5. Ramadhan

Ole wao wanaokula kwa makusudi mchana wa Ramadhan

Kutoka kwa Abu Umama al–Bahili (Allah amridhie) amehadithia kwamba siku moja alimsikia Mtume wa Allah (rehema za Allah na amani zimshukie) akisema: “Nilipokuwa nimelala, watu wawili (Malaika) walinijia, wakanishika mikono yangu na kunichukua mpaka kwenye mlima wenye muinuko mkali kisha wakaniambia, ‘Panda mlima huu.’” Nikawajibu, ‘Siwezi kupanda.’ Wakasema: ‘Sisi tutakusaidia.’”

Hatimaye Mtume na wale watu wawili walipanda mlima, na walipofika katikati wakasikia sauti za kilio cha kutisha. Mtume akawauliza:

“Ni kelele gani hizo?” Watu wale wakamjibu: “Hizo ni kelele za watu wa motoni.” Kisha watu wale wakamchukua Mtume na kwenda naye upande mwingine. Walipofika huko wakakuta watu wametundikwa kwa visigino vyao (kichwa chini miguu juu) huku wakivuja damu nyingi mdomoni. Mtume akawauliza: “Ni akina nani hawa?” Wakasema: “Hawa ni wale wanaofungua (swaumu) kabla ya muda wa kufuturu kuingia.” [An–Nasai].

Mafunzo ya tukio hili:

Ndoto za Mitume ni ukweli mtupu na kile wanachokiota na kukiona katika ndoto zao ni taarifa na mafundisho yaliyojificha ambayo Allah ‘Azza Wajallah’ huwadhihirishia Mitume wake kwa njia ya wahyi ili wapate kuwafahamisha wafuasi wao mafundisho sahihi ya dini.

Mitume na Manabii wa Allah (amani iwashukie) waliwaelekeza watu katika ibada ya Muabudiwa Mmoja na kuwaonya wasimshirikishe Allah na kitu chochote. Aidha wajumbe hao wa Allah waliwabainishia watu ubaya wa kuabudia masanamu na kuonesha udhaifu wa masanamu hayo. Mtume (rehema na amani ya Allah zimshukie) aliona katika ndoto yake matukio tofauti, likiwemo la kuadhibiwa watu wanaokula mchana wa Ramadhanima kwa kufungua swaumu kabla ya muda wa kufungulia au kuacha kufunga pasina sababu ya kisharia.

Watu wenye tabia hizi, siku ya Kiyama wataning’inizwa kama inavyoning’inizwa nyama ilotundikwa buchani kisha midomo yao itapasuliwa pembeni huku ikiwa inavuja damu nyingi.

Hii ni mojawapo ya adhabu zenye machungu makali ambazo watapewa watu waliofungua swaumu kabla ya muda na wale walioacha kufunga pasina sababu ya kisharia. Wenye kutekeleza nguzo ya funga kwa kuzingatia masharti ya swaumu na nguzo zake ndio watakaoepushwa na adhabu ya siku ya Kiyama.

Na kama tujuavyo, swaumu ni miongoni mwa masomo makuu ya vitendo (pratical) ambayo humuandaa mfungaji wa kweli kuwa mchamungu. Swaumu pia huilea nafsi ya mfungaji na kumkataza kufanya mambo yaliyoharamishwa. Hii ina maana, swaumu ni mazoezi ya kimwili na kiroho ambayo humtayarisha Muislamu kukabiliana na matukio ya ghafla, yenye kuhuzunisha na kutia simanzi.

Na kwa hakika, swaumu si kujizuwia kula na kunywa tu. Ni zaidi ya hapo. Ukiacha kujizuia kula na kunywa, tunapaswa pia kujizuia na mambo mengine ya maasi ikiwemo kusema uongo, kutukana, kusengenya, kufitinisha au kuchonganisha watu, kutazama haramu, na kadhalika. Mtume (rehema na amani ya Allah zimshukie) amesema:

“Yeyote ambaye hatoacha kusema uongo, kusengenya, kufitinisha, kutoa ushuhuda wa uongo, basi ajue kuwa Allah hana haja na swaumu yake katika kuacha chakula chake na kinywaji chake.” [Bukhari na Muslim].

Ni dhambi kubwa kula mchana wa Ramadhan

Kuacha kufunga pasina sababu za kisharia ni dhambi kubwa mbele ya Allah. Qur’an Tukufu imeyagawa madhambi katika makundi mawili. Kuna madhambi makubwa na madogo.

