5. Ramadhan

Mwezi wa Ramadhan ni Fursa Adhimu

Kila sifa njema anastahiki Allah, Mmiliki wa ulimwengu; kisha sala na amani zimfikie Mtume wetu Muhammad rehema na amani zimshukie. Hakika tumesifiwa kuwa umma bora kwa kile kitendo cha kuamrishana mema na kukataza mabaya.

Alhamdulillah tupo katika mwezi wa Ramadhan, ambao Allah ameufadhilisha kuliko miezi mingine. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alikuwa anawaambia Maswahaba zake (Allah awarehemu) pindi yanapokuja masiku kama haya:

“Hakika umekujieni mwezi wa Ramadhan, mwezi wenye baraka, Allah amefaradhisha ndani yake funga, inafunguliwa ndani yake milango ya pepo na kufungwa milango ya moto, na wanafungwa mashetani, ndani yake kuna usiku bora zaidi ya miezi elfu, atakayeikosa heri hiyo basi huyo atakuwa amepoteza.” [Ahmad na Nasaiy katika Musnad zao].

Kufikiwa na mwezi huu ni neema kubwa kutoka kwa Allah kwa kutuongezea umri katika maisha yetu ili tuweze kujiaanda na kuupokea mwezi huu. Kuonesha umuhimu na ubora wa neema hii imekuja Hadithi iliyosimuliwa na Imam Ahmad na An- Nasai pale alipoambiwa Mtume wa Allah kuhusiana na watu watatu katika Maswahaba zake, ambapo wawili walifariki Mashahidi na akabakia mmoja wao kwa muda wa mwaka kisha naye akafariki. Huyu watatu alipata kuota amewapita wenzake katika makazi peponi. Maswahaba wa Mtume wakastaajabishwa na hili. Wakamuuliza Mtume kuhusiana na jambo hili.

Mtume akasema: “Hivi hakupata kuishi mwaka mzima na akafanya ndani yake kadha wa kadha katika sala na ukamdiriki mwezi wa Ramadhan na akafunga. Naapa kwa yule nafsi yangu ipo mikononi mwake, hakika tofauti iliyopo baina yao ni kama umbali uliopo baina mbingu na ardhi.”

Hii inatuonesha fadhila na ubora wa kudiriki masiku haya na namna gani sala na funga zinavyomnyanyua mfanyaji wa matendo hayo. Kadhalika Mtume ametutahadharisha kuingia ndani ya mwezi wa Ramadhan kisha tutoke hali ya kuwa hatujasamehewa madhambi yetu, kama ilivyokuja katika Hadithi, Mtume alipokuwa anapanda katika mimbari na kusikika akiitikia ‘Aamin’ mara tatu. Maswahaba walipomuuliza kuhusiana, miongoni mwa aliyoyasema ni kupata hasara kwa yule aliyedirikiwa na mwezi wa Ramadhan na ukaondoka bila ya kusamehewa. [Ibn Hibbaan].

Kadhalika zimekuja Hadithi takriban tatu kaika Bukhari zenye kutofautina katika matendo lakini makusidio yake ni moja.
Mtume amesema: “Mwenye kufunga Ramadhan kwa imani na kutaka radhi za Allah atasamehewa yale yaliyotangulia katika madhambi yake.” Hadithi zingine zinaeleza kuwa, mwenye kusimama katika mwezi wa Ramadhan na nyingine mwenye kusimama usiku wa Laylatul Qadri – atasamehewa yale yaliyotangulia katika madhambi yake.

Ukitazama katika Hadithi zote hizi, maneno, ‘Imani’ na ‘Ihtisab’ yamerudiwa, kwa maana mwenye kusadikisha ya kuwa Allah amemuamrisha kufunga katika mwezi huu kwa lengo la kutekeleza amri yake na kutaraji malipo na ujira kutoka kwa Allah. Na baada ya yote hayo matokeo yake ni kusamehewa madhambi yako yaliyokutangulia.

