5. Ramadhan

Njia za kupambana na adui nafsi

Mtu mmoja aliyekuwa akifanya biashara ya tende katika mji wa Madina alijiwa na mwanamke mrembo aliyehitaji kununua tende, shetani akamtia wasiwasi muuza tende na kumpambia yule mwanamke mrembo akitaka kufanya naye zinaa. Muuza tende alimwambia mwanamke yule: “Nyumbani kwangu kuna tende nzuri zaidi ya hizi.” Hivyo wote wawili wakaongozana kuelekea nyumbani kwa muuza tende.

Punde baada ya kuingia ndani, muuza tende alianza kumkumbatia mwanamke yule na kumbusu, lakini akazinduka ghafla na kusitisha mpango wake huo muovu. Mwanamke huyo alikuwa anaishi peke yake nyumbani kwani mumewe alikuwa amekwenda kupigana jihadi. Katika hali isiyotarajiwa, muuza tende alijikuta akielemewa na mawazo kutokana na makosa aliyoyafanya, hivyo akaelekea nyumbani kwa Abubakr (Allah amridhie) na kumueleza yote yaliyotokea. Abubakr akamwambia: “Tubia kwa Allah, jisitiri na hakikisha humwambii yeyote jambo hili.”

Hata hivyo muuza tende alishindwa kuvumilia hivyo akamwendea Umar bin Khattab (Allah amridhie) na kumueleza kilichotokea. Umar akarudia maneno yaleyale aliyosema Abubakr. Muuza tende hakuridhika na ushauri huo, akaona ni vema amuendee Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) na kumuelezea alichokifanya. Mtume akamwambia: “Umemfanyia hivi mwanamke ambaye mumewe amekwenda kupigana Jihad?” Muuza tende aliumizwa sana na kitendo alichokifanya hadi kutamani asingekuwa amesilimu isipokuwa siku ile, akidhani kwamba Allah atamuingiza motoni.

Mtume alikaa kimya kwa muda mrefu akiwa ameinamisha kichwa chake chini, Allah akamteremshia aya hii:

“Na simamisha sala katika ncha mbili za mchana na sehemu ya kwanza ya usiku. Hakika mema yanaondosha maovu. Huu ni ukumbusho kwa wanaokumbuka.” [Qur’an, 11:114].

Mtume alimsomea aya hii muuza tende, naye akafurahi sana na kupata faraja na utulivu wa moyo (nafsi). Baadhi ya Maswahaba wakamuuliza Mtume:

“Ewe Mjumbe wa Allah! Hilo ni kwake tu (huyo muuza tende) au ni kwa watu wote? Mtume akasema: “Ni kwa ajili ya watu wote.” [Tirmidhi].

Mafunzo ya tukio hili:

Wanawake wadumishe sitara ya hijab Mwanamke anapaswa kuvaa hijabu ya kisharia muda wote kama alivyoamrishwa na Allah ‘Azza Wajallah’:

“Ewe Nabi! Waambie wake zako na mabinti zako, na wanawake wa Waumini wajiteremshie shungi zao. Hivyo kunapeleka karibu zaidi watambulikane (kwa heshima) wasiudhiwe. Na Allah daima ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.” [Qur’an, 33:59].

“Na waambie waumini wanawake wainamishe macho yao na wahifadhi tupu zao, na wala wasidhihirishe mapambo yao isipokuwa yale yanayodhihirika. Na waangushe shungi zao mpaka vifuani mwao.” [Qur’an, 24:31].

Kwa muktadha huo, sitara ya kisharia inahitajika zaidi kwa mwanamke hasa katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhan ili kulinda swaumu yake na za wengine. Katika tukio hili, tumeshuhudia urembo wa mwanamke ulivyoleta madhara na ushawishi kwa mtu mwema (muuza tende) mpaka akakaribia kufanya kitendo kichafu cha zinaa. Ni kwa ajili hii Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) akasema:

“Sijaacha baada yangu fitna yenye kudhuru wanaume zaidi kuliko (fitna ya) wanawake.” [Bukhari na Muslim].

