5. Ramadhan

Ramadhan, tuijue Qur’an

Qur’an kuteremka kwa herufi saba

Kabla ya kumuelewesha msomaji makusudio ya kuteremka Qur’an kwa herufi saba, kwanza tuirejee habari iliyonukuliwa kutoka kwa AbdirRahman bin Abdil-Qaari. AbdirRahman alimsikia Umar akiHadithia: “Nilimsikia Hisham bin Hakim akisoma Sura ya Alfurqan kinyume na niisomavyo mimi kwa mujibu wa alivyonifundisha Mtume. Nikamuachia mpaka alipomaliza.

Nikamkunja kwa nguo zake na kumleta mbele ya Mtume. Na kusema, ‘Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu! Mimi nimemsikia huyu akisoma kinyume na ulivyonifundisha.’ Mtume akamwambia Hisham, ‘Hebu soma.’Akasoma vile nilivyomsikia akisoma. Mtume akasema, ‘Sawa. Hivi ndivyo ilivyoteremshwa.’ Kisha akaniambia, ‘Haya na wewe soma. ’Nikasoma kisha akasema, ’Sawa, hivi ndivyo ilivyoteremshwa. Hii Qur’an imeteremshwa kwa herufi saba, basi someni kwa namna itakavyokuwa rahisi kwenu.” [Taz: ‘Al-ahruf sab-ah lil Qur’an’ uk.11]

Kutokana na nukuu hii, tunajifunza kwamba, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) aliwafundisha Maswahaba kuisoma Qur’an kwa herufi [lahaja] mbalimbali ambapo Maswahaba hao nao walitofautiana katika kuichukua kutoka kwake. Kuna wengine waliichukua kwa herufi moja, wengine mbili, wengine zaidi. Mtume alipofariki na Maswahaba kutawanyika katika miji mbalimbali, na wao waliwafundisha wanafunzi wao kwa mujibu wa walivyoinukuu kutoka kwake. Hivyo basi, wanafunzi hao walitofautiana pia katika kuichukua kwa walimu wao na katika kuisoma pia.

Maana ya kushuka Qur’an kwa herufi saba

Herufi saba maana yake ni njia saba katika kutofautiana mapito (usomaji) wake huku mwandiko [mchoro wa neno wa asili] ukiwa ni mmoja. Tofauti hizi zilitokana na lahaja za lugha ya Kiarabu, lengo likiwa ni kurahisisha kuisoma kwa wale watamkao lugha ya Kiarabu kwa lahaja zao ambao kwa mara ya kwanza ndiyo waliipokea Qur’an.


Katika Hadithi tunajifunza kuwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alimuomba Allah amruhusu kuwasomea wanafunzi wake kwa herufi hizo ili iwe rahisi kuitamka. Mtume alijua kwamba, wangelitakiwa waisome kwa herufi ama lahaja moja tu, ingelikuwa usumbufu kuitamka kwa usahihi. Vilahaja hivi ambavyo vilikuwa na njia zake kuu saba ndivyo huitwa ‘Herufi saba.’ Mtume alivifahamu na kuwa na uwezo kuvitumia vyote.

Kutoka kwa Abdallah bin Abbas anasema: “Nimemsikia Mtume wa Allah akisema: “Jibril alinisomea Qur’an kwa herufi [lahaja] moja. Nilimuomba anizidishie akanizidishia mpaka zikafika herufi saba.”[Bukhari; pia katikaTaarikhul– Qur’an juz 1 uk77].

Kwa mfano aya ya 259 katika sura ya pili imekuja: “Wandhur ila-idhaam kayfa nunshizuhaa…” wengine imekuwa wepesi kuisoma: “Wandhur ila-idhaami kayfa nunshiruhaa…” hizi ni herufi mbili zenye asili moja na maana za karibu sana. Mfano mwengine ni hitilafu katika umoja, uwili na uwingi wa neno, mfano: “Walladhynahum liamaanaatihim waah-dihim raaoun,” kwa wengine imesomwa: “Liamaanatihim…”

Jambo lingine la msingi ambalo ni vyema msomaji wetu kulifahamu ni kwamba, kuteremka Qur’an kwa herufi saba haina maana kuwa kila neno katika Qur’an linasomwa kwa herufi [lahaja] saba. Hitilafu hiyo imetokea kwa maneno machache, na ni pale tu zilipokosana lahaja za lugha ya Qur’an [Kiarabu].
Tofauti ya hizo lahaja za Kiarabu ni sawa tu na tofauti ya lahaja za lugha ya Kiswahili. Kuna Watanga, Wapemba, Watumbatu, Wazaramo, Wamakunduchi, Wamombasa na wengine wote watumiao Kiswahili.

Licha yakukosana katika lahaja zao, sehemu kubwa ya maneno ya lugha yao [Kiswahili] hulingana na hivyo wanaelewana.

