5. Ramadhan

Mwanamke wa Kiislamu na Ramadhan

Kitabu, “Mwanamke wa Kiislamu katika Ramadhan”, cha Sheikh Muhammad bin Rashid Al-Ghufayliy ni katika vitabu muhimu kuhusu ya mada hii nyeti. Kitabu hiki kinamsaidia imamu wa msikiti, mume na mwanamke mwenyewe wa Kiislamu.

Kwa kawaida, mwanamke wa Kiislamu katika mwezi wa Ramadhan hugeuzwa kuwa mpishi huku akitumia muda mwingi jikoni kupika futari na daku za kila aina kuwaridhisha wanaume na wageni waalikwa. Matokeo yake, mwanamke huyu anakosa fadhila za mwezi wa Ramadhan. Hana muda wa kusikiliza darasa, kusoma Qur’an na kufanya ibada mbalimbali kulinganisha na mwanaume. Hili ni moja ya makosa ambayo tunayafanya…Sasa endelea.

Mwanamke Muislamu nyumbani kwake
Mwanamke katika Uislamu amepewa majukumu yanayolingana na maumbile yake.

Allah Ta’ala anasema kuwaambia wanaume wa Kiislamu: “Na wawekeni mahali pale mnapoishi kulingana na uwezo wenu.” [Qur’an, 65:6].

Lakini kuwekwa huku mwanamke nyumbani anapoishi mwanaume maana yake ni kwamba, mahali stahiki pamwanamke wa Kiislamu ni nyumbani kwake. Hili linasisitizwa na Hadithi ya Mtume isemayo: “Kila nafsi katika wana wa Adam ni kiongozi. Basi mwanaume ni kiongozi wa familia yake na mwanamke ni kiongozi katika nyumba yake.” [Rejea: ‘Sunan Abuu Dawud,’ Hadithi Na. 455].

Hapa maana yake ni kuwa, mwanaume ni kiongozi mkuu wa familia na mwanamke ni kiongozi wa masuala yote ya nyumbani kwa mume wake. Kwa hiyo, wote wawili ni viongozi ingawa mwanaume ana daraja ya juu ya mwanamke na ndiye msimamizi wake huku kila mmoja akiwa na majukumu yake.

Sasa unapokuja mwezi mtukufu wa Ramadhan na mwanamke ndiye kiongozi wa masuala ya ndani ya nyumba, inabidi ajipange kuhakikisha kwamba majukumu ya nyumbani kwake hayamfanyi akakosa muda wa kufanya ibada mbalimbali ndani ya mwezi huu.

Mwanamke wa Kiislamu afanye nini basi akiwa ndani ya mwezi wa Ramadhan?
Kwanza, mwanamke wa Kiislamu ndiye anayebaki nyumbani wakati mume ametoka kwenda kutafuta riziki kwa ajili ya familia. Kwa mwanamke aliyeajiriwa, apange utaratibu wa kuhakikisha majukumu yake ya nyumbani yanatekelezwa, hata kama yeye hayupo nyumbani.

Kwa hiyo, mwanamke wa Kiislamu anapaswa awasimamie waliopo nyumbani katika watoto, ndugu zake au ndugu wa mume na watumishi wake katika suala zima la ibada akianzia na kuwahimiza kusimamisha sala. Watoto wa kiume waende msikiti ulio karibu na wanapoishi, lakini watoto wa kike wasali nyumbani kama Sunna ilivyoelekeza.

Kama kiongozi, mwanamke anawajibu wa kuwahimiza kusoma Qur’an, kusikiliza mawaidha na kujichunga na yale yote yanayovunja swaumu mchana. Pia, usiku wa Ramadhan, ana wajibu wa kuwahimiza kwenda msikitini kusali Isha na Sunna ya Tarawehe.

Hata hivyo, mwanamke hawezi kuyafanya haya yote ikiwa yeye mwenyewe amepinda na si mwenye kumcha Allah ipasavyo. Kutengenea kwake ndiyo kutengenea kwa watu wote walio chini yake nyumbani kwake; kuharibika kwake ndiyo kuharibika kwao.

Kuhusu watoto, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Muamrisheni mtoto mdogo kutekeleza sala akifikisha umri wa miaka saba, na akifikisha miaka 10 mchapeni kwa ajili ya kuacha kwake sala.” [Rejea: ‘AbuuDawud,’ Hadithi Na. 456].

Pili, ni wajibu wa mwanamke kuwahimiza watoto kufunga swaumu ya Ramadhan kama walivyowaamrisha kusali sala tano. Anasema Rabii’ah bint Mu’awadh (Allah amrehemu): “Tulikuwa tukifunga Ramadhan na watoto wetu wanafunga pamoja nasi na tunawawekea vitu vya kuchezea kutokamana na sufi (pamba), mmoja
wao akililia chakula tunampa vitu hivyo mpaka ikifikia wakati wa kufuturu.” [Bukhari na Muslim].

Show More

Related Articles

Back to top button
Close