5. Ramadhan

Namna ya kumshirikisha mtoto katika neema za Ramadhan

Watoto hasa wale wenye umri mdogo sana, hujifunza kwa kutenda. Huwaona wakubwa wao wanavyofanya kisha na wao wanawaiga. Ni kwa sababu hii ndio maana michezo mbalimbali (role play) hutumika kama methodolojia muhimu ya kufundishia watoto wadogo hususan wale walio chekechea hadi shule ya msingi.

Ni kwa msingi huo pia, mtoto hujifunza kufunga swaumu kwa kuiga. Nalo hili ni jambo muhimu. Ijulikane kuwa, ingawa funga si wajibu kwa mtoto! Kwa Mzazi asitegemee kuwa, kama mtoto atakuja kufunga ghafla baada ya kufikia baleghe
iwapo kama hakuanza kuzoeshwa taratibu akiwa mtoto.

Ikiwa ni nguzo ya nne ya Uislamu, ni muhimu kwa watoto waeleweshwe umuhimu wa funga na umuhimu wa mwezi huu mtukufu. Licha ya kuwa ni ibada yenye malipo makubwa, funga pia inaweza kusaidia kumjenga mtoto katika tabia njema.

Funga inafundisha uaminifu, kwa sababu mtu anaweza kula na akadai amefunga bila wengine kujua. Kuwa na fursa ya kufanya hivyo lakini usifanye, huo ni uaminifu. Pia, mtoto kwa kujifunza kufunga anapata kuonja uchungu wa kushinda na njaa na kiu, na hivyo kumjenga katika kuwaonea huruma masikini.

Aanze umri gani kujifunza kufunga?
Umri ambao mtoto anaweza kuanza kufundishwa kufunga unatofautiana kati ya mtoto na mtoto. Kuna ambao wanaanza kufunga wakiwa na miaka saba au kuendelea. Vyovyote iwavyo, namna bora ya kumfundisha mtoto kufunga ni kumshawishi aanze kufunga taratibu, yaani anaweza kufunga kwa masaa machache siku ya kwanza, kisha masaa yanaweza kuongezeka taratibu.

Hata kwa mtoto anayeweza kumudu kufunga siku nzima, ni vema katika Ramadhan ya mwanzo asifunge siku zote ili kumuondolea ugumu. Kumbuka kuwa, haya kwake ni mafunzo; ni tofauti na wewe unayewajibikiwa kufunga. Kwa watoto wanaoenda shule, na wakawa na wasiwasi watashindwa kuzingatia masomo vizuri iwapo watafunga, wanaweza kuanza kujifunza kufunga siku za mwishoni mwa wiki, yaani Jumamosi na
Jumapili, ambapo wazazi watapata fursa ya kuwa nao karibu, na kuwafuatilia na kuwapa moyo.

Licha ya kuwa ni ibada yenye malipo makubwa, funga pia inaweza kusaidia kumjenga mtoto katika tabia njema

Moja ya mbinu inayotumika kumshajiisha mtoto kufunga ni kumzawadia, kwa jitihada zake. Siku yake ya kwanza, ikiwa amefunga aidha kwa saa kadhaa au siku nzima, mnunulie kitu akipendacho na umjulishe kuwa unampatia zawadi hiyo kwa sababu amekufurahisha kwa juhudi yake ya kufunga. Pia, inapendeza kumuandalia mtoto zawadi nzuri siku ya Idd, kumpongeza kwa jitihada yake ya kufunga.

Ili kumrahisishia mtoto funga, muamshe kwa ajili ya kula daku usiku. Pia, hakikisha daku inacheleweshwa kadri iwezekanavyo. Ukiacha ukweli kuwa chakula cha daku kinampa mtu nguvu ya kufunga, pia inampa mtoto ufahamu kuwa, funga ni jambo kubwa linalohitaji maandalizi. Njia nyingine ya kumsaidia mtoto kuweza kujifunza kiurahisi kufunga, ni kumtafutia vitu vya kumsahaulisha maumivu ya kiu na njaa. Inaweza kuwa matembezi mafupi au kitu chochote cha kuchezea, alimradi kiwe cha halali. Bila kufanya hivi, harufu ya chakula inaweza kumshawishi mtoto kutamani kula.

Jambo moja linaloweza kumshawishi mtoto kuvunja swaumu yake ni kukaa na watu wasiofunga. Kwa hiyo katika kumfundisha mtoto kufunga, ni muhimu pia kuchunga watu anaocheza nao.
Jaribu kutembelea ndugu ambao
wanafunga, hususan mahali penye mtoto ambaye anaweza akampa changamoto mwanao.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close