2. Deen

MAISHA YA MASWAHABA: Salmaan al-Faarisy (as) -2

Kutoka katika kitabu,‘Suwarun min hayati swahaba,’ Salmaan Alfarsiy, Swahaba mtukufu, anaendelea kusimulia, kuwa baada ya kuishi Ammuuriya na mwalimu wake muda aliojaaliwa, ulifika muda wa mwalimu kuiaga dunia.

Salmaan Alfaarisy (Allah amridhie) alimuuliza: “Unaniusia nini baada ya wewe kuondoka?” Mwalimu wake akamjibu: “Sidhani kama kumebaki mtu yoyote juu ya mgongo huu wa ardhi aliyeshika dini sahihi hii tuliyoishika sisi. Lakini sasa zimeshafika zama za kutokea Mtume katika jamii ya Waarabu. Atakuja na dini (mafunzo) ya Ibrahim (amani ya Allah imshukie). Kisha atahamia nchi yenye mitende mji wenye maumbile ya changarawe. Na utamjua kwa alama zake hazijifichi.

Alama za Mtume huyo

Kuhusu alama za Mtume huyo, aliambiwa: “Anakula zawadi wala hali sadaka. Katikati ya mabega yake kuna muhuri wa Utume,” akaongeza: “Basi kama utaweza kufika katika mji huo, nenda.”

Salmaan aenda Arabuni

Salmaan anasema aliishi siku kadhaa Ammuuriya. Ukaja msafara wa kibiashara wa Waarabu, nikawaambia: “Kama mtakubali kwenda nami mpaka nchi za Waarabu nitakupeni n’gombe na kondoo wangu hawa.” Wakasema, “Sawa.” Wale wafanyabiashara wakamchukua na akawapa wanyama. Anasimulia: “Tulipofika Wadilquraa (mahali kati ya Madina na Sham), waliniteka na kuniuza kwa Yahudi mmoja nikawa mtumwa wake.”

Salmaan ndani ya ardhi ya Utume

Salmaan anasema kwamba hazikupita siku nyingi Yahudi aliyemnunua alitembelewa na (nduguye) mtoto wa ammi yake kutoka Banii Quraidha (moja makabila ya kiyahudi yaliyokuwa Madina). Naye akamuuza kwa ndugu yake huyo, ambaye naye alimchukua hadi Yathriba, yaani Madina.

Akizungumzia alama za mji huo, Salmaan anasema:

Nikaiona mitende mirefu vilevile alivyonisifia sahibu wangu kule Ammuuriya. Nikaishi hapo nikiwa mtumwa. Wakati huu Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alikuwa Makka akiwalingania watu lakini kutokana na majukumu ya kiutumwa sikuwa nikipata habari zake vya kutosha.” (uk 112)

Salmaan ajua Mtume yuko Madina

Hazikupita siku nyingi Mtume aliwasili Madina, Salmaan anasimulia: “Nikiwa juu ya mtende, na bwana wangu akiwa amekaa chini yake, mara alimjia mtoto wa baba yake mdogo na kumwambia, ‘Mungu amewalaani Banu Qayla (akiwa na maana ya Awsi na Khazraj)! Hivi sasa wamejikusanya Quba wakiwa pamoja na mtu aliyefika leo kutoka Makka akidai kuwa yeye ni Mtume!’

Aliposikia maneno yale, Salmaan alishikwa na kitetemeshi cha homa kikali mpaka akahofia kuanguka. Akateremka haraka na kuanza kumuuliza yule mtu aliyeleta taarifa: “Unasemaje? Hebu rejea ile habari. . .” Bwana wake alikasirika na kumpiga kibao, kisha akamwambia kwa ukali: “Yanakuhusu nini hayo. rudi kwenye shughuli yako.”

Salmaan akutana na Mtume

Ilipofika jioni, Salmaan alikwenda kumtafuta Mtume akibeba baadhi ya tende alizopanga kumpelekea ili kuhakikisha ukweli wa utume wake. Akaingia kwa Mtume na kumwambia: “Nimesikia kwamba wewe ni mtu mwema, na una wafuasi wageni wana shida. Basi nimekuletea tende kidogo hizi sadaka.” Kisha akamsogezea. Salmaan anasimulia kuwa, Mtume aliwapa tende zile Maswahaba zake na kuwaambia: “Kuleni,” lakini yeye kamwe hakula. Akajisemea moyoni, hili moja limetimia.

Salmaan anasema, alipotoka hapo, alienda kukusanya tende nyengine. Mtume alipoondoka Quba na kuingia mjini Madina, alimfuata tena na kumwambia: “Mimi nimekuona huli sadaka, lakini leo nimekuletea tende kama zawadi.” Mtume akala na akawaamrisha Maswahaba wake wakala pamoja. “Nikasema kimoyomoyo: na hili la pili limetimia.”

Siku nyingine Salmaan alimfuata Mtume akiwa Baqii (sehemu ya makaburi ya Waislamu), akamkuta amekaa akiwa amevaa maguo mawili mazito. Akamsalimia kisha akazunguka kwa nyuma ya mgongo wake ili aone alama ya mwisho (ya tatu) ambayo alimsifia mwalimu wake kule Ammuuriya. Salmaan anasema: “Mtume alifahamu lengo langu alikivua kishali chake nikauona muhuri wa utume mgongoni kwake, nikamkumbatia na kulia kwa furaha.” Mtume kuona hali ile alimuuliza Salmaan: “Una nini na nini habari yako
wewe?” Salman akajibu: “Nikamsimulia Mtume kisa changu kwa urefu kikamshangaza vya kutosha na kufurahishwa sana.” “Mtume alitaka niwasimulie pia Maswahaba zake, nikafanya hivyo.

Mkasa wangu uliwashangaza na kuwafurahisha sana pia.” Salmaan akasilimu na kuanzia hapo alipata umaarufu na kupendwa na Waislamu Madina nzima. Mtume alimtaka Salmaan aandikiane na bwana wake (Yahudi) kumuacha huru, na ilifanyika hivyo. Salmaan alitakiwa ampandie bwana wake mitende mia tatu na kumtoza wakia 40 za dhahabu.

Waislamu walimsaidia kutekeleza hayo na Salmaan akawa huru huku akiwa amejivunia neema kubwa ya ajabu ambayo ni Uislamu. Hapa ndipo safari ya kuitafuta dini ya haki ilipomfikisha Swahaba huyu mkubwa Mfursi Salmaan (mwenda nyuma ya uhakika).

Itaendelea  inshaaAllah

Maisha ya Maswahaba: Salmaan Al-Faarisy sehemu ya kwanza👇👇👇

MAISHA YA MASWAHABA: Salmaan al-Faarisy (Allah amridhie)

 

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close