2. Deen

Mwenye kujinasibisha na watu yuko pamoja nao

Krismasi na mwaka mpya ni miongoni mwa sikukuu za wasiokuwa Waislamu ambazo husherehekewa kwa msisimko  mkubwa duniani. Utafiti unadhihirisha kuwa sikukuu hizi zinasherehekewa kwenye mataifa mengi kama sikukuu za kidini na pia za kitaifa (public holidays).

Sikukuu hizi pia husherehekewa hata na baadhi ya mataifa yasiyo na muelekeo wowote wa dini. Mathalan, katika sikukuu ya Krismasi hapa nchini utawaona watu wakipamba nyumba zao kwa mti maalumu (mti wa Krismasi), pia watu hutembeleana na kubadilishana zawadi. Yote haya yana mizizi yake  kihistoria. Hata hivyo, ni watu wachache mno wanaofahamu undani wa sikukuu hii.

Mtunzi wa kitabu kinachoitwa, ‘The Christmas Encyclopedia’ anathibitisha kuwa, hakuna dalili ya kimaandiko inayoitaja siku ya Desemba 25 kama ndiyo siku halisi aliyozaliwa Nabii Isa (Yesu), bali hii ni siku iliyotokana na sherehe za kipagani za Warumi zinazofanywa mwishoni mwa kila mwaka.

Baadaye, sherehe hizo zikabadilishwa na kuingizwa katika ibada inayodaiwa  kuwa ya Kikristo katika mwaka wa 350 Miladiya, wakati ambapo Papa Julius  wa kwanza aliitangaza Desemba 25 kuwa siku ya kuzaliwa kwa Isa (Yesu). Ni  katika msimu huu ambao maduka hufurika wanunuzi wakisaka zawadi za Krismas.

Katika hili pia wapo baadhi ya Waislamu ambao huungana na marafiki, majirani au wafanyakazi wenzao kwa lengo la kufurahikia sherehe hizi zilizo kinyume kabisa na mafundisho ya Uislamu. Makatazo yanaenea pia kwa kila jambo linalohusu sherehe hii kama vile kushiriki kwenye tafrija (parties), kubadilishana zawadi au  chakula, kupeana zawadi, na pia kupongezana kwa maneno kama vile ‘Merry Christmas’ au ‘Happy New year’.

Ikiwa ni mmoja wao, yafaa ujiulize ni kwa nini unamuasi Allah hali ya kuwa umeahidi kutomshirikisha? Tunauliza hivyo tukitambua kuwa kwa mujibu wa itikadi ya Kikristo, Yesu siyo tu mwana wa Mungu bali ni Mungu hasa. Si ni sisi ambao ndani ya Sala zetu tunamuambia Mwenyezi Mungu:

Wewe tu tunakuabudu , na wewe tu tunakuomba msaada.” (Qur’an, 1:5).

Kama tunaitakidi hivyo iweje tushirikiane na wenye imani kinyume na imani yetu kwenye sikukuu zao? Sikukuu ni jambo la ibada, hivyo kama imeegemezwa katika imani potofu kwa mujibu wa Uislamu, kusherehekea sikukuu hiyo ni kuunga mkono upotovu.

Pamoja na hayo, katika hali ya kawaida, Muislamu hajakatazwa kushirikiana na wasiokuwa Waislamu katika mambo ambayo hayakiuki sharia na taratibu za ibada za Kiislamu. Swali ni kwamba, vipi Muislamu ajitenge na kusherehekea sikukuu hii? Sisi Waislamu, hatuna nafasi wala umuhimu wa kusherehekea Krismas kwani kufanya hivyo ni kuendeleza uzushi huu katika vizazi vyetu, lakini pia kuingiza mila za wengine ndani ya Uislamu.

Hivyo, Waislamu hatupaswi kuwa watu wa kuiga mitindo na kasumba zisizo na faida wala msingi. Katika kututahadharisha na tabia hii, Mtume (rehema na amani ya Allah zimfikie) amesema:

Mwenye kujinasibisha na watu huwa ni  mmoja wao.” (Abu Daud)

Na katika Qur’an, Allah anatuonya: “Mkikufuru, basi Mwenyezi Mungu si mwenye haja nanyi, lakini hafurahii kufuru kwa waja wake. Na mkishukuru Yeye hufurahika nanyi. Wala  mbebaji habebi mzigo wa mwingine.” (Qur’an, 39:7).

Hii inaonesha dhahiri kuwa,  Allah na Mtume wametukataza tusisherehekee kwa namna yoyote sikukuu kama  hizi. Tutosheke na kauli ya Mtume (rehema na amani ya Allah zimfikie) alipotuambia:

Mtafuata nyendo za watu waliokuwa kabla yenu, shubiri kwa shubiri, hatua kwa hatua, hata kama waliingia kwenye shimo la mbulukenge mtawafuata.”

Tukasema: “Ee Mjumbe wa Allah Je, Unamaanisha Mayahudi na Manaswara?” Akasema: “Kwani nani zaidi yao?” (Bukhari na Muslim).

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close