5. Ramadhan

Ramadhan, mwezi wa jitihada!

Mtume wa Mwenyezi Mungu (rehema za Allah na amani zimshukie) aliwahutubia Maswahaba zake siku ya mwisho kabisa ya mwezi wa Shaaban, akisema: “Enyi watu! Mwezi Mtukufu umewajia, mwezi uliobarikiwa, mwezi ambao ndani yake kuna usiku ulio bora kuliko miezi elfu moja, mwezi ambao Allah ameufanya lazima kwenu kufunga mchana, kusali usiku. Yeyote atakayejikurubisha kwa Allah kwa kufanya ziada yoyote ya matendo mema katika mwezi huu, atapata malipo sawa na kufanya kitendo cha wajibu wakati mwingine wowote, na yeyote atakayefanya kitendo cha wajibu (mwezi huu) atalipwa mara 70 zaidi. Ni mwezi wa subira na malipo ya subira ni Pepo. Ni mwezi wa hisani, ni mwezi ambao riziki za Muumini zinaongezeka. Yeyote anayempa futari mtu aliyefunga, atasamehewa madhambi yake, na atanusuriwa na moto wa Jehanamu, na atapata malipo sawa na mtu aliyefunga, bila ya malipo yake kupunguzwa hata kidogo.” [Ibn Khuzaymah].

Imesimuliwa pia na Abu Huraira (Allah amridhie): Mtume amesema: “. . . yeyote anayefunga mwezi mtukufu wa Ramadhan kwa uadilifu wa imani na kutarajia malipo ya Allah, madhambi yake yote ya nyuma yatasamehewa. ” [Bukhari].

Huu ni mwezi ambao tunahangaika na matamanio na silika zetu. Ni mwezi ambao Muislamu anajiweka mbali na vile anavyovipenda zaidi na kutafuta ukuruba na Muumba wake. Ni mwezi ambao Muislamu anaizuilia nafsi yake na vile avipendavyo kama chakula, vinywaji, jimai na kadhalika. Anajizuilia na raha hizo ili kupata kitu kikubwa zaidi-radhi za Allah ‘Azza wa Jalla’.

Mafunzo haya ya siku 30 yameletwa ili kumuinua mtu na kumfikisha viwango vya juu zaidi vya kiroho. Hii ndiyo ile ‘Taqwa’ ambayo Mwenyezi Mungu katika Sura Baqarah ameisema: “Enyi mlioamini! Mmelazimishwa kufunga, kama walivyolazimishwa waliokuwa kabla yenu, ili mpate kumcha Mwenyezi Mungu.” [Qur’an, 2:183].

Mwezi Mtukufu wa Ramadhan unatuonesha sisi ni nani kama wanadamu. Ni binadamu tu ndiye mwenye uwezo wa kudhibiti matamanio yake na silka (insticts) kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Hiki ndicho kinachowatofautisha wanadamu na viumbe wengine wa kundi la wanyama (animal kingdom). Silka yetu ya kiroho inainuliwa kwa gharama ya silka yetu ya vitu. Hii inatufanya kuwa karibu zaidi na Allah Ta’ala na kututofautisha kama wanadamu. Kwa bahati mbaya sana, leo tunaishi katika ulimwengu ambao binadamu amekuwa mtumwa wa matamanio yake na silka – hiyo ndiyo maana hasa ya kuishi kwenye ulimwengu wa kisekula.

Ngono, fedha, kuponda raha na Israfu ya chakula, ndivyo vitu vinavyopendwa zaidi ulimwenguni. Hayo ndiyo yanayowasilishwa kama maana halisi ya mafanikio. Hayo ndiyo watu wote wanayoyatafuta katika maisha yao. Hadhi ya binadamu ulimwenguni leo imeshushwa hadi kufikia kiwango cha mnyama. Hii imeleta fitna ulimwenguni ambapo watu tofauti, makabila tofauti, rangi tofauti na mataifa tofauti wanapigana wakati wote, ili kukidhi matamanio yao ya vitu (material desires).

Uislamu, kama itikadi, umekuja kumnyanyua mwanadamu kutoka kwenye utumwa na ushindani kama huo na kumuweka katika viwango vya juu zaidi. Hiyo ndiyo thamani halisi ya kufunga na umuhimu wa Ramadhan. Ramadhan siyo mwezi tu wa kujinyima kula na kunywa. Ramadhan ni mwezi wa mafunzo ambayo yanapaswa kumkomboa binadamu kutoka kwenye utumwa wa kupenda vitu na kumuwezesha kudhibiti matamanio yake kwa kiwango cha juu kabisa ambacho kitazalisha maelewano ndani ya jamii. Hiki ndicho tunachopaswa kuvuna kwenye mwezi huu wa kupambana na nafsi zetu.
Wakati mamilioni ya Waislamu duniani kote wanafunga, kama umma, tunapaswa kuuonesha ulimwengu, hadhi yetu kama binadamu tuliojikomboa kutoka kwenye utumwa wa matamanio ya dunia, na kuelekea kwenye utumwa wa kumtumikia Mwenyezi Mungu.