Tunalojifunza
Inatubainikia kwamba, hapo mwanzo, Qur’an iliteremshwa kwa lahaja moja (ya Kikureish). Mtume akaomba iteremshwe kwa zaidi ya herufi moja, akaongezewa mpaka zikafika saba, naye akazifundisha kwa Maswahaba wake, kama tulivyoona.
Kutokana na hofu ya visomo, (herufi) hizo kuzua mtafaruku na kuwa sababu ya maadui kukichezea kitabu cha Mwenyezi Mungu, Khalifa wa tatu, Swahaba Uthman –kama tutakavyoona- aliwarudisha Waislamu kwenye kuisoma Qur’an kwa herufi [lahaja] ya Kikureish.

Uthman aikusanya Qur’an
Baada ya kuyafahamu hayo, twende sasa tukajifunze jinsi Qur’an ilivyokusanywa wakati wa Amirul-Muuminina, Uthman (Allah amridhie). Ukusanyaji wa Qur’an ulifanyika tena wakati wa utawala wa Khalifa wa tatu, Uthman (Allah amridhie). Haja ya kuchukua hatua hiyo ilikuwa kama ifuatavyo. Katika vita vya Armenia na Azerbaijan huko pande za Iraq, Hudhayfa bin Alyamaan mmoja wa Maswahaba waliohudhuria alikuta hitilafu kubwa ya usomaji wa Qur’an. Hali hii ilipelekea Waislamu kusingamana na kukufurishana.

Aliporudi tu, Hudhayfa alimfuata Amirul-Muuminin Uthman na kumuhabarisha. Jambo hili liliwashughulisha Maswahaba wote, wakaogopa kusijezuka fitna ya kubadilisha kisomo na makusudio ya Qur’an.

Katika Hadithi, Anas (Allah amridhie) anasimulia kwa kusema: “Hudhayfa alimwambia Uthman, ‘Udiriki umma kabla haujahitalifiana [juu ya kitabu chao] kama walivyohitalifiana Wayahudi na Wakiristo.’ Ndipo Uthman akamtuma kwa Mama Hafswa (Allah amridhie) akimuomba amletee Msahafu [wa mwanzo] akiahidi kuurudisha kwake tena.’

Khalifa Uthman achagua watendaji makini
Khalifa Uthman aliwachagua Maswahaba makini wakiwemo Zaid bin Thabit, Abdullah bin Zubeir, Said bin Al-as na AbdurRahman bin Alharith bin Hishaam, na kuwaagiza wanukuu kutoka Msahafu wa asili nakala kadhaa, kisha Uthman akaurudisha Msahafu wa asili kwa Mama wa Waislamu, Hafsa. [Taz: ‘Mabahith fii uluum al – Qur’an,’uk 129-130].
Hapo ndio wakakubaliana kuunukuu Msahafu wa Abubakr na wakakubaliana wawakusanye watu wote kwenye usomaji uliyothibiti kutoka kwa Mtume kwa herufi moja.

Wema waliopita walivyosifu juhudi za Uthman
Hatua aliyoichukua Khalifa Uthman iliungwa mkono na kupongezwa sana tokea wakati wa Maswahaba wenzake hadi sasa. Kutokana na simulizi ya Suweid bin Ghafla anasema, Ali bin Abii Twalib (Allah amridhie) anasema: “Msimtaje Uthman ila kwa kheri, Naapa kwamba, hakulifanya hili alilolifanya (kuwakusanya watu juu ya usomaji mmoja) ila kwa makubaliano ya kundi kubwa miongoni mwetu.

Anaendelea Uthman kusema kuwa, katika kikao walichokaa (Uthman) alisema: “Nimepata taarifa yakwamba, baadhi ya Waislamu wanadai [wanabomoana] na kusema, ‘Usomaji wangu ni bora kuliko usomaji wako,’na hili huenda likawafanya wakufurishane.” Ali akaendelea kusema: “Tukamuuliza, ‘Sasa unasemaje?’Uthman akasema, ‘Mimi naona tuwakusanye watu juu ya kisomo [herufi] moja tu; pasiwe tena mifarakano wala hitilafu.’ Tukasema, ‘Ni vyema kabisa ulivyoona’” [Abuu Daud, pia angalia Mabahith uk. 131].

Idadi ya nakala zilizonukuliwa
Inasemekana kuwa nakala hizi zilikuwa saba na zilitumwa kwenye miji mikuu ya Waislamu zama hizo, Nayo ni Makka, Sham, Basra, Kufa, Yemen, na Bahrain, Na nakala moja ilibaki Madina. Uthman aliagiza nakala hizi zitumike na Misahafu yote isiyokuwa hii ichomwe moto. Misahafu hii kwa sasa inaaminika kwamba, haipatikani tena katika ulimwengu huu.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close