2. Deen

Muigeni Nabii Yusuf, wahasibu waaswa

Wasomi Waislamu waliosomea fani ya Uhasibu nchini wameaswa wajitambue kwamba na wamuige Nabii Yusuf katika kazi zao za uhasibu aidha serikalini, katika makampuni na mashirika ya umma au yale ya watu binafsi.

Hayo yalisemwa na Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Jumuiya na Taasisi za Answar Sunnah Tanzania (BASUTA), Sheikh Muhammad Issa, wakati akizungumza na wahitimu wa ngazi za Astashahada, Stashahada na Shahada katika fani mbali mbali ikiwemo Uhasibu (Accountancy) katika Chuo cha Uhasibu (TIA) jijini Dar es Salaam.

“Ninyi mna mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi, lakini pia mnaweza pia kuwa na mchango mkubwa katika kudumaza maendeleo ya nchi iwapo mtatumia fani yenu kufanya ufisadi,” alisema Sheikh Muhammad.

Sheikh Muhammad aliwaasa wahitimu hao kujitambua kwamba wao ni Waislamu kwanza kisha waitumie fani yao ya uhasibu kwa maslahi ya taifa kama alivyofanya Nabii Yusuf (amani ya Allah imshukie).

“Nabii Yusuf aliomba kazi ya Uhasibu na Utunzaji Hazina chini ya Mtawala wa Misri. Katika kuelezea sifa zake (CV), Yusuf alisema “… hakika mimi ni Mhifadhi (Mhasibu) Mwaminifu.” [Qur’an 12:55].

Sheikh Muhammad alisema, kinachokosekana kwa wahasibu wengi ni sifa ya uaminifu na kuwafanya wengi kutumia ajira wanazopata kuliibia taifa mabilioni ya fedha

“Mkurugenzi wa Kampuni, Waziri, Katibu Mkuu, Kamishna na mtu mwingine yeyote hawezi kuiibia serikali au kampuni pasina kuwahusisha ninyi wahasibu. Kwa hiyo msikubali kutumika kwa kalamu zenu kuiibia serikali au mtu yeyote, muigeni Nabii Yusuf,” alisisitiza Sheikh Muhammad.

Awali, akizungumza katika mahafali hayo, Sheikh wa Wilaya ya Temeke, Sheikh Zailai Mkoyogoye, aliwaasa wahitimu hao kuishi maisha ya Kiislamu popote pale watakapokwenda.

“Kuweni mabalozi wazuri wa Uislamu huko muendako ili kuupa heshima Uislamu na jamii kwa ujumla”, alisema sheikh Zailai.

Naye mlinganiaji Sheikh Mapande akiongea katika mahafali hayo kuhusu mada ‘Wajibu wa msomi Muislamu’ alisema: “Elimu yao iwe dira ya kuonesha kuwa yuko aliyewawezesha kufika pale walipofika na anapasa kusujudiwa” alisema.

Aliwataka wahitimu kuitumia elimu waliyoipta kwa malengo ya kulitumikia taifa lakini hasa kwa ajili ya dini yao ya Uislamu. Mbali na wahitimu, mahafali hayo yalihudhuriwa na wazazi na walezi wa wanafunzi waliohitimu pamoja na wanajamii na viongozi wa Kiislamu.

Akieleza masikitiko yao, vijana wa Kiislamu chuoni hapo walisema kwamba changamoto kubwa waliyonayo ni kukosa msikiti wa kufanyia ibada zao baada ya ule wa muda uliokuwepo kubomolewa na chuo.

Walitumia mahafali hayo kuchangisha fedha kwa ajili ya safari ya Kida’wah watakayoifanya vijijini mkoani Morogororo na kwa pamoja zilichangwa shilingi milioni moja uchangishaji ukiongozwa na Sheikh Muhammad Issa.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close