5. Ramadhan

Fadhila na faida za Qiyamu llayl

Kutoka kwa abdullah bin umar (allah amridhie) amesema: “Wakati wa uhai wa mtume (rehema za allah na amani zimshukie), mtu mmoja alikuwa akimsimulia mtume ndoto aliyoota, nami nikatamani niote ndoto ambayo nitamsimulia nabii wa Allah. Wakati huo nilikuwa kijana ambaye bado sijaoa, nikawa nalala katika msikiti wa mtume. Siku moja nikaota malaika wawili wamenichukua na kunipeleka motoni, huko nikawaona watu ninaowafahamu, nikasema (mara tatu): ‘najilinda kwa allah na adhabu ya moto.’ Haukupita muda mrefu nikakutana na malaika mwingine akaniambia, ‘usiogope.’

“Nikamsimulia jambo hilo Hafswa (Allah amridhie) naye akamsimulia Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie). Mtume akasema, ‘Hakika Abdullah ni mtu bora, laiti angelikuwa anasimama usiku (kuswali).’”

Kuanzia siku hiyo Abdullah akawa halali usiku isipokuwa muda mchache.

Katika riwaya nyingine, Abdullah amesema: “Nilikutana na Malaika mwingine akaniambia,  ‘Usiogope kwani wewe ni mtu mwema.’ Nilipoangalia ndani ya moto nikaona watu (wakiwamo Makuraish) wamening’inizwa kwa minyororo vichwa vyao vikiwa chini muda wote. Malaika wakanipeleka upande wa kulia.”

“Nikamsimulia jambo hilo Hafswa (Allah amridhie) naye akamsimulia Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie).” [Muslim].

Mafunzo ya tukio Fadhila za Qiyamu Llayl

Ibada za usiku zina ujira mkubwa mbele ya Allah Aliyetukuka na pia ni sababu ya kupata msamaha wa Allah kama ilivyokuja katika hadithi. “Mwenye kusimama (usiku wa Ramadhan kwa sala) kwa imani na kutaka radhi za Allah – atasamehewa yale yaliyotangulia katika madhambi yake.”

 Al–Haafidh bin Rajab (Allah amrehemu) amesema: “Muumini anajumuisha jihadi mbili kwa ajili ya nafsi yake katika mwezi wa Ramadhan; jihadi ya mchana kwa kufunga na jihadi ya usiku kwa kusimama (kuswali). Atakayejumuisha jihadi hizi mbili atapata ujira wake bila ya hesabu.” [Fat–hul bari].

kufufua Sunna

Sala za usiku ni miongoni mwa sala za Sunna ambazo Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ametuhimiza kuziswali ndani ya mwezi wa Ramadhan. Visimamo vya usiku ni darasa muhimu katika kukuza imani ya Muislamu na kuutakasa moyo kutokana na maasi, chuki, uhasidi na kadhalika.

Abu Huraira (Allah amridhie) amenukuuu hadithi kutoka kwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) aliyesema: “Allah Ta’ala amesema, ‘Nimewatayarishia waja Wangu wema kile ambacho jicho lolote halijapata kuona na sikio lolote halijapata kusikia na wala haijapata kupita katika moyo wa binadamu.”

Abu Huraira akasema: “Ukitaka soma (kauli ya Allah), ‘Nafsi yeyote haijui iliofichiwa katika hayo yanayofurahisha macho huko Peponi.’” [Qur’an, 32:17].

kuswali usiku huboresha afya ya mwili

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ametuambia: “Shikamaneni na sala za usiku (Qiyamu Llayl) kwani ni desturi za waja wema kabla yenu na pia ni njia ya kujikurubisha kwa Allah Ta’ala, na zinazuia madhambi na kufuta maovu…” [Ahmad na Tirmidhiy, na Sheikh Albani amesema ni hadithi sahihi].

kutamani mambo ya kheri

Katika tukio hili tunajifunza umuhimu wa kushindana kufanya mambo ya kheri. Abdullahi (Allah amridhie) alikuwa akitamani kuota ndoto njema ambayo atamsimulia Mtume (rehema na amani ya Allah zimshukie) ili iwe sababu ya yeye kubashiriwa Pepo.

Kingine ambacho tunajifunza kupitia tukio hili ni kwamba Abdullahi alipenda kulala kwenye masikiti wa Mtume k w a ajili ya kufanya ibada licha ya kuwa na umri mdogo.

Nafasi ya ndoto katika maisha ya Muislamu

Kwa kawaida, mwanadamu huota ndoto mbalimbali, zipo za kutisha kiasi cha kuwafanya watu wahangaike huku na kule kujua tafsiri ya ndoto zao walizoota. Hata hivyo, watu wengi huamini kuwa ndoto zinaweza kumfahamisha mtu kuhusu maisha yake ya baadaye na hivyo kutafuta njia za kushughulika nazo pasipo kutambua kuwa wameingia katika mtego wa shetani.

Ndoto njema

Hizi ni ndoto nzuri na zenye bishara njema kwa mtu. Kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu, inaruhusiwa kuwasimulia watu ndoto njema uliyoota.

Ndoto mbaya

Hizi ni ndoto mbaya za kutisha ambazo hutokana na shetani. Kwa mujibu wa Uislamu haimpasi yeyote kusimulia ndoto mbaya aliyoiota au kuidadisi kwani huo ni mlango anaoutumia shetani kuingiza wasiwasi katika nyoyo za watu.

Ndoto za msongo wa mawazo

Wakati mwingine mtu hukumbwa na matatizo mengi hadi akawa na msongo wa mawazo, unaoweza kusababisha ndoto. Asilimia kubwa ya ndoto hizi hutokana na wasiwasi wa shetani, hivyo ni vema kuzipuuza na kujilinda kwa Allah kutokana na shetani.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close