2. Deen

Muonekano wa Uislamu kwa watu wa Kitabu na namna ya kuamiliana nao

Hakika Uislamu ni dini aliyokuja nayo Mtume Mtukufu Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) toka kwa Mwenyezi Mungu, Mola mlezi wa ulimwengu. Amesema Mwenyezi Mungu Aliyetukuka: “Bila ya shaka Dini mbele ya Mwenyezi Mungu ni Uislamu.” (Quran, 3: 19).

Na hii ni baada ya Mola wetu kuiridhia dini hii kwetu na pia kutimiza neema zake kwetu. Amesema Mwenyezi Mungu Aliyetukuka: “Leo nimekukamilishieni dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe ndiyo Dini.” (Quran, 5:3).

Uislamu ni dini ya rehema na ihsani. Imeenea rehema yake kwa viumbe vyote na kuenea ihisani yake kwa vitu vyote. Ihsani na rehema za Uislamu hazikuishia kwa Waumini wake peke yake, bali kwa watu wote, ikiwemo waliotofautiana na dini hii tukufu.

Amesema Mwenyezi Mungu Aliyetukuka: “Nasi hatukukutuma ila uwe ni Rehema kwa walimwengu wote.” (Qur’an 21: 107). Hakika, Mwenyezi Mungu amewaumba wanadamu na kuwagawanya katika makundi mawili, walioamini na makafiri.

Amesema Mwenyezi Mungu Aliyetukuka: “Yeye ndiye aliye kuumbeni. Miongoni mwenu yupo aliye kafiri, na yupo aliye Muumini. Na Mwenyezi Mungu anayaona mnayo yatenda.” (Quran, 64:2). Miongoni mwa wasio Waislamu wapo watu wa kitabu kama Mayahudi na Manaswara na wapo wasio na kitabu kama majusi na washirikina.

Qur’an Tukufu imebainisha kuwa, watu wa kitabu ni watu wa karibu mno kwetu kuliko wengine. Anasema Mwenyezi Mungu Aliyetukuka: “Hakika utawakuta walio shadidi kuliko watu wote katika uadui kwa walio amini ni Mayahudi na washirikina. Na utawakuta walio karibu mno kwa mapenzi ni wale wanao sema: Sisi ni Manasara. Hayo ni kwa sababu wapo miongoni mwao makasisi na wamonaki, na kwa sababu wao hawafanyi kiburi.” (Quran 5:82).

Hakika Uislamu unahimiza kuamiliana kwa wema na watu wa kitabu. Uislamu unamuamrisha mfuasi wake afanye mjadala mzuri na watu wa kitabu. Amesema Mwenyezi Mungu Aliyetukuka: “Wala msijadiliane na Watu wa Kitabu ila kwa njia iliyo nzuri kabisa, isipo kuwa wale waliodhulumu miongoni mwao. Na semeni: Tumeyaamini yaliyo teremshwa kwetu na yaliyo teremshwa kwenu. Na Mungu wetu na Mungu wenu ni Mmoja. Na sisi ni wenye kusilimu kwake.” (Quran 29:46).

Pia ameturuhusu Mwenyezi Mungu vyakula vyao, bali pia imehalalishwa kwa mwanamume Muislamu kumuoa mwanamke mtiifu miongoni mwa wanawake zao. Anasema Mwenyezi Mungu Aliyetukuka: “Leo mmehalalishiwa kila vilivyo vizuri. Na chakula cha walio pewa Kitabu ni halali kwenu, na chakula chenu ni halali kwao. Na pia wanawake wema miongoni mwa Waumini, na wanawake wema miongoni mwa walio pewa Kitabu kabla yenu, mtakapo wapa mahari yao, mkafunga nao ndoa, bila ya kufanya uhasharati wala kuwaweka kinyumba. Na anaye kataa kuamini bila shaka a’mali yake imepotea, naye katika Akhera atakuwa miongoni mwa wenye khasara.” (Quran, 5:5).

Kisha Mwenyezi Mungu amempa kila mtu uhuru wa kuabudu. Si halali kwangu wala haifai kwako kumlazimisha mtu au kumteza nguvu juu ya kuingia katika dini au kwenye Imani.

Mwenyezi Mungu aliweka kanuni hii kubwa nayo ndiyo inayotofautisha sheria zetu nzuri. Anasema Mwenyezi Mungu Aliyetukuka: “Hakuna kulazimishana katika dini.” (Quran 2:256). Na pia anasema: “Na sema: Hii ni kweli itokayo kwa Mola wako Mlezi. Basi atakaye, aamini. Na atakaye, akatae.” (Qur’an, 18:29). Na kisha akasema: “Nyinyi mna dini yenu, nami nina dini yangu.” (Qur’an, 109:6).

Na hapa unadhihiri utukufu wa Uislamu katika kuamiliana na wasio waislamu iwe kwa mazungumzo au kwa mwenendo na matendo. Amesema Mwenyezi Mungu Aliyetukuka: “Mwenyezi Mungu hakukatazini kuwafanyia wema na uadilifu wale ambao hawakukupigeni vita, wala hawakukutoeni makwenu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao uadilifu.” (Quran 60:8).

Na amesema tena: “Waite waelekee kwenye Njia ya Mola wako Mlezi kwa hikima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora. Hakika Mola wako Mlezi ndiye anaye mjua zaidi aliye ipotea Njia yake, na Yeye ndiye anaye wajua zaidi walio ongoka.” (Qur’an, 16:125).

Na ijulikane kwamba, Mwenyezi Mungu Aliyetukuka amesema na watu, kwa maana ya watu wote. Hapakusemwa kwa Waislamu wala kwa Waumini bali wameambiwa watu wote ili kueneza na kufikisha neno zuri, bila ya kuangalia dini na imani.

Kwa msingi huo, ni muhimu kwa Muislamu atoe kauli iliyo nzuri zaidi na iliyo bora. Iwapo kuna neno zuri na neno jingine zuri zaidi, basi Muislamu anatakiwa aseme lililozuri zaidi na aliache lililo zuri, tena kwa tamko la ubora zaidi. Mwenyezi Mungu anasema: “Na sema kuwaambia waja wangu waseme yaliyo mazuri zaidi.” (Qur’an 17:53). Kwa yakini, Uislamu umeamrisha kuamiliana vizuri na wasio-waislamu kwa kuwalingania kuingia katika dini hii tukufu ambayo inahifadhi dini na kuwapa uhuru.

Ametupigia mwenyewe Mtume wetu mfano bora katika wema wa kuamiliana na wa wasio waumini. Imepokewa kutoka kwa Aisha kwamba, walikuwa Mayahudi wakimsalimia Mtume (rehema za Allah na Amani zimshukie) kwa kusema: “Kifo kiwe juu yako.” Akafahamu Aisha maneno yao, naye akasema: “Juu yenu kifo na laana.” Mtume akasema: “Pole pole ewe Aisha hakika Mwenyezi Mungu anapenda upole katika mambo yote.”

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close