6. Kutoka Katika Quran na Sunnah

Uislamu Unakataa Vurugu na Aina Zote za Misimamo Mikali

Ukati na kati (uwastani) ni sifa mojawapo kuu ya sheria takatifu ya Kiislamu. Sheria hii inasifika kwa usamehevu, ulaini na kuhurumiana na kuendana maumbile sahihi ya mwanadamu.

Uislamu ni dini inayopendelea zaidi ukati na kati katika mambo yake yote yaani kidini, kiibada, kihukumu, katika miamala yake na kadhalika.

Kwa hiyo, Mwenyezi Mungu Aliyetukuka amebainisha kuwa huu ni umma wa wastani na hata mbinu zake ni za kiwastani – wastani. Mwenyezi Mungu anasema:

“Na vivyo hivyo tumekufanyeni muwe Umma wa wastani.” [Quran, 2:143].

Kwa mujibu wa aya hiyo, umma wa Kiislamu ni umma wa wastani ambao unakuwa mashahidi juu ya watu wote kwa uadilifu na kuwaelekeza kwenye maadili mema.

Pia, Uislamu ni dini ya wepesi na ulaini. Si dini ya kuwashadidishia watu na kuwalazimisha kufanya wasiyoyaweza. Uislamu ni dini ya uwiano baina ya mahitaji ya kimwili na roho.

Muislamu haruhusiwi kujizuia vitu vilivyo halali kwake, bali anatakiwa kujikurubisha kwa Mola wake kupitia wajibu, sunna na mubaha.

Kwa maana hiyo, ukati na kati (wastani) ni kuhakikisha kunakuwa na uwiano katika kuendesha mambo ya viumbe vyote, na kutokana na matakwa ya Mwenyezi Mungu na Sunna na hekima yake aliyoipitisha na kuipanga tangu hapo awali.

Uwiano huu unamaanisha wastani na kusawazisha baina ya vitu vyote na kuvifanya vikamilishane. Uwiano huo ndio kaida ya msingi na sifa kuu ya ukati na kati. Uwiano huu ukikosekana, basi huo uwastani unakuwa umekosa nguzo yake na msingi. Matokeo ya hali hiyo ni kujitokeza upendeleo na pia kukosekana uadilifu na hivyo uwiano kupotea.

Kwa jumla, kupendelea ncha moja kuliko nyingine kunakataliwa katika Uislamu kwani kama tulivyotaja, dini hii, ni ya wastani na uadilifu bila kupunguza wala kuongeza. Hakika ijulikane kuwa, kukosekana uwiano na usawa ni chanzo cha matatizo mengi.

Sura mbalimbali za ukati na kati katika Uislamu

Ishara za wastani katika Uislamu na sura zake ziko nyingi. Miongoni mwa sura hizo ni:

Mosi: Uwastani na ukati na kati wa Uislamu katika sheria zake unadhihirika katika sheria kama vile kufuata mbinu ya kutoa hukumu kidogo kidogo.

Moja ya dalili za rehma ya Mwenyezi Mungu aliyokuja nayo Mtume ni sheria ya Kiislamu ambayo haikutoa agizo au katazo mara moja, bali kidogo kidogo ili Waislamu waweze kutekeleza lile agizo kirahisi na kuzoea kuliepuka (au kulifanya) na hatimaye kuachana nalo kabisa.

Sheria ya Kiislamu ilifuata mbinu hiyo katika hukumu nyingi, hasa katika makatazo au mambo yaliyoharamishwa.

Mfano wa hayo, ni kama vile amri ya kuondoa masanamu katika eneo la Ka’aba. Hukumu hiyo ilitolewa na kutekelezwa taratibu ambapo inajulikana kuwa, mwishowe masanamu yaliondolewa siku Mtume alipoingia Makka akiwa mshindi siku ya Al-Fat-h.

Mfano mwingine ni katazo la ulevi ambao uliharamishwa kidogo kidogo.Mwanzoni wa Uislamu, sheria ya Kiislamu ilijikita zaidi katika kuharamisha maovu kuliko kuamrisha mema kwa kuwa kuanzisha jamii mpya inahitaji kuondoa athari mbaya za enzi zilizopita.

