5. Ramadhan

Swaumu, chuo cha tabia njema na Uchamungu

Usama bin Sharyk (Allah amridhie) amehadithia kwamba, siku moja walikuwa wamekaa na Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie), ghafla wakaja watu na kusema: “Yupi kati ya waja wanaopendwa zaidi na Allah?” Mtume akawaambia: “Ni yule mwenye tabia nzuri.” [Twabraniy, na ameisahihisha Albaniy].


Tabia ni hitajio la kimaumbile na la kimsingi katika maisha ya mwanadamu kwa sababu ndiyo inayoleta nidhamu. Kadhalika, tabia ni njia bora inayoweza kumfikisha mtu katika utii wa Allah na utekelezaji maagizo yake.


Mafundisho ya tukio
Tukio hili linatuonesha uzito wa tabia njema na nafasi yake katika Uislamu. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Mche Allah popote ulipo, na fuatisha baya ulilofanya kwa kufanya jema, (hilo jema) litafuta hilo baya, na changanyika/ishi na watu kwa tabia njema.” [Tirmidhiy].

Tabia njema ni mhimili muhimu katika kuimarisha uhusiano na mafungamano baina ya watu, na pia humpendezesha sana Allah. Mtume ametufahamisha kuwa, miongoni mwa malengo makubwa ya kutumwa kwake ni kukamilisha (kutimiza) tabia njema, kama anavyothibitisha: “Hakika nimetumwa ili nikamilishe tabia njema.” [Ahmad]. Kwa maana hiyo, tabia njema ni moja kati ya malengo makuu ya kutumwa Nabii Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie).


Ramadhan na tabia njema
Ramadhan ni chuo cha mafunzo ya tabia njema kwa sababu, katika mwezi huo mja analazimika kujiepusha na mambo yenye kufunguza ili kulinda swaumu yake. Baadhi ya mambo hayo yanafungamana moja kwa moja na suala la tabia.


Hii ni kwa sababu, ndani ya Ramadhan mja anajifunza ukarimu, huruma, kusubiri, uvumilivu na kusaidia watu. Kupitia Ramadhan, Waislamu hufanya hima yakujifunza mambo mbalimbali kuhusiana na ibada za funga, sala, zaka, kusoma Qur’an, pia hujilazimisha kuacha maovu.


Kwa upande wa subira, huwa na nguvu zaidi pale inapokuwa mja amesubiri na kuvumilia katika jambo ambalo nafsi inalipenda. Mambo mengi ambayo waja wametakiwa kujizuia nayo ndani ya funga ni mambo ambayo nafsi inayapenda. Ndani ya funga, nafsi inatakiwa kuvumilia kwa kudumu juu ya utii wa Mola wake, inatakiwa ivumilie kwa kuacha maasi na inatakiwa ivumilie machungu yanayotokana na funga yakiwamo njaa na kiu.


Kujizuia na machafu
Katika ibada ya funga, mja anajizuia na baadhi ya mambo yaliyo halali katika mchana wa mwezi usiokuwa wa Ramadhan kama vile kula, kunywa pamoja na kujamiiana na mke wake. Hii ni njia ya kuizoesha nafsi namna ya kujizuia na yale ambayo Allah ameyakataza na kuyawekea mipaka katika maisha ya mwanadamu.


Mtume (rehema na amani za Allah zimshukie) amesema: “Mtu asiyeacha kusema uongo na kuufanyia kazi, Allah hana haja na kuacha kwake mtu huyu
kula na kunywa.”


Na pia amesema Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie): “Ikiwa siku mmoja wenu amefunga asiongee maneno machafu wala asipige makelele, wala asifanye vitendo vya kijinga. Na ikiwa mtu atamtukana au kumpiga, basi amwambie, ‘Mimi nimefunga.’”


Haya ni malezi bora ambayo yanapatikana katika ibada ya funga, yakilenga kuidhibiti nafsi na kuzuia viungo dhidi ya mambo aliyoyaharamisha Allah. Hivyo, Ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa, viungo vyote vinafunga katika yale aliyoyakataza Allah. Ikiwa umefunga katika vile alivyovihalalisha Allah, ni wajibu pia kufunga katika vile alivyoviharamisha.


Funga ndiyo ponya ya matamanio yote, ni ibada yenye taathira kubwa katika kuhifadhi na kulinda viungo, ndiyo nguvu ya ndani inayoweza kuidhibiti nafsi na kudhibiti viungo katika yale aliyoyakataza Allah. Hata hivyo, hayawezi kupatikana haya isipokuwa kwa mambo matatu, kujizuia na matamanio ya tumbo na tupu, kuvumilia kwa kuacha maasi ya aina zote na kufunga kwa ajili ya kumtii Allah kwa kumtakasia nia na wala si kufunga kwa ajili ya mazoea au kuiridhisha jamii.


Kuilea nafsi katika kuvidhibiti viungo
Tuchukue mfano wa kiungo kimoja ambacho kinadhibitiwa sana katika funga, nacho ni ulimi. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amekataza mwenye kufunga kutukana, kupiga makelele, kuzungumza mazungumzo ya kijinga, kusengenya na mengineyo.


Haya yote ni matendo ya ulimi, kipande kidogo cha nyama ambacho Allah Aliyetukuka kwa uwezo wake amekipa uwezo wa kusema, lakini kinaweza kuwa ni sababu ya kuangamia kwa mja au kuokoka na adhabu za Allah.


Mtume (rehema na amani za Allah zimshukie) amesema: “Muislamu wa kweli ni yule ambaye wamesalimika Waislamu kutokana na ulimi wake na mkono wake.” [Muslim]. Na akasema tena: “Yeyote anayemwamini Allah na siku ya mwisho azungumze maneno mazuri au anyamaze.” [Bukhari na Muslim].


Kuilea nafsi katika tabia ya ukarimu na kufanya wema
Kusaidia wengine ni miongoni mwa matunda yanayotokana na ibada ya funga. Kitendo cha kushinda na njaa mchana kutwa, katika utekelezaji wa ibada ya funga, humkumbusha mwanadamu hali halisi ya maisha ya mafukara, masikini na wenye shida.


Hili ni jambo ambalo linaacha taathira kubwa katika nafsi ya mja baada ya Ramadhan na kumfanya awe na huruma na mwenye kupenda kuwafanyia ihsani watu kutokana na mazoea mazuri aliyokuwa nayo ndani ya Ramadhan.


Njaa humfanya mwanadamu awe na tabia ya kufanya hisani, ukarimu na kusaidia wengine. Ni kwa kuzingatia hilo, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alikuwa ni mkarimu kushinda watu wote. Ukarimu wa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ulikuwa ukiongezeka maradufu katika mwezi mtukufu wa Ramadhan, ambapo Malaika Jibril alikuwa
akishuka kwa ajili ya kumsomesha Mtume Qur’an.


Ibn Abbas (Allah amridhie), anasimulia: “Mtume wa Allah alikuwa karimu mno katika mambo ya heri kushinda upepo
uvumao kwa kasi.” [Bukhari].

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close