Madhambi makubwa Madhambi makubwa n i makosa yote ambayo Allah na Mtume wake wameyakemea na kuyalaani. Katika tukio hili, tumeshuhudia malaika wakimhabarisha Mtume kuhusu adhabu watakayoipata wale wanaokula kwa makusudi mchana wa Ramadhan. Hii ni dalili kuwa kuacha kufunga mwezi wa Ramadhan pasina sababu za kisharia ni dhambi kubwa itakayopelekea wengi kuingia matatani siku ya Kiyama.

Akitaja orodha ya madhambi makubwa yenye kumchukiza Allah, Imam Dhahabi (Allah amrehemu) katika kitabu chake kiitwacho ‘Alkabaair’ (madhambi makubwa) amesema: “Dhambi ya kumi ni kula mchana wa Ramadhan bila udhuru wa kisharia.”

Imam Dhahabi anaendelea kusema kuwa mtu ambaye amethibitika kula mchana wa Ramadhan bila udhuru wa kisharia, Kadhi (Hakimu) wa eneo hilo anatakiwa ampe adhabu ya ta’adhiir (yani amuadhiri na kumfedhehesha mbele za watu) ili wengine wapate kuogopa kula mchana.

Tuipe Ramadhan haki yake

Mwezi wa Ramadhan una fadhila kubwa na hadhi ya kipekee ukilinganisha na miezi mingine. Hivyo, Waislamu tunapaswa kuilinda hadhi hii kwani hata baadhi ya wasiokuwa Waislamu huacha kufanya maasi kila inapoingia Ramadhan.

Wasiokuwa Waislamu wanafanya hivyo kwa sababu wanaamini kula mchana wa Ramadhan ni laana, uasi, utovu wa adabu na kutoheshimu maagizo ya Mwenyezi Mungu.

Watu wengi huacha kufunga kwa visingizio mbalimbali ili wapate sababu ya kula mchana wa Ramadhan. Kama Waislamu tuna wajibu wa kuhakikisha ndugu na jamaa zetu wa karibu wanatekeleza ibada ya funga, na ikitokea mtu ameacha kufunga basi awe na udhuru wa kisharia unaomruhusu kula mchana wa Ramadhan na siyo kufuata matamanio ya nafsi yake.

Umakini unahitajika wakati wa kufuturu na kula daku Mtume (rehema na amani ya Allah imshukie) amesema:

“Watu wataendelea kuwa katika kheri madhali watakuwa wanaharakisha kufuturu.” [Bukhari na Muslim]. Katika ufafanuzi wake kuhusu Hadith hii, Sheikh Bassamu (Allah amrehemu) amesema: “Kuchelewa kufuturu ni tabia ya Mayuhudi. Mayahudi huchelewesha futari hadi pale zinapochomoza nyota.” [Taz: ‘Taysiirul – Allam’].

Kuchelewesha daku

Mtume ametuambia: “Kuleni daku, kwani ndani yake kuna baraka.” [Bukhari na Muslim]. Na katika hadith iliyosimuliwa na Abu Sa’id Al–Khudriy (Allah amridhie), Mtume (rehema na amani ya Allah zimshukie) amesema: “Daku ni mlo uliobarikiwa, hivyo usiupuuze japo kwa fundo la maji kwani Allah na Malaika wanamrehemu mwenye kula daku.” [Ahmad]. Kula daku ni Sunna iliyothibiti kutoka kwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie). Na wakati bora wa kula daku ni kabla ya sala ya Alfajiri. Kutoka kwa Zaid bin Thabit (Allah amridhie) amesema, walikula daku pamoja na Mtume wa Allah (rehema za Allah na amani zimshukie), kisha Mtume akanyanyuka kwenda kuswali. Zaid akamuuliza Mtume: “Kulikuwa na muda gani baina ya iqama na daku?” Mtume akamwambia: “Kama aya hamsini hivi.” [Bukhari].

Hadith hii tukufu ni dalili kuwa imesuniwa kuchelewesha kula daku hadi muda kidogo kabla ya sala ya Alfajiri, kwani kitambo cha Mtume wa Allah na Zaid kumaliza kula daku na kuingia katika sala ilikuwa ni kiasi cha mtu kusoma aya hamsini (50) za Qur’an Tukufu kwa kisomo cha wastani; si cha haraka wala cha kuvuta sana.

Hatahivyo, pamoja na umuhimu huu wa kuchelewa kula daku na kuwahi kufuturu, tunapaswa kuzingatia muda sahihi wa kula daku na futari. Iwapo tutafungua swaumu nje ya wakati uliowekwa kisharia tutakuwa tunashirikiana na wale wanaokula mchana wa Ramadhan kumuasi Allah na hivyo kustahiki adhabu ya Allah siku ya Kiyama.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close