Kwa hiyo, sheria ilianza kuharamisha mabaya haya kidogo kidogo kama njia ya kuziandaa nafsi (hasa za waliozoea kufanya mabaya haya) zikubali hukumu za Mwenyezi Mungu na hatimaye ili kuhakikisha mwitikio wa hukumu za dini kwa walengwa.

Pia, mfumo huo wa kuharamisha na kutoa makatazo kidogo kidogo unalenga kutoa hukumu kwa ulaini na upole na kuwapa walinganiwa fursa ya kupata nafuu kutokana na mabaya haya ambayo ni kama maradhi yanayohitaji muda kiasi mpaka kufikia kupona kabisa.

Mfumo wa kutoa hukumu za kisheria kidogo kidogo ulihitajika hasa katika mambo yaliyoendelea kwa muda mrefu katika jamii ya kabla ya Uislamu kama ulevi na ibada ya masanamu.

Yeyote anayetafakuri kuhusu hukumu zote za sheria ya Kiislamu hatapata ugumu kutambua kuwa hukumu hizo zimetegemea sana urahisishaji na wepesishaji.

Urahisishaji na wepesishaji ndiyo mbinu ya Mwenyezi Mungu na Mtume. Pia, ni sifa ya msingi ya dini hii adhimu.

Sifa takatifu za dini hii zinadhihirika wazi katika Sira ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) na shime aliyokuwa nayo katika kufanya wepesi na upole. Mbinu hii pia ilidhihirika pale Mtume alipowahimza Maswahaba kufuata mbinu hiyo hiyo katika da’awa na katika kutoa hukumu za kisheria.

Ushahidi wa wepesishaji

Ushahidi wa kuthibitisha upole wa dini na wepesi wake ziko nyingi. Mwenyezi Mungu anasema:

“Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito.” [Qur’an, 2:185]. Anasema pia:“Hapendi Mwenyezi Mungu kukutieni katika taabu.” [Qur’an, 5: 6]. Anasisitiza pia: “Wala hakuweka juu yenu mambo mazito katika Dini.” [22: 78].

Vile vile, katika sunna za Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie), jambo hilo hilo limesisitiziwa sana ambapo Abu Huraira amesimulia kuwa Mtume amesema:

“Hakika dini hii ni nyepesi, na hakuna yeyote atakayebishana na dini ila atashindwa. Kwa hiyo, fanyeni ulaini na upole na jitahidini zaidi katika ibada nyakati za asubuhi na jioni na sehemu ya usiku.”

Pia, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alikuwa mfano bora wa upole na ulaini, ambapo hiyo ndiyo ilikuwa sifa yake kuu, kama alivyoeleza Bi. Aisha (Allah amridhie) aliposema:

“Mtume akiwa anachagua baina ya mambo mawili alikuwa anachagua lililo rahisi zaidi.”

Pili: Wastani wa Uislamu katika da’awah. Kwa kweli ulingianiaji wa Uislamu una mbinu maalum ambazo kimsingi zinategemea upole na usamehevu.

Daawa ya Kiislamu haitumii nguvu kama wanavyodai baadhi ya wasiojua chochote kuhusu Uislamu.

Ushahidi wa hili ni ukweli kwamba, wengi waliojiunga na Uislamu hawakulazimishwa kufanya hivyo bali waliona na kutambua utukufu wa dini hiyo na usamehevu wake. Kwa hakika historia ya Kiislamu haikushuhudia tukio hata moja la kuwalazimisha au kutishia watu waingie katika dini, hata katika hali ya vita na maadui.

Zaidi ya hayo, lengo kuu ya dini ni kuwaongoza watu wote kwenye njia ya Mwenyezi Mungu ambayo ni njia ya amani, utulivu na uhuru. Kwa hiyo, da’awa ya Kiislamu haikuhusishwa na Waarabu peke yao kwani Uislamu ni dini iliyoteremshwa kwa wanadamu wote.

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ndiye rehma kwa ulimwengu. Hivyo, mbinu aliyoitumia katika kulingania ilitokana na kauli ya Mwenyezi Mungu:

“Waite waelekee kwenye Njia ya Mola wako Mlezi kwa hikima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora. Hakika Mola wako Mlezi ndiye anaye mjua zaidi aliye ipotea Njia yake, na Yeye ndiye anayewajua zaidi walio ongoka.” [Qur’an, 16: 125]

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close