vyengine viliteremshwa kwa mkupuo mmoja, lakini hali haikuwa hivyo kwa Qur’an. Wataalamu wa fani ya Uluumul-Qur’an wanasema kuwa, Qur’an ina miteremko miwili: mteremko wa kwanza ni ule wa kutoka mbingu ya saba hadi mbingu ya dunia, yaani mbingu hii inayoonekana ama inayohisika, kama anavyoeleza mwenyewe Allah Aliyetukuka: “Hakika sisi tumeiteremsha (Qur’an) katika usiku wenye cheo.” (Qur’an, 97:1).

Mteremko wa pili, ni kuteremshwa kutoka uwingu wa dunia kidogo kidogo, kuja kwenye moyo wa Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) kwa mujibu wa matukio kwa muda wa miaka 23.

Namna Qur’an ilivyohifadhiwa Kitu cha kwanza muhimu kwa Muislamu kukifahamu ni kwamba, muda wa ulinganiaji wa Mtume ulikuwa ni miaka 23 tu. Ni katika kipindi hiki ndiyo Qur’an iliteremshwa kwake kama tulivyogusia, ambapo Malaika aliyehusika na jukumu hili alikuwa ni Jibril (amani ya Allah iwe juu yake), kama anavyosema Allah aliyetukuka: “Na hakika huu ni uteremsho kutoka kwa Mola wa viumbe ameuteremsha Roho Muaminiwa (Jibril) juu ya moyo wako ili uwe miongoni mwa waonyaji, kwa lugha ya Kiarabu wazi wazi.” (Qur’an, 26:190-195).

Historia inatuonesha kwamba, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) akiwa katika moja ya milima ya nje kidogo ya mji wa Makka, katika pango la Hiraa, ndani ya mwezi wa Ramadhan, kwa mara ya kwanza aliupokea ujumbe huu ambao sasa umehifadhiwa katika msahafu, akaambiwa: “Soma.” Kuanzia hapo Qur’an ilianza kuhifadhiwa katika sura kuu mbili, yaani kuhifadhiwa katika vifua vya watu na kwa kuandikwa.

Sura ya kwanza: Kuhifadhiwa vifuani
Kila ilipoteremka sura au Aya, Mtume aliihifadhi moyoni, na aliwasomea Maswahaba zake, ambao nao waliihifadhi vifuani na wakafundishana. Kadhalika Maswahaba hao pia walikwenda kuwahifadhisha wake na watoto wao, na kwa namna hiyo Qur’an ikahifadhika.

Sura ya pili. Kuandikwa Sura ya pili ya kuhifadhiwa Qur’an ni kuandikwa. Licha ya kuhifadhiwa katika vifua, Qur’an iliandikwa kwenye vifaa vya kuandikia vilivyokuwepo zama hizo, zikiwemo ngozi, na mawe yaliyotakata.

Mtume aliwachagua waandishi mahiri miongoni mwa Maswahaba zake ambao waliiandika Qur’an katika vifaa kama hivyo, na kuhakikisha kuwa hakipotei kitu. Hali ilikuwa hivyo hivyo katika mfululizo wote wa kushuka Qur’an, na katika vipindi vyote vya utume, kipindi cha Makka (miaka 13) na kipindi cha Madina (miaka 10).

Baadhi ya waandishi wa Mtume
Mtume alikuwa na waandishi wengi sana waliokuwa wakiiandika Qur’an. Sheikh Abubakr Jabir Aljazaairy (Mungu amrehemu) amewataja waandishi 22 katika kitabu chake, ‘Hadhal-habib Muhammad. Miongoni mwao ni Hawa makhalifa wanne. Abubakr, Umar, Uthman na Ali (Allah awaridhie).

Wengine ni Zaid bin Thabit, Ubay bin Kaab, Muawiya bin Abii Sufyan, Abdallah bin Zaid, Arqam bin Abi-arqam, Thabit bin Qays bin Shammaas, Handhwala bin Rabii, na wengine wengi.

Uteremkaji wa Aya/sura
Kimsingi ni sura chache tu zilizoteremka zote kamili. Hivyo basi, kila ilipoteremka Aya moja au zaidi, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) aliwaelekeza Maswahaba pakuziandika, na ilipomaliza sura aliwafahamisha kuwa, sura sasa imekwisha, na kuwataka waandike
‘Bismillah,’ kama kianzilishi cha sura nyingine. Kadhalika, kulikuwa na uwezekano sura mbili ama zaidi kuteremka kwa pamoja.

Mfano wa sura zilizoteremka kamili
Takriban sura zote fupi fupi ziliteremka kamili. Sura hizo ni pamoja na Surat Alfaatiha, Surat Alkawthar, Surat Masad, Surat Qadr, Surat Ikhlas, Surat Falaq, na Surat Nnas. Surat nyengine fupi zilizoshuka kwa mkupuo mmoja ni Surat Al-fiil, Nasr, Surat Al – Kaafiroun.

Wanazuoni wamezitaja sura nyengine ndefu zilizoshuka kwa mkupuo mmoja –licha ya ikhtilafu ndogo miongoni mwao-kuwa ni pamoja na Alkahf, An-aam, Alfat-h, Yusuf, At-tauba, Asswaff, Almursalat, na kadhalika, kama alivyoyaeleza hayo Imam AsSuyuti. Kila Maswahaba hao waandishi walipomaliza aliwataka wasome walichokiandika, ili kuhakikisha kuwa wameandika ndivyo. Kisha Sahifa (nyaraka/kopi) zilihifadhiwa katika nyumba ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie).

Mtume alifikwa na umauti Qur’an ikiwa imehidhiwa katika njia mbalimbali, ikiwemo vifuani, na maandishi. Ama kuikusanya katika msahafu mmoja, hili halikufanywa wakati wa Mtume. Jambo hili lilitokea wakati wa Khalifa Abubakr (Allah amridhie) kama tutakavyoona katika matoleo yanayofuata inshaaAllah.

Kwa nini Qur’an haikukusanywa wakati wa Mtume
Wataalamu wametaja sababu mbalimbali zilizopelekea kutokukusanywa kwa Qur’an katika msahafu mmoja wakati wa Mtume. Miongoni mwa sababu hizo ni uchache wa vifaa vya kuandikia. Pia, Maswahaba wengi walikuwa wamehifadhi Qur’an katika nyoyo zao, na wala hapakuwepo na hofu ya kupotea. Maswahaba hao ndiyo waliokuwa wakitegemewa kuirithisha kumbukumbu hiyo kwa wengine.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close