Lakini Ramadhan siyo tu ni mwezi wa kuhangaika na nafsi zetu wenyewe, bali pia ni mwezi wa kuakisi mapambano mapana zaidi yanayoendelea katika ulimwengu tunaoishi. Ni mwezi ambao Allah ‘Azza wa Jalla’ ameiteremsha Qur’an Al-Kareem: “Mwezi wa Ramadhan ambao imeteremshwa humo Qur’an kuwa ni muongozo kwa watu, na hoja zilizo wazi za uongofu na upambanuzi. . . “[Qur’an, 2:185].

Tangu mwanzo, hii Qur’an imekuja kama changamoto kwa kila mfumo mwingine wa maisha katika huu ulimwengu. Qur’an haikuja ili isomwe kwa madaha na kupamba ndani ya misikiti. Wala haikuja ili kukamilisha kisomo chake kwa siku 30 za mwezi wa Ramadhan – ingawa hayo ni malengo mema. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu mwenyewe, ameileta hii Qur’an kama muongozo [Huda] na kipambanuzi [Furqan] kwa ajili ya wanadamu. Qur’an imetubainishia wazi kabisa jinsi ya kujua jema na baya, vipi tunapaswa kuridhisha matamanio yetu na silka, na vipi tunapaswa kuongoza masuala yetu ya kijamii na ya umma.

Qur’an Tukufu imeshushwa kama muongozo kwa kila kipengele cha maisha ya mwanadamu. Hii Qur’an iliteremshwa ndani ya mwezi wa Ramadhan kama rehema kwa wanadamu. Maswahaba [Allah awaridhie wote] walizipokea Aya za Qur’an pale Makka kama zilivyokuwa zikifunuliwa, na walijipanga sawa sawa kiharakati kupinga maadili yote, vigezo, sheria, kanuni, na mifumo iliyowekwa katika jamii ile, kutokana na itikadi za kikafiri.

Maswahaba waliingia kwenye mapambano ya kiakili dhidi ya fikra na mawazo yote potofu. Baada ya kupokea ukweli wa Aya za Qur’an, hawakujifunga na kusoma tu kwa madaha Aya hizo, au kubaki nayo maudhui ya Qur’an wao peke yao. La hasha! bali nguvu ya fikra za Kiislamu iliwalazimisha kuamiliana na jamii iliyowazunguka, ambayo ilijengwa kwa msingi wa fikra na mawazo potofu. Qur’an Tukufu ilionesha njia ya kitaalamu [intellectual way] ya kufuta fikra hizo kwenye jamii. Allah Ta’ala ametufunulia: “Ameangamia mwanadamu! Nini kinachomkufurisha? Kwa kitu gani amemuumba? Kwa tone la manii, akamuumba na akamkadiria. Kisha akamsahilishia njia. Kisha akamfisha, akamtia kaburini. Kisha apendapo atamfufua. La! Hajamaliza aliyomuamuru.” [Qur’an, 80:17-23].

Au wao wameumbwa pasipo kutokana na kitu chochote, au ni wao ndiyo waumbaji? Au wao wameziumba mbingu na ardhi? Bali hawana yakini.” [Qur’an 52:35-36]. “Na mali yake yatamfaa nini atakapokuwa anadidimia?”[Qur’an, 92:11]. “Ole wao hao wapunjao! Ambao wanapojipimia kwa watu hudai watimiziwe. Na wao wanapowapimia watu kwa kipimo au mizani hupunguza. Kwani hawadhani hao kwamba watafufuliwa Katika Siku iliyo kuu?” [Qur’an, 83:1-5].”Wala hii si kauli ya Shetani aliyelaaniwa. Basi mnakwenda wapi? Haikuwa hii ila ni ukumbusho kwa walimwengu wote“[Qur’an, 81:25-27]. Leo hii mapambano kama hayo bado yapo. Uislamu unashambuliwa na kudhalilishwa. Fikra za Kiislamu zinaoneshwa kama vile zimepitwa na wakati na za kale. Uislamu unaoneshwa kama dini ya kinyama, ukatili na ya vurugu.

Miaka 1400 iliyopita, Makuraish walieneza uongo kuhusu Mtume wetu Mtukufu (rehema za Allah na amani zimshukie), wakimkejeli na kumtukana. Mashambulizi hayo hayo yanatokea tena leo, hususan kwenye ulimwengu wa Magharibi. Ukafiri hauna silaha nyingine dhidi ya Uislamu zaidi ya propaganda za kijinga, matusi, kashfa, kejeli na uongo.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close