5. Ramadhan

Maandalizi ya Mashindano ya Kimataifa ya Kuhifadhi Qur’an yanoga

Maandalizi ya Mashindano ya Kimataifa ya Kuhifadhi Qur’an hapa nchini yanayoandaliwa na Jumuiya ya Kuhifadhisha Qur’an, Tanzania yamezidi kushika kasi ambapo mchujo unaendelea kutafuta wawakilishi wawili wa Tanzania katika mashindano hayo.

Wawakilishi hao wawili wa Tanzania, mmoja kutokea Zanzibar na mwingine Tanzania Bara, ndiyo watakaopeperusha bendera ya Tanzania katika kilele cha mashindano siku ya Mei 26 katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.

Akizungumzia mchujo wa mashindano ya mwaka huu, upande wa Bara, mashindano ya mwaka huu ambayo, Sheikh Othman Kaporo amesema zoezi la uchujaji linaendelea kanda tofauti. “Kwa sasa tumewafuata vijana huko mikoani katika kanda tano tofauti,” alisema Sheikh Kaporo.

Sheikh Kaporo alisema, mchujo wa mwisho utafanyika mkoani Dodoma ambapo baada ya hapo mshindi mmoja atakayepatikana upande wa Tanzania Bara atakayeiwakilisha nchi katika mashindano hayo ya kimataifa. Mshindi huyo wa Bara ataungana na yule wa Zanzibar na hivyo kufanya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa na washiriki wawili.

Kuhusu washiriki wa kimataifa, Sheikh Kaporo alisema wameshatuma mialiko kwa nchi zaidi ya 35 duniani na tayari nchi 22 zimethibitisha kushiriki. Taasisi hiyo ilianza kuendesha mashindano hayo tangu mwaka 1992, ambapo inatajwa kuwa yamesaidia kuibua vijana wengi waliohifadhi Qur’an hapa nchini. Kuhusu malengo ya mashindano hayo, Sheikh Kaporo alisema ni kuwajenga vijana kimaadili ili wawajibike kwa jamii na taifa, kama yalivyo mafundisho ya Qur’an.

Sisi tunawatengeneza vijana wetu waweze kuwa na tabia nzuri na maadili mema,ili tuwezeshe kustawisha amani na uwajibikaji na ili tuweze kupambana na ufisadi,” alisema Sheikh Kaporo. Aidha, Sheikh Kaporo alisema, wanaendelea na mchakato wa kumtafuta mtu atakayepewa tuzo ya kuihudumia Qur’an. “InshaaAllah, tutakuwa na tuzo ya mtendaji mzuri katika kuihudumia Qur’an katika level (ngazi) ya Kimataifa. Mtu huyo anakuwa amefanya kazi ya kuitangaza, kuifundisha na kadhalika,” alisema Sheikh Kaporo.

Sheikh Kaporo alisema, mshindi atapatikana kwa kupigiwa kura na taasisi kubwa kutoka sehemu mbalimbali duniani. Tuzo hiyo tayari imeshatolewa kwa watu kadhaa huko nyuma. Mtu wa kwanza kupewa ni tuzo hiyo ni Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Pili, Mzee Ali Hassan Mwinyi.

Wengine waliowahi kupewa tuzo hiyo ni Msimamizi wa Kuhifadhisha Qur’an Duniani Dkt. Abdallah Ally Basfari, Mwenyekiti wa Tuzo za Kimataifa Dkt. Walid Shwaib na Makamu wa Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Gharib Bilal.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close