2. Deen

Muziki: sanaa iliyolaaniwa mbinguni na ardhini

Muziki au nyimbo ni miongoni mwa sauti za Shetani (Iblis) aliyelaaniwa. Tangu zama na zama, shetani amekuwa akitumia ujahili wa watu na kuwapambia muziki kwa kuufanya kuwa pambo la dunia, na hivyo kuwanasa kirahisi katika mtego wake.

Lakini ili tujue ubaya wa muziki, ni lazima kwanza tumfahamu adui shetani na harakati zake, kwa sababu viwili hivyo (shetani na muziki) vinafanya kazi pamoja, na vinaishi nyumba moja Allah Ta’ala anasema kumwambia Iblis: “Na wachochee uwawezao katika wao kwa sauti yako, na wakusanyie jeshi lako la wapandao farasi na waendao kwa miguu. Na shirikiana nao katika mali na watoto, na waahidi. Na shetani hawapi ahadi ila ya udanganyifu.” (Qur’ an, 17:64).

Hii maana yake ni nyimbo, ngoma na kila aina ya muziki kama alivyosema Mujaahid katika tafsir ya Ibn Kathir. Na katika upokezi wake Imam Bukhari, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Watakuwepo watu katika umma wangu watakaojaribu kuhalalisha zinaa, uvaaji wa hariri, pombe na muziki.”

Baadhi ya watu watakuwa pembeni mwa mlima na mchungaji wao atawajia jioni na kuwaomba haja (fulani). Watasema: “Rudi kesho”. Allah atawaangamiza usiku, atawaangushia milima kisha atawabadilisha waliobakia wawe nyani na nguruwe na watabakia hivyo hadi Siku ya Kiyama.

Pamoja na makaripio hayo, inasikitisha kuona watu wengi wakiwamo Waislamu wameangukia kwenye janga la muziki. Waislamu wengi bado wanaimba taarabu na aina nyingine za muziki bila ya woga wala hofu. Na katika kutetea uovu wao huo, baadhi yao wanasema hakuna ubaya wowote wao kuimba muziki kwa sababu muziki ni ajira kama zilivyo ajira nyingine, pia ni sehemu ya burudani inayoweza kuwaondoshea watu majonzi na msongo wa mawazo.

Hizi ni fikra potofu ambazo shetani amewapambia watu ili kutimiza azma yake ya kuwazuia kutenda kheri. Shetani ameupamba muziki na kuufanya kuwa ni jambo jema kabisa. Hii ndio sababu aya nyingi za Qur’ an tukufu zinatuonya na kututanabahisha kuhusiana na muziki. Mathalan katika Surat Nahl (Qur’an, 16:63), Mwenyezi Mungu anaapa kwa kusema:

Wallahi! Sisi tulituma Mitume kwa umati zilizokuwepo kabla yako, lakini Shetani aliwapambia vitendo vyao. Kwa hivyo leo yeye ndiye rafiki yao; nao watapata adhabu chungu.”

MADHARA YA KUSIKILIZA MUZIKI

Kuamsha hisia za mwili

Muziki huweza kuamsha hisia za mwili na kumfanya mtu ashindwe kujizuia (self-control). Katika kumbi za muziki (disko), watu hupoteza uwezo wakudhibiti hisia zao kutokana na athari za midundo na hivyo kufanya mambo mengi maovu na ya aibu wakati wanapocheza muziki.

Muziki ni sababu ya unafiki

Muziki ni haramu na ni uovu, pia ni miongoni mwa maradhi ya moyo na kususuwaa kwa moyo (yani moyo kuwa mgumu), na kumzuilia mtu asitekeleze ibada ya swala na dhikri.Imam Ahmad (Allah amrehem) amesema:

Haunishangazi mimi muziki kwani unaotesha moyoni mbegu ya unafiki. Na huenda makruhu iliyopo katika maneno yao ni umakuruhu wa uharamu na sio wa kawaida.”

Kikwazo dhidi ya Qur’an

Muziki unazuia moyo kuisoma na kuisikiliza Qur’an tukufu. Imamu Ibnul Qayyimul Jauziyy (Alla amrehemu) amesema:

Na miongoni mwa vitimbi vya adui wa Allah (Iblis) na mitego yake ambayo amemtegea mtu aliyepungukiwa na akili na elimu ya dini, na mitego hiyo imezinasa nyoyo za wajinga na wabatilifu ni kusikiliza nyimbo, ngoma, makofi na muziki kwa ala zilizoharamishwa ambazo zinazuia nyoyo kuisoma na kuisikiliza Qur’an tukufu, na kuziingiza katika kushiriki mambo ya kihuni. Basi hiyo ndiyo Qur’an ya Shetani na ni pazia nzito baina yao (wanaosikiliza na wanaoimba muziki) na Allah.”

Hivyo ndugu yangu, usidanganywe na pumbao lenye msisimko wa muda mfupi na kuuza akhera yako ambayo ni ya milele, yenye kudumu. Shetani anafahamu faida za ibada ya kusoma Qur’an, adhkaar, kusikiliza mawaidha na nyinginezo na ndio maana anakupambia muziki ili usione umuhimu wa kuzitekeleza.

Vyovyote iwavyo, muziki hauwezi kukupa furaha na amani ya nafsi. Burudiko halisi lipo katika kumtaja, kumtukuza Mwenyezi Mungu na kushika sharia yake. Kujihusisha kwako na muziki ima kwa kutunga mashairi, kuimba, kucheza, kuuza ‘tape au CD’ n.k kunaweza kupelekea ubebe mzigo mkubwa wa madhambi kwako na kwa watu wengine.

Mwenyezi Mungu anasema: “Hakika sisi tunawafufua wafu, na tunayaandika wanayoyatanguliza, na wanayoyaacha nyuma. Na kila kitu tumekihifadhi katika daftari asili lenye kubainisha.” (Qur’ an, 36:12).

Hivi haikuingii hofu katika moyo wako kuwa huenda mwisho wako ukawa ni kuimba nyimbo badala ya kusema ‘Laa Ilaaha Illa Llah’, neno ambalo ukilitaja wakati wa kufa utaingia peponi?

Tafakari na chukua tahadhari kwa kutosikiliza muziki. Kama mwanadamu unapaswa kulinda akili yako kwa kutosikiliza mambo yasiyofaa ukiwamo muziki kwa sababu akili ndiyo inayotoa maamuzi yanayoamua mustakabali wa maisha yako ya sasa na yajayo huko akhera.

Tunamuomba Allah atujaalie kuwa miongoni mwa waja wake wasikiao mawaidha na kuyafanyia kazi. Ameen…

 

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close