5. Ramadhan

Mwanamke wa Kiislamu ajiandaaje kwa Ramadhan?-3

Masharti ya toba

Ewe dada yangu katika imani, kuna masharti ambayo mwenye kutubu anapaswa kuyatekeleza. Sharti la kwanza ni kuiangalia nafsi yako mwenyewe na kujaribu kukumbuka na kujutia dhambi uliyoitenda. Sharti la pili ni kujiondoa au kujiweka mbali haraka na dhambi hiyo. Sharti la tatu ni kuazimia kwa dhati kwamba hutorejea tena katika dhambi hiyo.

Allah anasema: “Hakika toba (inay-
okubaliwa) ni juu ya wale wafanyao
jambo ovu pasina kujua kisha hutubia
haraka haraka.” [Qur’an, 4:17].

Ewe dada yangu, tubu kwa kuacha kuvaa vazi la sitara (Hijab) au kuvaa vazi hilo pasina kukidhi vigezo vya kisheria. Vigezo vya sharia ni kutobana, kutokuwa na marembo na rangi rangi za kuvutia watu, na pia kutoachia nywele za kichwa chako zionekane.

Tubia kwa kujipamba kwa hina, wanja na rangi za midomo mbele ya wanaume ambao siyo haramu kwao kukuoa. Tubia kwa kukosa utii kwa wazazi wako na mume wako, na kwa kuwatelekeza watoto wako wadogo hadi ukashika anasa za dunia. Tubia kwa kujihusisha na mazungumzo yasiyo na maana (laghwu), kusengenya, utesi na kuchonganisha au kufitinisha watu. Tubia kwa Allah kwa kuangalia maigizo, sinema, kusikiliza nyimbo, miziki na taarabu.

Tubia kwa kuihama Qur’an na ukawa huisomi kuifanya kitu kilichohamwa, kabla Mtume wa Allah hajakushitaki Siku ya Kiyama akisema: “. . . ewe Mola Mlezi wangu, hakika watu wangu waliifanya hii Qur’an kitu kilichohamwa.” [Qur’an, 25:30]. Tubu kwa kutokushukuru neema za Allah alizokuteremshia huku ukikumbuka maneno yake pale aliposema: “Na hata mkizihesabu neema za Allah hamuwezi kuzijua zote.” [Qur’an, 16:18].

Ewe dada yangu katika imani, tubia kwa kukosa subira na kulalamika pindi Allah alipokugusa kwa mtihani huu au ule. Tubia kwa kila dhambi uijuayo na hata usiyoijua, huenda Allah akakusamehe. Katika kuivuta huruma ya Allah, jitahidi kutenda mambo mema kabla na hata baada ya kutubia dhambi zako. Toa sadaka, onea huruma masikini, kuwa mnyenyekevu kwa wazazi na mume wako, kwani kufanya hayo kutavuta huruma ya Allah juu yako. Ikiwa kuna mtu ulimsengenya, nenda kwake umuombe msamaha. Usifanye hivyo tu iwapo unahofia kufanya kwako hivyo kunaweza kupelekea kukosekana kwa amani au kuibuka ugomvi naye.

Ewe dada yangu, kama kuna mtu uliyemdhulumu mali yake fanya haraka mrejeshee pamoja na kumuomba msamaha. Hayo ni muhimu uyafanye siyo tu kwa ajili ya kujiandaa kwa mwezi wa Ramadhan, bali kujiokoa kabla ya siku ambayo mema yako yatachukuliwa wapewe uliowadhulumu na yakiisha yachukuliwe madhambi yao urundikiwe wewe. Rejea kwa Allah kwani ni jambo zuri lililoje! Mja kurejea kwa Mola wake.

Katika kujiandaa kwa mwezi wa Ramadhan fanya zoezi hili la kutubia kila siku na uzidishe sana kuleta istighfari. Ili kufanikiwa inabidi kupambana haswa na nafsi na pia shetani, na hilo si jambo jepesi hata kidogo. Lakini jitahidi ili uingie katika maneno ya Allah: “Na wale wanaofanya juhudi ndani ya (amri zetu) bila shaka tutawaongoza katika njia zetu (za kheri) na hakika Allah yuko na wale watendao mema.” [Qur’an, 29:69].

Kuwa imara ewe dada yangu na jipe moyo kwamba Allah anasamehe madhambi yote. Ukifanya hivyo bila shaka utabadilika kwani Allah anasema: “Hakika Allah habadilishi hali ya watu mpaka wabadilishe yaliyo ndani ya nafsi zao.” [Qur’an, 13:11].

Kuwasamehe waliokukosea
Ewe dada yangu katika imani, sambamba na wajibu wa kwanza tuliouona wa kutubia kwa Allah kuna wajibu mwingine pia unapaswa kuufanya katika kujiandaa na mwezi wa Ramadhan. Wajibu ninaouzungumzia ni ule wa wewe pia kuwasamehe waliokukosea, hata kama hawajaja kukuomba msamaha. Kufanya hivyo ni kuisadia nafsi yako kwani Allah ni mwepesi kumsamehe mja anaye wasamehe wanadamu wenzake.

Tukumbuke kisa cha Abubakar Swiddiq (Allah amridhie) alipoapa kwamba hatomsaidia mtumishi wake ambaye alishiriki katika kumzushia uongo Bi. Aisha (Allah amridhie) kwamba amezini, kashfa ambayo ilibuniwa na wanafiki kumpaka matope mke huyo kipenzi wa Mtume.

Allah Ta’ala akateremsha
Aya isemayo: “Je hampendi
Allah awasamehe na ninyi?
Na Allah ni msamehevu mrehemevu.” [Qur’an, 24:22].

Hivyo, tuwasamehe wale wote waliotukosea kwa sababu pia hii ni tabia na mwenendo wa Waumini. Allah Ta’ala anasema: “Na iwapo mtasamehe na kupuuza na mkamuomba Allah msamaha, basi hakika Allah ni msamehevu na mrehemevu.” [Qur’an, 64:14].

Kuwasamehe watu wengi na kuacha kung’ang’ania ugomvi au kulipiza kisasi ndiyo mlango wa sisi pia kusamehewa na Allah dhambi zetu. Allah ameweka wazi kwamba kama sisi hatupendi kuwasamehe wengine basi na sisi hatutasamehewa.

Ewe dada yangu katika imani, hii ndiyo namna nzuri ya kujiandaa kwa swaumu ya mwezi wa Ramadhan. Kufunga swaumu za Sunna katika mwezi wa Shaaban, na kujibidiisha na kuwasamehe waliotukosea na pia kumuomba Allah msamaha.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close