5. Ramadhan

Karibu Ramadhan

Masheikh mbalimbali wametoa nasaha juu ya namna ya kujiandaa na kuutumia mwezi wa Ramadhan ili kufikia lengo la kuwa wachamungu. Aidha, masheikh hao wakiongozwa na Mufti wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kaabi, wametaja matendo yanayopaswa kufanywa ndani ya Ramadhan na yale yanayokatazwa, kwa mujibu wa Qur’an na Sunna. Akiongea na gazeti hili kwa njia ya simu kutokea Zanzibar, Mufti wa Zanzibar, Sheikh Kaabi, amesema, ni wajibu wa kila Muislamu kujiandaa kwa kusafisha nia na kufanya toba ya kweli.

Ni wajibu wetu kujitayarisha kwa mwezi wa Ramadhan kwa matayarisho yaliyo mazuri. Hiyo ni pamoja na kuwa na nia safi na kufanya toba ya kweli; na siyo kujitayarisha kwa kula na kunywa,” alisema Mufti Kaabi na kisha akahimiza masikilizano na mapatano kwa wale waliogombana ili wote waingie kwenye mwezi wa Ramadhan wakiwa na mioyo safi isiyo na chuki na vinyongo.

Pia, Mufti Kaabi alitoa wito kwa wafanyabiashara kutopandisha holela bei za vyakula huku akihimiza usomaji wa Qur’an katika mwezi huo. Kwa upande mwingine, Mufti Kaabi amekemea vitendo vya vunja jungu ambavyo huambatana na maasi, akisema ni vitendo viovu.

Watu wasivunje jungu kwa kufanya maasi kabla ya Ramadhan na kwa kwenda beach (fukweni). Hayo ni maasi makubwa,” alisema Mufti.

Sheikh Barahiyan: Kufunga bila kusali ni kosa kubwa

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Vijana wa Kianswar ya jijini Tanga (AMYC), Sheikh Salim Barahiyan, Sheikh Barahiyan alisema, funga ya Ramadhan inaendana na sala, na kusema kuwa ni wajibu wa kila Muislamu kuhakikisha anafunga na kusali pia.

“Wito wangu kwa Waislamu, ni kwamba, wengi katika Waislamu kwa sasa ima hawafungi au wanafunga lakini hawasali. Hili ni moja kati ya makosa makubwa sana, kwa sababu sala ni katika nguzo ya Uislamu lakini pia kitu cha kwanza atakachoulizwa mja katika matendo yake kwa ujumla Siku ya Kiyama ni sala,” alisema Sheikh Barahiyan.

Aidha, Sheikh Barahiyan amewatolea wito wanawake wa Kiislamu kuhakikisha wanavaa mavazi ya stara katika mwezi wa Ramadhan ili funga zao zisipate misukosuko, na kisha wadumu katika mwenendo huo hata baada ya Ramadhan. “Wakina mama wengi wa Kiislamu hawajisitiri vizuri. Wafahamu katika mwezi wa Ramadhan suala la stara ni muhimu kwao pia, tofauti na hivyo funga zao zitakuwa na mashaka,” alisema Sheikh Barahiyan.

Katibu wa BASUTA
Naye Katibu wa Baraza la Sunna nchini (BASUTA), Sheikh Shaaban Mussa amesema, katika mwezi wa Ramadhan, milango ya pepo hufunguliwa, milango ya moto hufungwa, na mashetani wakorofi hudhibitiwa na hivyo basi Waislamu wajiandae kuvuna thawabu nyingi.

Sheikh Shaaban aliwashauri Waislamu kuutumia vema mwezi wa Ramadhan kwa kujiwekea ratiba ya kusoma Qur’an, kuwahi misikitini mapema, kusikiliza darasa kutoka kwa Masheikh na kutoa sadaka kwa wingi kwani malipo au ujira wa sadaka katika mwezi wa Ramadhan huwa mara dufu.

Akiunga mkono hoja ya Sheikh Barahiyan kuhusu umuhimu wa sala za faradhi, Sheikh Shaaban aliwataka Waislamu kuhakikisha siyo tu wanasali sala zote tano kwa siku lakini pia, kwa wanaume, wahudhurie sala hizo msikitini ili kupata fadhila za kusali jamaa. Kadhalika, Sheikh Shaaban alishawashauru Waislamu kutoacha kuhudhuria sala ya Tarawehe na kuhakikisha wanamaliza rakaa zote na imamu. Pia alihimiza kusali sala nyingine za sunna za kisimamo cha usiku.

Sheikh Shaaban pia amewataka wale wenye uwezo wa kwenda Umra katika kipindi cha mwezi wa Ramadhani wafanye hivyo kwani ujira wa Umra katika mwezi wa Ramadhani unalingana na ujira wa hijja. Katika kuhimiza nukta hii, Sheikh Shaaban alisema ipo riwaya nyingine isemayo Umra kipindi cha Ramadhan ni sawa na kuhiji na Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie).


“Kuudiriki mwezi wa Ramadhan
ni fursa adhimu kwetu ambayo yafaa
tuikumbatie kwa mikono miwili
kwani hakuna ajuae kama ataidiriki
Ramadhan ya mwakani,” alisema
Sheikh Shaaban.

