5. Ramadhan

Shura ya Maimamu: Waislamu tusaidiane mahitaji ya Ramadhan

Shura ya Maimamu Tanzania imewakumbusha Waislamu kuwasaidia wenzao wenye shida ili waweze kukidhi mahitaji yao muhimu ndani ya mwezi wa Ramadhan yakiwamo yale ya futari na mengineyo.

“Ni muhimu kuwasaidia wenye shida ili waweze kuimudu Ramadhan; na pia tuwatembelee wagonjwa majumbani, hospitalini na wafungwa magerezani,”

ilisema sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa na Katibu wake, Sheikh Ponda Issa Ponda, Kuhusu magereza, barua hiyo imeshauri mamlaka kuu za mahakama ziweke utaratibu wa kurahisisha utoaji wa dhamana kwa watuhumiwa ili kupunguza msongamano magerezani, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupambana na Covid-19.

Katika barua hiyo, Sheikh Ponda pia alisisitiza umuhimu wa wananchi kuwa na maarifa sahihi kuhusu maradhi haya. Alisema, ni bora na muhimu wananchi wapewe elimu zaidi ili wajue mbinu za kujikinga na maambukizi.

Aidha, Sheikh Ponda aliwataka Waislamu kuutumia ipasavyo mfungo wa Ramadhan kwa kuomba toba na kuzidisha matendo mema ili kupata nusra ya Mwenyezi Mungu.

“Tuzingatie kuwa Allah hawezi kutupa chochote kama hatutendi na kuomba yanayostahiki kuombwa. Ikiwa tutafanya hivyo ndani ya Ramadhan hii kwa Ikhlas na umoja, Allah atapokea maombi yetu na kuleta nusra katika matatizo yanayotukabili ndani ya muda mfupi,” aliongeza kusema Sheikh Ponda.

Kadhalika, Sheikh Ponda alibainisha kuwa matendo yanayoweza kuwapa baraka Waislamu katika mwezi wa Ramadhan ni pamoja na kuwakumbuka wale wanaokabiliwa na mateso mbalimbali kutoka kwa watu madhalimu ulimwenguni kote.

“Watu wa Nabii Musa waliomba siku za kawaida wakakubaliwa. Itakuwaje kwa wale watakaofanya maombi ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan? Kama watu wa Musa walikubaliwa, itakuwaje kwa wale watakaoomba katika sala za jamaa kwa siku 30?” alihoji.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close