5. Ramadhan

Hekima ya kufunga mwezi wa Ramadhan

Funga ya Ramadhan ni miongoni mwa nguzo tano za Uislamu na ni dalili na alama inayothibitisha Uislamu wa mtu.

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Uislamu umejengwa juu ya nguzo tano; kukiri na kushuhudia kwamba hapana Muabudiwa wa haki isipokuwa Allah na Muhammad ni Mtume wake, kusimamisha sala, kutoa zaka, kufunga mwezi wa Ramadhan na kwenda kuhiji (Makkah).” [Bukhari na Muslim].

Na miongoni mwa majina ya Allah ‘Azza Wajallah’ ni Al–Hakim (Mwenye Busara). Neno ‘Hakim’ linatolewa kutoka kwenye mzizi wa ‘hukmu’ (hukumu) na ‘hikmah’ (Hekima). Mwenyezi Mungu ndiye anayetoa hukumu, na hukumu zake ni zenye hekima zaidi na sahihi kabisa hazina chembe ya dosari.

Mwenyezi Mungu hatoi hukumu yoyote isipokuwa kuna hekima kubwa nyuma ya hukumu hiyo, ambayo tunaweza kuielewa, au mawazo yetu yanaweza yasiongozwe kuielewa, pia tunaweza kujua sehemu yake ndogo, lakini sehemu kubwa ikawa tumefichwa.

Allah ‘Azza Wajallah’ ametaja sababu na hekima ya kuamrisha funga juu yetu pale aliposema: “Enyi Mlioamini! Mmeamrishwa kufunga kama walivyoamrishwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumchamungu.” [Qur’an, 2:183].

Kufunga maana yake ni kujenga tabia ya kukinai mambo ya hii Dunia na raha zake, na kutafuta yale ambayo yako pamoja na Allah ‘Azza Wajallah’. Hii ni moja ya njia bora kabisa za kumsaidia mtu kutekeleza amri za Uislamu.

Wanazuoni mbalimbali (Allah awarehemu), wametaja baadhi ya sababu kwa nini funga imeamrishwa, ambazo zote zina vipengele vya ‘taqwa’ ndani yake. Si vibaya kuvinukuu hapa ili kuwafanya watu wanaofunga wawe makini kufikia.

Hebu tuone baadhi ya vipengele vya hekima na sababu za kufunga. Mosi, funga humfanya mtu ampende allah na Mtume

Kumpenda Allah na Mtume wake ni miongoni mwa mambo yanayothibitisha imani ya mtu. Pia, ni msingi muhimu wa kukubaliwa kwa matendo (amali) ya mtu.

Amesema Mjumbe wa Allah (rehema za Allah na amani zimshukie): “Mwenye mambo matatu atakuwa ameonja ladha ya imani: Ampende zaidi Allah na Mtume wake kuliko chochote, awapende watu kwa ajili ya Allah na achukie ukafiri kama anavyochukia kutupwa motoni.” [Bukhari na Muslim].

Pili, kuthamini na kushukuru neema za allah

Kufunga ni njia ya kutufanya tuthamini na kushukuru kwa neema na raha ambazo Allah ‘Azza Wajallah’ ametupa kwa sababu kufunga maana yake ni kuacha kula, kunywa, jimai, mambo ambayo kusema kweli ndiyo raha kubwa zaidi hapa Duniani.

Ukizikosa neema na raha hizi ndiyo unaweza kutambua thamani yake. Hivyo basi, kupitia swaumu tunayaacha mambo haya kwa muda ili tutambue thamani ya neema hizo na hatimaye tuhamasike kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema hizo.

Tatu, kinga dhidi ya maovu

Kufunga ni njia mojawapo ya kuacha mambo ya haramu. Hii ni kwa sababu, kama mtu anaweza kuacha vitu ambavyo ni halali kwa ajili ya kumridhisha Allah ‘Azza Wajallah’ na kuogopa adhabu yake iumizayo, basi mtu huyo anaweza pia kuacha mambo ya haramu, kwa sababu hizohizo. Kwa hiyo kufunga ni njia mojawapo ya kuepuka mambo ambayo Mwenyezi Mungu ameyakataza.

Nne, kudhibiti matamanio

Kufunga kunatuwezesha kudhibiti matamanio yetu. Mtu anapokuwa ameshiba, matamanio yake yanaongezeka; lakini anapokuwa na njaa, matamanio hayo yanakuwa dhaifu.

Ushahidi wa hili ni kauli ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ambaye amesema: “Enyi vijana! Yeyote miongoni mwenu mwenye uwezo wa kuoa na aoe, kwa sababu itamsaidia kujihifadhi na kulinda heshima yake. Yeyote asiyeweza kuoa, basi afunge kwa sababu hii itakuwa kinga kwake.” [Bukhari na Muslim].

Tano, huruma na ukarimu

Kufunga kunatufanya tuwe wakarimu na wenye huruma kwa masikini, kwa sababu mtu anayefunga anapohisi machungu ya njaa kwa muda mfupi, basi atawakumbuka wale walio katika hali hii wakati wote.

Kwa kuwakumbuka masikini na kuwasaidia kujiondoa kutoka katika njaa na kiu wanayosikia, mfungaji atakuwa ameonesha ukarimu wao. Kwa hiyo, kufunga kunafundisha kuwaonea huruma masikini.

Sita, kufunga kunamfedhehesha na kumdhoofidha shetani

Hii ina maana kufunga kunadhoofisha athari za minong’ono (wasiwasi) ya shetani kwa mtu anayefunga, hali inayopunguza madhambi yake. Ushahidi wa hili ni kauli ya Mtume (rehema za Allah na amani zimfikie) aliposema:

“Shetani anatembea kwenye mwili wa watoto wa Adam kama vile damu inavyotembea.”

Kwa hiyo, kufunga kunaminya njia ambazo shetani anapitia, na hivyo ushawishi wake kwa watoto wa Adam unakuwa mdogo.

Saba, kumhofu allah

Mtu anayefunga anajifunza kukumbuka yale ambayo Allah Aliyetukuka wakati wote anayaangalia. Mfungaji anaacha yale mambo anayoyapenda, hata kama ana uwezo wa kuyafanya kwa sababu anajua kwamba Mwenyezi Mungu anamuona.

Mtume amesema: “Yule ambaye haachi kusema uwongo na haachi kufanya vitendo viovu, Allah hana haja na kuona kuwa anaacha chakula chake na kinywaji chake (yani Allah hana haja na funga yake).” [Bukhari].

Akasema tena Mtume: “Swaumu si kujizuia na kula na kunywa tu, bali pia (kujizuia) na maneno ya kipuuzi na mazungumzo machafu. Anapotukanwa mmoja wenu au kuudhiwa, anatakiwa aseme, “Mimi nimefunga, mimi nimefunga.’” [Ibn Khuzaymah, Ibn Hibbaan na Haakim].

Nane, kuzizoea ibada

Kufunga kunamfanya Muislamu azoee kwa kiasi kikubwa kufanya vitendo vya ibada kwa sababu mfungaji aghalabu hufanya ibada mara kwa mara.

Hizi ni baadhi tu ya sababu kwanini funga imeamrishwa. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atusaidie kuzifanya funga zetu zifikie malengo, ili tumuabudu Yeye kwa usahihi.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close