Hatari ya kukaa faragha na mwanamke asiye maharimu

Faragha ni moja kati ya vishawishi vikubwa vya maasi. Mtume amesema:

“Asikae faragha mwanamume na mwanamke ila awe pamoja na maharim wake (ndugu asiyeweza kumuoa).” [Bukhari na Muslim].

Tukio hili linaonesha hatari ya mwanamume kukaa faragha na mwanamke ambaye si maharim wake. Ukirejea katika tukio hili, utabaini kuwa yule muuza tende alitafuta faragha ili afanye kile alichodhamiria (zinaa), lakini Allah ‘Azza Wajallah’ kwa taufiki yake alimzindua na hatimaye akasitisha mpango wa kutaka kuzini.

Tahadhari na kuingia katika nyumba za watu

Wanawake wanatakiwa wachukue tahadhari pindi wanapoitwa katika nyumba za watu na wahakikishe wanafuatana na ndugu, jamaa au waume zao kila wanapokwenda katika nyumba za watu. Mwanamke hapaswi kumuamini mwanamume asiye maharim wake hata kama ni mtu mwema sana.

Hii ni kwa sababu, kimaumbile mwanadamu ni kiumbe mwenye tabia ya kufanya makosa bila kutegemea hasa pale anaposhawishika kufanya uovu.

Kumbuka nawe una ndugu na jamaa

Pindi unapodhamiria kufanya uchafu wa zinaa na mke, dada, mama au bint wa mtu, ni vizuri ukakumbuka kuwa nawe una ndugu na rafiki zako ambao abadan huwezi kukubali waziniwe.

Epuka mambo yanayopelekea kufanya maovu

Kuna njia nyingi zinazopelekea mtu kumuasi Allah ndani ya mwezi mtukufu wa Ramadhan. Nyingi ya njia hizo zinatokana na mambo ya pumbao kama vile kujenga urafiki na watu waovu, kutazama filamu hasa zenye maudhui yanayopelekea kwenye matamanio na kusikiliza/ kutazama muziki.

Mambo mengine yanayopelekea mtu kumuasi Allah ndani ya mwezi wa Ramadhan ni pamoja na kufuatilia mambo ya mitandaoni pasina kuzingatia mipaka ya kisharia, kushiriki michezo ya pumbao, kukaa vijiweni na kuzungumzia mambo yasiyo ya uchamungu au kubishana na watu juu ya mambo yanayohusu soka na michezo mingine.

Kupambana na vishawishi vya nafsi

Miongoni mwa mambo yanayohitaji nguvu kubwa na uangalifu maalumu ni suala la kupambana na vishawishi vya nafsi. Kwa hakika hili si jambo jepesi, ni jambo linalohitaji taufiq ya Allah na kujibidiisha katika mambo ya kheri na kuepuka matamanio ya nafsi.

Yeyote anayetaka kuiondoa nafsi yake katika maovu ni lazima awe tayari kuacha kufanya mambo kwa mazoea. Na hii ndiyo njia pekee inayoweza kumtoa mtu katika dimbwi la maasi, upotovu, utii wa nafsi na matamanio yake na kumpeleka kwenye njia ya uongofu.

Allah anasema: “Na ama yule anayeogopa kusimamishwa mbele ya Mola wake Mlezi, na akajizuilia nafsi yake na matamanio. Basi huyo pepo itakuwa ndiyo makazi yake!” [Qur’an, 79:40–41].

Tusiwe wanyonge mbele ya maasi

Katika tukio hili, tumeshuhudia udhaifu mkubwa aliokuwa nao muuza tende katika kuyakabili maasi.

Inasikitisha kuona baadhi ya watu wamejisalimisha kwa shetani na kuyafanya maasi kuwa ni sehemu ya maisha yao. Jambo hili lina madhara makubwa kwa mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla, hasa ikizingatiwa kuwa binadamu ni kiumbe pekee aliyeumbwa na ufahamu mkubwa kuliko viumbe wote.

Ili tusiwe wanyonge (dhaifu) mbele ya maasi ni lazima tuweke maazimio ya kutubia na kutorejea tena katika maasi. Hii ni hatua muhimu na nzuri itakayotuwezesha kupata msaada wa Allah ‘Azza Wajallah’ na kuyaepuka maasi.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close