6. Kutoka Katika Quran na Sunnah

Wito wa Allah kwa Waumini

Allah ‘Azza Wajallah’ anatusimulia kisa cha majini waliokuwa wanamsikiliza Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) akisoma Qur’ an. Baada ya kurejea kwenye makazi yao, majini waliwahimiza wenzao kuitikia wito wa Allah.

Majini walisema kuwaambia wenzao: “Enyi kaumu yetu! Hakika sisi tumesikia Kitabu kimeteremshwa baada ya Musa kinachosadikisha yaliyo kabla yake, kinaongoza kwenye haki na kuelekeza katika njia iliyonyooka. Enyi kaumu yetu! Muitikieni mlinganiaji wa Allah na mumuamini. (Allah) atakusameheni madhambi yenu na atawakinga na adhabu chungu. Na wasiomuitikia mlinganiaji wa Allah hawatashinda katika ardhi, wala hawatakuwa na walinzi mbele yake. Hao wamo katika upotovu ulio wazi.” [Qur’ an, 46: 3o–32].

Katika ufafanuzi wake kuhusu aya hizi, Imam Ibn Kathir (Allah amrehemu) amesema: “Katika aya hizi kuna dalili kuwa Allah alimtuma Nabii Muhammad (rehema na amani zimshukie) kuja kuwalingania dini wanadamu na majini.” [Rejea tafsiri ya Ibn Kathir].

lah iweje binadamu tushindwe! Allah na Mtume wake wametutaka tuitikie wito wao kwa kuwatii na kujiepusha na shari za shetani.

“Enyi mlioamini! Muitikieni Mwenyezi Mungu na Mtume anapokuitieni jambo la kukupeni uzima wa milele. Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu huingia kati ya mtu na moyo wake na hakika kwake Yeye (Allah) mtakusanywa.” [Qur’ an, 8:24].

Kazi ya Mitume

Mwenyezi Mungu Mtukufu aliwaleta Mitume na Manabii ulimwenguni na akawapa nguvu na miujiza mbalimbali ili waweze kuwaaminisha watu yale wanayowahubiria. Mwenyezi Mungu anawazungumzia Mitume wake kwa kusema:

“Mitume hao ni wabashiri na waonyaji ili watu wasiwe na hoja juu ya Mwenyezi Mungu baada ya kuletewa Mitume. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Mwenye hekima.” [Qur’ an, 4:165].

Allah kwa hekima yake amejaalia kuwepo kwa makundi mawili ya watu (kundi la peponi na kundi la motoni) na akabainisha njia ya kheri na ya shari kupitia Mitume wake na vitabu alivyowateremshia, kisha akampa mwanadamu uhuru wa kuchagua njia aipendayo.

Na hakika si vinginevyo, wenye kufanya maasi watapata adhabu chungu Siku ya Kiyama kama anavyosisitiza ndani ya Qur’ an: “Na hakika wenye kuasi bila ya shaka watapata marejeo maovu kabisa, nayo ni Jehannam! Wataingia humo. Nacho hicho ni kitanda kiovu mno cha kulalia. Ndiyo hivi! Basi na wayaonje maji ya moto na ya usaha na adhabu nyinginezo za namna hii.

Hili ndilo kundi litakaloingia pamoja nanyi. Hapana makaribisho mema kwao. Hakika hao wataingia motoni. Waseme: Lakini nyinyi hamna mapokezi mazuri! Nyinyi ndiyo mliotusababibishia haya, napo ni pahala paovu kabisa! Waseme: Mola wetu Mlezi! Aliyetusabibisha haya mzidishie adhabu mara mbili motoni. Watasema: Tuna nini hata hatuwaoni wale tuliowahesabu kuwa ndiyo waovu? Tulikosea tulipowafanyia masihara, au macho yetu hayawaoni? Hakika hayo bila ya shaka ndiyo mahasimiano ya watu wa motoni.” [Qur’ an, 38:55–64].

