5. Ramadhan

Tuikaribishe Ramadhan kwa kujitathmini

Miaka inasogea, miezi inakatika, siku nazo zinakwenda mbio. Hili ni jambo la kushtua kwani mabadiliko ya miaka, miezi, wiki na siku ni tangazo kwa mwanadamu juu ya kupungua umri wake na hivyo kukaribia kifo.

Kasi hii ya mabadiliko ya nyakati imetajwa kama moja ya dalili za Kiyama. Imethibiti kutoka kwa Anas bin Malik (Allah amridhie) kuwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema:

“Hakitosimama Kiyama mpaka nyakati zikaribiane, mwaka utakuwa ni kama mwezi, na mwezi utakuwa kama wiki, na wiki itakuwa kama siku, na siku itakuwa kama muda wa kuungua jani la mtende.” [Tirmidhiy na Ibn Hibban].

Kukaribiana huku kwa nyakati ni jambo ambalo hakika yake ipo wazi, hivi sasa kwa sababu ukilinganisha kati ya Ramadhan ya mwaka jana na itakayokuja siku chache zijazo, utagundua ni kwa kiasi gani dunia inavyokimbia kwa kasi ya ajabu. Swali la msingi la kujiuliza ni je, tulifikia lengo la funga katika Ramadhan ya mwaka jana?

Mara kwa mara huwa tunakumbushana kuwa Ramadhan ni mwezi wa malezi, uliosheheni mazoezi ya kimwili na kiroho. Mazoezi haya ndiyo yanayopelekea mtu kufikia hatua nzuri ya kutekeleza maamrisho ya Allah na kujiepusha na makatazo yake wakati na baada ya Ramadhan.

Kwa sababu zimebaki siku chache kabla ya kuanza mfungo wa Ramadhan nimeona, ni vema tukumbushane kuhusu suala la kujitathmini na kujiuliza ikiwa tulifikia lengo la Ramadhan ya mwaka uliopita au la. Na je, tulitekeleza kikamilifu maamrisho ya Allah na kujiepusha na makatazo?

Bila shaka kwa baadhi yetu, jawabu ni hapana. Sababu ni kwamba, kila unapomalizika mwezi wa Ramadhan, baadhi ya Waislamu hawaendelei na ibada walizokuwa wakizifanya ndani ya Ramadhan. Wanasahau kuwa matendo mbalimbali ya kiibada wanayoyafanya ndani ya Ramadhan pia wanapaswa kuyafanya katika miezi mingine.

Swaumu huulea moyo katika Ikhlas (utakasifu wa nia), hubadilisha mwenendo wa nafsi ya mfungaji na kumfunza namna bora ya kuishi na watu. Kushindwa kutekeleza ibada baada ya Ramadhan ni kielelezo cha kuwapo kwa upungufu na kasoro katika ibada tunazozifanya ndani ya Ramadhan.

Kama tujuavyo, uhai wa mwanadamu hupitiwa na miaka, miezi, wiki, saa, dakika na sekunde. Hii ndiyo tafsiri nyepesi ya uhai wa mwanadamu. Tangu kuumbwa kwa ulimwengu watu wengi, wameshafariki na wengine mamia kwa maelfu tutaiaga dunia muda wetu wa kuishi utakapomalizika. Na kwa hakika Allah haicheleweshi nafsi pindi muda wake wa kuondoka unapowadia.

Tunamuomba Allah Aliyetukuka atujaalie kumtii yeye na atufishe hali ya kuwa ameturidhia. Siku zote watu werevu, wenye busara na akili timilifu huyatathmini mabadiliko ya nyakati na kuyaweka akilini. Ama watu walioghafilika na maisha ya dunia husherehekea kumalizika kwa miaka, miezi na siku. Wanasahau kuwa kadiri miaka inavyosonga mbele ndivyo umri wao wa kuishi unavyopungua.

Tunapozungumzia wakati katika maisha ya Muislamu tunamzindua na kumkumbusha kuwa muda si rafiki, ima autumie vizuri au aupoteze kwa kuyafanya yale yasiyokuwa na msaada kwake.

Swali ni je, tunapoikaribia Ramadhan tunajiandaa vipi kuutumia muda wetu ikiwa tulishindwa kulifanya hilo ndani ya mwezi wa Ramdhani iliyopita na hata baada yake?

Tumekuwa tunachezea wakati na kupata hasara, jambo hili litakwisha lini ikiwa hatuna makusudio na maazimio ya kweli ya kuhakikisha kuwa tunaachana na tabia ya kupoteza wakati ili tuutumie katika kuwekeza wakati wetu katika heri.

Tuache mazoea

Kufunga kwa mazoea ni moja kati ya sababu zinazopelekea watu wengi kutofikia lengo la swaumu. Yamkini, Waislamu wengi wanaofunga swaumu ya Ramadhan hujizuia kula na kunywa, pia hufanya ibada muhimu za sala, kutoa kama sadaka na kadhalika, lakini hawajizuii na madhambi ya usengenyi, kusema uongo, kufitinisha, kutukana na kuwavunjia watu heshima nk.

Kando na hao, pia wapo wanaofunga mwezi wa Ramadhan ili na wao waonekane wameidiriki ibada ya swaumu (Waislamu). Kadhalika, kuna wanaolazimika kufunga aidha kwa mashinikizo ya watu wanaowazunguka au kwa hofu ya kuitwa ‘makobe.’

Bila shaka hawa ni katika wale wanaopata hasara kwa kuwa funga zao zinakosa unyenyekevu na Ikhlas, na hivyo kutolipwa thawabu siku ya Kiyama (hesabu).

Tufunge kwa ikhlas

Kama zilivyo ibada nyingine, swaumu ya Ramadhan pia ina nguzo, sharti na sunna zake. Zaidi ni kwamba, ibada yoyote anayoifanya Muislamu ni lazima iambatane na Ikhlas, kwani Mwenyezi Mungu hakubali amali ya mtu ila ile ambayo imekusudiwa kwake, yaani Ikhlas, moyo msafi, pamoja na kuzingatia mwenendo wa Mtume wake Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie).

Ikhlas itakapoondoka, funga ya mja hugeuka kuwa amali isiyokuwa na malipo yoyote kwa Mwenyezi Mungu. Allah Aliyetukuka anasema:

“Na hawakuamrishwa kitu ila wamuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumtakasia Dini, wawe waongofu, na washike sala, na watoe zaka. Na hiyo ndiyo dini madhubuti.” [Qur’an, 98:5–6].

Katika kuhimiza suala la Ikhlas katika ibada ya funga, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema:

“Atakayefunga Ramadhan kwa imani na kwa kutegemea malipo kutoka kwa Allah, basi mtu huyo atasamehewa madhambi yake yaliyopita.” (Bukhari na Muslim).

Kwa upande mwingine, mtu anaweza kufunga swaumu ya Ramadhan, lakini asifaidike na funga yake. Abu Hurayra (Allah amridhie) alimsikia Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) akisema:

“Inawezekana mtu anayefunga asipate chochote katika funga yake isipokuwa njaa na yule anayesimama usiku kusali asipate chochote isipokuwa uchovu.” (Nasai).

Kwa mujibu wa Hadithi hii, ni wazi kuwa katika jamii yetu wapo watu wanaofunga mwezi mzima wa Ramadhan lakini swaumu zao zinakwenda patupu kwa sababu ya kukosa Ikhlas. Hivyo basi, ni muhimu sana kutambua nafasi ya Ikhlas katika ibada zetu ili tupate ujira mwema Siku ya Kiyama.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close