Sheikh Alhadi na kufuturisha

Naye Sheikh wa mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salum amehimiza watu kufuturisha akisema ibada hiyo ina ujira mkubwa. “Kufuturisha kuna baraka kubwa, na Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amehimiza Waumini kufuturisha. Kufuturisha maana yake ni kile kifungua kinywa, baada ya kuwa mtu amefunga. Hiyo ndio inaitwa ‘iftwaar.’ Vile vinavyofuata baada ya hapo – mihogo, tambi, sambusa – ni vyakula,” alifafanua Sheikh Alhadi.

Pia Sheikh Alhadi alisema, kuwa katika kufungua swaumu, suala la kuzingatia ni kuzama kwa Jua wakati wa jioni na si adhana kama ilivyozoeleweka na watu wengi.

“Waislamu wengi wanadhani mtu anatakiwa afungue baada ya adhana. Adhana siyo kigezo cha kisheria cha kufungua. Kigezo cha kisheria cha kufungua ni kuchwa kwa Jua,” alisema Sheikh Alhadi na kuongeza: “Maana unaweza ukapita mahali uko safarini hakuna msikiti – uko barabarani, uko porini – unatarajia adhana utaisikia wapi?Utakuta mtu amekaa Jua limeshakucha anasema, ‘Mimi nasubiria adhana.’ Ni lazima uharakishe kufungua, hiyo ndio sunna.”

Kundecha aasaa vijana Kiislamu

Naye Amir wa Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Musa Kundecha alielekeza nasaha zake vijana wa Kiislamu kuutumia mwezi huo ili kujisafisha na matendo yasiyompendeza Mwenyezi Mungu.

“Ramadhan ni msimu maalumu wa ibada kwa tamko la Mtume, kwamba, umewafikieni mwezi wenye baraka, mwezi ambao milango ya pepo hufunguliwa, milango ya moto hufungwa na mashetani hufungwa. Maana yake, hii ni fursa maalum na adhimu kwa vijana ya kurejea kwa Mola wao, hasa vijana ambao wana tatizo kubwa sana la kudanganyika kutokana na vishawishi vya shetani,” alisema Sheikh Kundecha

Pia, Sheikh Kundecha aliwaambia vijana, Ramadhan ni kama kipindi cha ‘promosheni’ kwa kuwa malipo ndani ya mwezi huo yanakuwa makubwa sana.

“Tunaweza kusema kwa lugha ya wahamasihaji Ramadhan ni kipindi cha promosheni. Malipo yanakuwa na fadhila kubwa sana. Sala ya sunna katika kipindi cha Ramadhan inafananishwa na sala ya faradhi nje ya Ramadhan. Ikiwa ni sala ya usiku inakuwa na nafasi bora na ukubwa zaidi. Sala ya usiku ni bora wakati wowote, lakini ikiingiliana na Ramadhan ubora wake unazidi mara 70 kuliko wakati wa kawaida,” alisema Sheikh Kundecha.

Sheikh Kundecha aliongeza kuwa vijana wasidanganyike sana kwa afya waliyonayo bali watumie fursa ya nguvu ya afya waliyopewa na Mwenyezi Mungu kufanya ibada kwa wingi katika mwezi huo.

Sheikh Katimba: jiepusheni na yanayoharibu swaumu
Naye msemaji wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Sheikh Rajab Katimba amehimiza Waislamu kujiepusha na mambo yanayobatilisha swamu.

“Mambo yanayobatilisha swaumu ni mengi, lakini moja ni kufunga bila nia lakini vilevile kula kwa makusudi, kumuingilia mke kwa makusudi na kusema uongo, yapo mengi ila haya ni baadhi tu,” alisema Sheikh Katimba Kwa upande wake, Sheikh Hashim Rusaganya amesema katika mwezi wa Ramadhan vitendo kama vya kunywa maji hadharani, kupiga ngoma za daku na kuendelea kuishi kimada havifai.

Sheikh Mkali: Someni Qur’an
Mwandishi pia alifanya mahojiano na Katibu wa Mudir wa Kituo cha Kiislamu cha Kimisri (Azhar Sharrif) kilichopo Chang’ombe jijini Dar es Salaam, Sheikh Yahya Mkali, aliyewanasihi Waislamu kukithirisha kusoma Qur’an kwa kuwa ndani ya mwezi huo ndimo kiliteremka kitabu hicho kitukufu.

“Waislamu wanapaswa kusoma sana Qur’an ndani ya mwezi wa Ramadhan kwani kitabu hicho kilishuka katika mwezi huo,” alisema Sheikh Mkali.

Maandalizi ya Mashindano ya Qur’an yanoga
Wakati masheikh wakiwanasihi Waislamu juu ya namna bora ya kuuendea mwezi wa Ramadhan, taasisi mbalimbali za Kiislamu zimeshaanza maandalizi ya mashindano ya Qur’an, ambayo hushamiri zaidi mwezi huo mtukufu.

Akizungumzia maandalizi ya mashindano ya kimataifa ya usomaji Qur’an, Mwenyekiti wa Taasisi ya kuhifadhisha Qur’an nchini, Sheikh Othman Kaporo amesema kwa sasa wanashirikisha kanda tano nchini ili kupata watakaoshiriki mashindano hayo ya kimataifa kutoka Tanzania. Sheikh Kaporo amesema mashindano ya mwaka huu yatakuwa ni ya aina yake na yatafanyika Mei 26 mwaka huu.

Kwa upande wa mashindano ya Afrika, Taasisi ya Al-Hikma Foundation nayo imeshaanza mchakato wa kupata washiriki kutoka katika nchi mbalimbali za Afrika. Mashindano hayo ya Afrika yanatarajia kufanyika Mei 19 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close