Hali ilivyo sasa

Wanadamu tumepuuza mafundisho ya dini na badala yake tunafuata matamanio ya nafsi zetu. Wengi wetu hatuko tayari kuitika wito wa walinganiaji na tumehiyari kumkufuru Allah.

Licha ya Uislamu kuharamisha zinaa, ulevi, kamari na riba, wapo miongoni mwetu wanaofanya maovu hayo bila hofu wala woga. Kinachosikitisha zaidi ni kwamba wapo Waislamu wanaoendesha maisha yao kwa kutegemea biashara haramu ya pombe, bangi, shisha, kucheza kamari na nyinginezo ambazo Allah na Mtume wameziharamisha.

Muongozo wa Mtume

Allah ‘Azza Wajallah’ na Mtume wake wametutaka tufuate njia ya sawa (Uislamu) ili tufanikiwe hapa Duniani na Akhera tuendako. Allah anasema:

“…hii ni njia yangu iliyonyooka, basi ifuateni. Na wala msifuate njia nyinginezo zitakufarikisheni na njia yake. Hivyo ndivyo alivyokuusieni (Allah) ili muwe wachamungu.” [Qur’ an, 6:153].

Na katika hadith iliyosimuliwa na An–Nawwaas bin Sam’aan (Allah amridhie), Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ametufahamisha kuwa Allah ametoa mfano wa Swiratwul Mustaqiym (njia iliyonyooka), na pemebeni mwa njia hiyo kuna kuta mbili zenye milango ya kutokea.

Katika milango hiyo kuna mapazia yaliyoteremshwa chini na mwanzoni mwa njia kuna mlinganiaji anayesema: “Enyi watu! Njooni muingie katika njia iliyonyooka wala msigawanyike. Na katika njia ya juu kuna mlinganiaji mwingine anayemwambia mtu anayetaka kufungua mojawapo ya milango: ‘Ole wako! Usifungue mlango huu kwani ukiufungua utaingia humo.’”

Kisha Mtume akafafanua maneno yake hayo kwa kusema: “Njia iliyonyooka ni Uislamu. Kuta mbili ni mipaka ya Allah na milango iliyofunguliwa ni yale yote aliyoyaharamisha Allah. Mlinganiaji aliyekaa mwanzoni mwa njia ni kitabu cha Allah (Qur’ an) na mlinganiaji aliyekaa juu ya njia ni mawaidha yaliyopo katika nyoyo za Waislamu.” [Ahmad].

Katika hadith hii, Allah Mtukufu anatutaka tumuelekee Yeye peke yake kwa kuingia katika dini yake (Uislamu) kisawasawa ili tupate makazi mema kesho Akhera.

Kuitika wito wa Allah

Kuitika wito wa Allah maana yake ni kutekeleza amri zake ikiwamo sala tano, funga (swaumu), kwenda hijja, kuamrisha mema na kukataza maovu na kuacha mambo maovu kama ulevi, uzinzi, kula riba, kula mali za watu kwa njia ya haramu na mengineyo.

Mwenye kuitika wito wa Allah huepukana na mtihani wa kufuata matamanio ya nafsi na pia huepukana na kufanya maasi. Katika hii dunia wapo watu wengi walioamua kumtii na kumuabudu shetani badala ya Mola aliyewaumba. Aghalabu watu hawa hupindisha sharia za Allah na kufanya mambo yenye kuridhisha nafsi zao.

Mbali na hao pia wapo waliowekeza muda wao mwingi katika kutafuta mali. Allah anauliza:

“Mmeshughulishwa na kutafuta wingi (wa mali). Mpaka mje makaburini. Sivyo hivyo, hivi punde mtajua,” [Qur’ an, 102:1–3].

Haya ni maonyo ya Mwenyezi Mungu juu ya wale waliowekeza muda wao katika kuishughulikia zaidi Dunia kuliko Akhera. Ni vema tukazingatia maneno hayo ya Allah kwa kuitikia wito wake ili tuwe watumishi wema na waaminifu kwake.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close