Kwa hiyo, hii ni fursa kwetu kujipinda kufanya mambo ya heri na ni fursa inayokuja kwa mwaka mara moja. Mwenye akili, siku zote, ni yule mwenye kujifanyia hesabu katika masiku haya na kuacha mambo yasiyo na faida ndani yake.

NUKTA TATU MUHIMU ZA KUJIANDAA
Katika kuukaribisha mwezi huu wa Ramadhan yatupasa tuziandae nafsi zetu kwa mambo kadhaa, miongoni mwa hayo ni.

Kuleta toba
Tuangalie ni kitu gani tumefanya katika miaka au siku zilizopita. Iwapo tumekosea, tuombe msamaha kwa Allah na kuweka azma iliyokuwa ya kweli katika nafsi zetu za kutoyarudia yale tuliyoyafanya kwani Allah ni Mwingi wa kusamehe na Mwenye huruma kama zilivyokuja Aya katika Qur’an.

Mwenyezi Mungu anasema: “Sema, ‘Enyi waja wangu waliojidhulumu nafsi zao! Msikate tamaa na rehema ya Mwenyezi Mungu. Hakika Mwenyezi Mungu husamehe dhambi zote. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.” (Qur’an, 39:53)

Kusameheana na kudumisha undugu
Kadhalika tujitahidi kuomba msamaha kwa wale tuliowakosea ili wapate kutusamehe, sambamba na hilo ukiwa ni mwenye haki ya mtu basi fanya uwezalo katika kurudisha amana ya watu kwani haki za watu zinapelekea kufisidi na kuharibu ibada. Haki za watu zinapaswa zirudi kwa wenyewe kwani ukimdhulumu mtu haki yake itakuwa umeingia katika uharamu na itapelekea dua zako kutojibiwa na Allah. Ushahidi ni Hadithi ya msafiri aliyepatwa na mavumbi, mwenye kunyanyua mikono yake mbinguni lakini kila kitu chake ni cha haramu, namna gani mtu huyu ataitikiwa dua yake? (Muslim).

Sambamba na kusameheana na watu uliowakosea, ni muhimu pia tudumishe undugu. Mahusiano mazuri na ndugu zetu kwani itazidisha mapenzi baina yenu. Usiwe tayari kuona udugu wenu unakatika kwani mtu mwenye kukata udugu haingii peponi.

Ratiba ya ibada
Mwisho kabisa yatupasa tujiwekee ratiba ya siku nzima na wala tusipoteze muda katika mambo yasiyo na faida. Kwa mfano ratiba ya kusoma Qur’an kwa mazingatio, tuweke ratiba ya kujua ni kitu gani Allah anataka kwangu mimi, kujua amri na makatazo yake, kujifunza katika visa mbalimbali, kisomo ambacho kitaleta athari katika moyo wako.

Allah anavyosema: “Mwenyezi Mungu ameteremsha Hadithi nzuri kabisa, Kitabu chenye kufanana na kukaririwa; husisimua kwacho ngozi za wenye kumkhofu Mola wao Mlezi. Kisha ngozi zao na nyoyo zao hulainika kwa kumkumbuka Mwenyezi Mungu. Huo ndiyo uwongofu wa Mwenyezi Mungu, na kwa huo humwongoa amtakaye. Na ambaye ameachwa na Mwenyezi Mungu kupotea, basi hapana wa kumwongoa. ” (Qur’an, 39:23)

Kama ilivyokuwa, mwezi wa Ramadhani ni mwezi ndani yake imeshushwa Qur’an, basi isiwe hamu yetu kusoma ili tumalize juzuu bila ya kuwa na mazingatio. Tunamuomba Allah atujaalie maandalizi yaliyokuwa mazuri katika kuuendea mwezi, atudumishe katika heri na atujaalie tuweze kuudiriki mwezi wa Ramadhan.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close