5. Ramadhan

Mitandao ya kijamii ni neema kwa Ramadhan

Mitandao ya kijamii imekuwa ikilaumiwa na kusifiwa. Kwa wale wanaolaumu wanadai kuwa mitandao ya kijamii imechangia sana kuharibu maadili hasa ya vijana.

Kwa upande wa pili, wapo wanaoona kuwa mitandao ya kijamii ni chachu ya maendeleo katika jamii. Mbali ya kurahisha usambazaji wa habari, mitandao ya kijamii imewezesha kazi mbalimbali za kidini na kijamii. Makala hii itachambua namna mitandao ya kijamii inavyosaidia Waislamu katika mfungo wa Ramadhan.

Katika miaka ya hivi karibuni, mitandao ya kijamii imekuwa neema kwa mwezi mtukufu wa Ramadhan. Neema za mitandao ya kijamii imesambaa katika mambo mengi lakini hapa nitajadili mambo miwili ambayo ni kwanza, kuhamasisha utoaji sadaka na da’awa.

Mitandao ya kijamii inavyohamasisha utoaji sadaka

Katika zama hizi, mitandao ya kijamii ikiwemo WhatsApp, Instagram, Facebook na Twitter imetumika sana kuhamasisha utoaji sadaka. Ukusanyaji sadaka, aghlabu, huanza kabla ya Ramadhan na kushamiri zaidi baada ya mfungo kuanza. Sadaka hukusanywa na taasisi zilizo rasmi, vikundi vya watu na hata mtu mmojammoja.

Ni jambo la kufurahisha kuwa kila mwaka hamasa inakua na wachangiaji wanaongezeka pia. Hii ni dalili kuwa watu wanakimbilia mambo ya kheri na wanatumia kwa usahihi neema ya mitandao ya kijamii.

Kuongezeka kwa wachangiaji kunasukumwa na ukweli kuwa mitandao ya kijamii imerahisisha mambo matatu. Kwanza, mitandao ya kijamii imerahisisha kuwafikia wachangiaji wengi kwa sababu inafikisha habari kote ulimwenguni. Taarifa yako unayoituma ukiwa Kware-Hai inaweza kumfikia mtu aliyepo Jeddah au Toronto ndani ya sekunde moja.

Pili, mitandao ya kijamii imeongeza uwazi katika matumizi ya sadaka kwa sababu wachangiaji hupewa mrejesho wenye ushahidi wa picha na video kuwa sadaka zao zilitumika kwa usahihi. Hii imeongeza uwajibikaji kwa viongozi wanaokusanya sadaka na hivyo kuongeza imani ya wachangiaji.

Tatu, mitandao imerahisisha namna ya kuwafikia wahitaji. Kama ilivyo kwa wachangiaji, mitandao imerahisha upatikanaji wa wahitaji. Fedha za sadaka zilizokusanywa huko Namasalau-Ruvuma, zinaweza kumfikia kwa urahisi kabisa mhitaji aliyepo Kingale-Kondoa. Hivyo, sadaka inaweza kugawanywa na kuwanufaisha watu wa karibu na hata wale walio mbali kabisa.

Mitando na da’awa

Kupitia mitandao ya kijamii, watu wamepata nafasi kubwa ya kufikiwa na elimu ya saumu. Kwa uzoefu wangu naona kuna njia tatu kubwa zilizoshamiri katika miaka ya hivi karibuni ya kulingania dini zikiwemo darsa za Zoom, vídeo fupifupi na mabango.

Darsa za Zoom na mitandao mingine

Mtandao wa Zoom umekuwa maarufu sana toka mwishoni mwa mwaka juzi kutokana na uwezo wa kutumika mubashara na kuchanganya video, sauti na maandishi kwa wakati mmoja. Kwa msaada wa Zoom, nimeshuhudia madarasa mengi ya kufunza watu saumu ya Ramadhan.

Muhimu zaidi ni kuwa, mtu anaweza kufaidi madarasa haya akiwa mahali popote, madhali ana kifaa chake cha mawasiliano (simu au kompyuta) na bando. Madarasa haya ya mitandaoni yamesaidia sana kutoa majibu ya maswali yote yanayowatatiza wafungaji. Madarasa kama haya ya Zoom pia yanapatikana katika mitandao ya Instagram, Facebook na Youtube.

Da’awah kupitia video fupifupi

Kuna elimu kubwa kuhusu Ramadhan inatolewa kupitia video za masheikh maarufu na wale wasio na maarufu zinazotumwa mitandaoni. Video hizi zimejaa mitandaoni zikihanikiza ukubwa na utukufu wa Ramadhan. Aidha, katika kipindi hiki cha Ramadhan kuna video nyingi za Qur’an ambazo siyo tu zimeongeza fursa kwa watu kusikiliza Qur’an, bali pia zinahimiza watu kujifunza na kutafakari kitabu cha Allah.

Pamoja na video fupifupi, kuna elimu kubwa inatolewa mitandaoni kupitia mawaidha ya sauti. Wapo masheikh ambao wamekuwa wakitoa darsa la mfululizo (series) kuhusu saumu na alhamdulilah zimewafaa watu wengi.

Da’awah kupitia mabango (banners)

Haya ni mabango madogomadogo yenye ujumbe mfupi unaohusu Ramadhan. Mara nyingi, mabango haya hunakshiwa kwa rangi nzuri na kuwa na mvuto maalum kwa wasomaji. Haishangazi kuona mabango haya husambaa kwa kasi kubwa katika mitandao yote ya kijamii. Makampuni madogo kwa makubwa, taasisi za serikali na za kiraia nao wanatumia sana mabango haya kwa lengo la kujitangaza sambamba na kutoa elimu ya Ramadhan. Kutokana na umuhimu wa mabango haya, watu wengi huyatumia kama ‘status’ katika akaunti zao kwa lengo lilelile kwa kuhakikisha elimu ya Ramadhan inawafikia watu wengi zaidi.

Kwa ujumla, mitandao ya kijamii imesaidia sana kurudisha heshima ya Ramadhan na kuongeza ufahamu juu ya ibada ya saumu. Ni jambo la kufurahisha sana kuona elimu ya Ramadhan inayotolewa kupitia mitandao ya kijamii imepenya na kuwafikia hata wasio Waislamu. Matumizi haya mazuri ya mitandao ya kijamii yanapaswa kupongezwa na kuendelezwa.

Heko kwa watumiaji wa mitandao. Heko kwa wafungaji. Heko kwa kwa Waislamu. Twamuomba Allah atul i p e sote kwa utumiaji mzuri wa mitandao ya kijamii.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close