5. Ramadhan

Chunga usiwe miongoni mwa wanaoshinda na njaa mwezi wa Ramadhan

Kisa cha watu wa pangoni, yaani ‘Aswhaabul Kahfi’ ni miongoni mwa visa vikongwe katika historia ya Uislamu na maisha ya mwanadamu kwa ujumla. Kisa hiki ambacho ni moja kati ya visa lukuki vinavyoonesha uwezo na ukubwa wa Allah Aliyetukuka, si maarufu katika Uislamu tu, bali hata katika jamii za wasiokuwa Waislamu.

Kwa muhtasari, kisa hiki kinawahusu watu wasiopungua saba, na mbwa wao, waliokimbia nchi yao kutokana na kulazimishwa kufanya ibada za masanamu. Wakiwa njiani, vijana hao waliingia pangoni kwa ajili ya kujipumzisha, lakini Allah Allah ‘Azza Wajallah’ kwa hekima yake aliwalaza humo kwa muda usiopungua miaka 309.

Allah Ta’ala anasimulia kwa kusema: “Vijana hao walipokimbilia kwenye pango walisema, ‘Mola wetu Mlezi! Tupe rehema itokayo kwako, na tutengenezee uongofu katika jambo letu.’ Tukayaziba masikio yao kuwalaza humo pangoni kwa muda wa miaka kadha wa kadha. Kisha tukawazindua ili tujue ni lipi katika makundi mawili lililohesabu sawa muda waliokaa. Sisi tunakusimulia habari zao kwa kweli. Hakika wao walikuwa ni vijana waliomuamini Mola wao Mlezi. Na Sisi tukawazidisha uongofu.” [Qur’an, 18:10-13].

Nimelazimika kukikumbuka kisa hiki kikongwe kwa kukinasibisha na maisha halisi wanayoishi Waislamu wengi ndani ya Ramadhan. Ikiwa imepita miaka 1438 tangu kufaradhishwa ibada ya swaumu kwa umma wa Nabii Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie), kuna kila dalili kwamba sehemu kubwa ya Waislamu hawajatambua utukufu na uzito wa ibada ya swaumu. Wengi tumelala usingizi wa pono kama ule wa Aswhaabul Kahfi.

Mwenye kufanya mema – awe
mwanaume au mwanamke
na hali yeye ni Muumini, tutampa
uhai ulio mzuri; na tutawalipa (huko
Akhera) malipo yao kutokana na mazuri
waliyokuwa wakiyafanya.”
(Qur’an, 16:97)

Matokeo yake, tumekuwa wazito kutekeleza ibada ya swaumu katika sura inayomridhisha Allah licha ya kuudiriki mwezi wa Ramadhan kila mwaka. Kama tujuavyo, swaumu ni miongoni mwa masomo makuu ya vitendo (pratical) ambayo humuandaa mfungaji wa kweli kuwa mchamungu. Swaumu pia huilea nafsi ya mfungaji na kumkataza kufanya mambo yaliyoharamishwa. Hii ina maana, swaumu ni mazoezi ya kimwili na kiroho ambayo humtayarisha Muislamu kukabiliana na matukio ya ghafla, yenye kuhuzunisha na kutia simanzi.

Na kwa hakika, swaumu si kujizuwia kula na kunywa tu. Ni zaidi ya hapo. Ukiacha kujizuia kula na kunywa, tunapaswa pia kujizuia na mambo mengine ya maasi ikiwemo kusema uongo, kutukana, kusengenya, kufitinisha au kuchonganisha watu, kutazama haramu, na kadhalika. Mtume (rehema na amani ya Allah zimshukie): “Yeyote ambaye hatoacha kusema uongo, kusengenya, kufitinisha, kutoa ushuhuda wa uongo, basi ajue kuwa Allah hana haja na swaumu yake katika kuacha chakula chake na kinywaji chake.” [Bukhari na Muslim].

Ni jambo la kusikitisha kuwa, wapo wanaokula rushwa, kutakatisha fedha na kuchuma riziki zisizo za halali hali wamefunga. Baadhi ya akinamama wanatembea uchi barabarani na kujipamba kwa manukato na mapambo mengine ya haramu wakidhani kutokula na kunywa katika mchana wa Ramadhan kumetosha swaumu zao kukubaliwa na Mwenyezi Mungu.

Huko ofisini, watu wanafunga na huku wakijihusisha na ubadhirifu wa mali za umma na kula rushwa kwa kudhani kuwa kufanya hivyo si dhambi. Kinachoshangaza zaidi ni kwamba, wengi miongoni mwetu Waislamu tunafunga pasina kusali; na hili ni kosa kubwa kisharia. Juu ya hilo, wanazuoni wengi wa sharia ya Kiislamu (Fuqahaau) wamesema swaumu haikubaliwi pasina kuswali.

Vile vile, ni makosa makubwa mtu kuswali siku za mwanzo za Ramadhan na kisha kuzembea au kuacha kusali katika siku zilizobaki. Wapo pia baadhi yetu wanaoitakidi kuwa kuangalia tamthilia na sinema ni halali kisharia. Ukweli ni kwamba, tamthilia nyingi zina maudhui machafu ndiyo maana sharia inawataka Waislamu kuinamisha chini macho yao wasiangalie mambo ya haramu.

Hivyo basi, Ramadhan hii iwe ni fursa adhimu ya kusahihisha makosa haya ili nafsi zetu zibadilike na kuielekea twa’a ya Allah. Ramadhan ni mwezi wenye fadhila, ubora na heri nyingi hasa kwa yule mwenye kufunga na kudumisha ibada ya sala, akawa pia ni mwenye kujitahidi kutumia fursa alizopewa na Allah katika kuchuma heri.

Atakayeafikishwa katika hayo, kwa hakika amefuzu na ametangulia mbele katika heri; na yule asiyefunga au kufanya uzembe katika kuziendea ibada ndani ya Ramadhan atakuwa amepata hasara.

Maana yake ni kwamba, mizani ya mja kwa upande wa mambo ya kheri kuwa nzito zaidi kuliko baadhi ya walioonekana kujitahidi zaidi, ni pamoja na kuidiriki Ramadhan na kutumia fursa hiyo katika kuwekeza kwenye kheri. Allah Aliyetukuka anasema: “Mwenye kufanya mema – awe mwanaume au mwanamke na hali yeye ni Muumini, tutampa uhai ulio mzuri; na tutawalipa (huko Akhera) malipo yao kutokana na mazuri waliyokuwa wakiyafanya.” [Qur’an, 16:97].

Hivyo, huu ni muda muafaka kwa wale wenye kupigania fursa za misimu ya kheri kuhakikisha kuwa hawatoki mikono mitupu katika msimu huu wa Ramadhan kwani mja hawezi kufikia daraja ya uchamungu isipokuwa kwa kudumisha matendo mema.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close