2. Deen

Lugha ya kiarabu, ilikotoka, ilipo na inakoelekea!

Kiarabu ni moja ya lugha kuu zilizobaki kutoka familia ya lugha za Kisemitiki (Semitic). Inazungumzwa upande wa Mashariki mwa bara Arab na Magharibi mwa bara Arab, eneo linalojulikana zaidi kama Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini, pia Mashariki na Magharibi mwa Afrika.

Kiarabu ni lugha ya nne mashuhuri zaidi ulimwenguni baada ya Kiingereza, Kifaransa na Kihispania. Kiarabu ni lugha rasmi ya wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League), ambayo ni mwamvuli wa nchi 21 kuanzia Oman katika bahari ya Arabuni, mpaka Morocco na Mauritania katika bahari ya Atlantiki.

Kiarabu pia kinazungumzwa kama lugha ya kwanza au ya pili katika nchi zilizo jirani na ulimwengu wa Kiarabu kama Chad, Mali, Senegal, Cameroon, Kaskazini mwa Nigeria, Sudan Kusini, Ethiopia, Eritrea, Iran Magharibi, Kusini mwa Uturuki na hata Israel, ambako lugha nyingine ya kisemitiki, Hebrew, ndiyo ya kwanza rasmi, wakati Kiarabu ikiwa lugha ya pili.

Kwa kuongezea hapo, kuna jamii za Kiarabu zinazoishi Ulaya Magharibi, Marekani na Kusini Mashariki mwa Asia, ambazo bado zinatumia lugha ya Kiarabu katika maisha yao ya kila siku. Kuna takriban watu Milioni 450 duniani leo wanaozungumza Kiarabu!

Lugha nyingine za Kisemitiki, ambazo bado zipo hai mpaka leo ni Amharic, inayozungumzwa nchini Ethiopia, Hebrew inayozungumzwa Israel, Tigrinya inayozungumzwa Eritrea, Maltese inayozungumzwa kwenye kisiwa cha Malta, kilichopo kwenye bahari ya Mediterranean, na Aramaic inayozungumzwa na baadhi ya jamii za Kikristo nchini Syria, kikiwemo kisiwa mashuhuri cha Ma’lula.

Lugha za Kisemitiki, ziliibukia
kule ambako sasa ndiyo Iraq na Syria
Magharibi, mwishoni mwa millenia
ya tatu kabla ya Yesu (BC). Za kwanza
kuibuka zilikuwa ni lugha za Akkadian
na Ebla. Baadaye, lugha za Ammorite
na Canaanite ziliibuka Syria na kwenye Peninsula ya Uarabuni. Wakati wa Millenia ya pili baada ya Yesu (AC), herufi (alphabet) za awali za Kisemitiki ziliibuka. Herufi hizi ziliendelea wakati lugha ya Aramaic ilipokuwa mashuhuri katika eneo ambalo sasa linajulikana kama Mashariki ya Kati.

Aramaic ndiyo iliyokuwa lugha ya Yesu, kama tunavyoona pale aliposema, kwa mujibu wa Biblia, wakati alipokamatwa na askari wa Kirumi, “Eloi Eloi lama Sabakhtani” (Mungu wangu Mungu wangu mbona umeniacha). Aramaic ilibaki kuwa lugha ya ibada za Kikristo mpaka karne ya 15. Lugha ya Kiarabu, kama tunavyoijua leo, ilianza taratibu mwanzoni mwa millenia ya kwanza baada ya Yesu, na ikakomaa zaidi wakati Qur’an ilipoteremshwa karne ya saba.

Waarabu walijivunia sana lugha yao na walidhani kwamba wao peke yao ndiyo wenye uwezo wa kujieleza kwa ufasaha. Kwa hiyo, waliwaita wasio Waarabu ‘Ajm’, ikiwa na maana ya watu wasioweza kuzungumza au kujieleza kwa ufasaha.

Lugha ya Kiarabu iliendelea sana wakati Qur’an ilipoteremshwa kwa Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie). Ilikuwa na washairi mashuhuri ambao kazi zao ziliandikwa kwenye ngozi na kuning’inizwa maeneo matakatifu ya Makka. Kulikuwa na washairi wazito kama Imra’ul-Qais, ambao ushairi wao unaweza kufanana na kazi bora kabisa katika historia ya ulimwengu. Huu ushairi wa kipindi cha kabla ya Uislamu, bado ni alama muhimu ya sarufi ya Kiarabu na semantiki. Sarufi ya Kiarabu pia iliendelea kikamilifu muda mfupi kabla ya kufunuliwa Qur’an.

Lafudhi iliyozungumzwa na kabila la Kuraish mjini Makka, ilidhaniwa kuwa ndiyo safi zaidi na iliyoendelea sana. Waarabu wengine waliifahamu. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alikuwa na kawaida ya kutembelea masoko mashuhuri ya msimu ya Arabia, ambapo aliwavutia washairi wa Kiarabu na wazungumzaji mashuhuri, wakati alipokuwa akisoma aya za Qur’an na kuwalingania watu Uislamu.

Hatuoni ishara yoyote ndani ya vitabu vya historia kwamba Waarabu waliwahi kulalamika kwamba maneno yaliyokuwa yakitamkwa na Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie), yalikuwa hayaeleweki kwao.

Waarabu wanaieleza lugha yao kama “lugha ya Dhwad”. “Dhwad” ni sauti ya kipekee na herufi ambayo hutumiwa na Waarabu peke yao. Kiarabu ni tofauti sana katika utaratibu wa matumizi ya maneno yenye mizizi ya tabia tatu (jidhr), ambayo hutumika kimahesabu kukusanya mamia ya maneno, majina na vitendo.

Mtu anayejua lugha ya Kiarabu ataelewa vizuri maana ya umbile lolote la maneno, majina na vitendo, kwa kuzingatia mzizi wa tabia tatu. Baada ya ujio wa Uislamu, ushindi wa Waarabu, na Waarabu kuhamia kwenye maeneo waliyoshinda, lugha ya Kiarabu ilisambaa kwenye ardhi zingine, zikiwemo zile himaya ambazo lugha zingine za Kisemitiki zilikuwa mashuhuri.

Kama matokeo ya ushindi huo na uhamiaji, Kiarabu kilisambaa maeneo yote ya Afrika Kaskazini, kuanzia Misri mpaka Morocco na Mauritania, na hata Andalusia (Uhispania) ambako Kiarabu kilistawi kwa karne saba. Baadhi ya kazi bora kabisa za Kiarabu katika fasihi na Uislamu ziliandikwa Andalusia.

Mpaka karne ya 16, Kiarabu kilibaki kuwa lugha ya kimataifa (international lingua franca). Matokeo ya hilo, istilahi nyingi za Kiarabu za kibiashara, kisayansi na kitabibu zimeingia kwenye baadhi ya lugha za Ulaya na bado zinatumika mpaka leo. Istilahi kama admiral (amir al-bahr), alchemy (al-kimiya), alcohol(al-kuhl), algebra (al-jabr), algorithm (al-Khawarizmi), alkali (qaly), almanac (al-munakh), cheque (shakk), carat (qirat), mattress (matrah) saffron (Za’faran), Satin (Zaitun), Sofa (Suffah) na zingine nyingi kama hizo, zote kimsingi ni maneno ya Kiarabu. 

 

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close