6. Kutoka Katika Quran na Sunnah

Uislamu Siyo Wafanyacho Waislamu Bali Qur’an na Sunna

Uislamu siyo kile wafanyacho Waislamu; bali ni kile Waislamu wanachopaswa kufanya. Maneno haya yapigiwe mstari siyo tu na kila mtu bali kila mwenye mamlaka pia ayatie katika faili lake. kwa sababu ni sahihi. Matendo ya Waislamu yanapaswa kupimwa katika mizani ya maelekezo sahihi ya Uislamu!

Uislamu siyo kile wafanyacho Waislamu; bali ni kile Waislamu wanachopaswa kufanya ni kauli yenye wigo mpana sana ndiyo maana ni Waislamu amba0 hufikishwa Mahakamani kwa sababu ya kufanya makosa mbalimbali na siyo Uislamu!

Uislamu ni nini basi?

Uislamu wenyewe ni maneno ya Allah yaliyotukuka yaliyomo ndani ya Kitabu Kitukufu cha Allah Aliyetukuka. Uislamu vilevile ni Maneno ya Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) ambaye hakuwa akinena kwa matashi yake. Maneno hayo yameandikwa katika vitabu maarufu vya Hadith!

Hapana shaka kuwa Qur’an ni Kitabu Kitukufu cha Allah na wala ‘Utukufu’ wake hauhitaji kuhakikiwa au kuthibitishwa na binadamu!

Viongozi wa Kiislamu mnapoapa kwa kushika Qur’ani ina maana gani? Pamoja na kutambuliwa kwa dini yenu, kuna ishara nyingine kuwa Kitabu hicho mnachokishika mnapoapa ni Kitukufu! Na hakika ni Kitukufu tena sana!

Nimetanguliza kusema kuwa Uislamu ni Qur’an na Sunna Sahihi. Hivyo kila kinachotokea, Muislamu anapaswa kukipima katika mizani za vitu hivi viwili!

Hata Wanazuoni wa Kiislamu wanachofanya wanapotoa fat’wa hunukuu katika Qur’an na Sunna au hutumia ‘Kanuni’ na ‘Misingi’ iliyowekwa na Qur’an na Sunna. Kwa kutumia ‘Misingi’ na ‘Kanuni’ hizo wanachosema ni lugha isiyokuwa ya moja kwa moja kuwa “Hivi tunavyosema ndivyo alivyosema Allah na Mtume wake.”

Tuelewane vizuri sana hapa! Narudia tena, Uislamu siyo kile wafanyacho Waislamu bali ni kile ambacho Waislamu wanapaswa kufanya kwa mujibu wa muongozo wa Qur’an na Sunna! Hivyo basi, Muislamu akiua mtu iwe ni kwa kukusudia au bila kukusudia; inakuwa ni Muislamu tena ni mtu binafsi ameua pengine mwenye jina maarufu la Kiislamu lakini siyo Waislamu wote wameua wala siyo Uislamu umeua!

Wakati fulani, baadhi ya makanisa katika baadhi ya nchi duniani yalikumbwa na kashfa ya ulawiti wa watoto wadogo! Maaskofu walituhumiwa kulawiti watoto! Kwa kutumia lugha hii hii, Papa alisema Ukristo siyo kile wanachofanya Wakristo bali wanachopaswa kufanya! Siyo sahihi ikitokea mtu mmoja Mkristo kumlawiti mtoto, isemwe kuwa Wakristo wote wanalawiti watoto au Ukristo unalawiti watoto!

Hii ninayotumia ni lugha ya kuiita ‘chepeo chepeo’ na siyo kuiita kijiko kikubwa! Tukio la jijini Dar es Salaam linaweza kupelekea Waislamu Wasomali kunyooshewa vidole, ‘Hawa watu hawaaaa!’ Allah Aliyetukuka ameamrisha mambo yanayotia watu shaka waachiwe watu wenye mamlaka wachunguze!

Kuhusu umuhimu wa kuwaachia watu wenye mamlaka, hebu turejea kauli ya Mwenyezi Mungu katika Qur’an 4:83:

“Na linapowafikia jambo lolote lilio khusu amani au la kitisho wao hulitangaza. Na lau kuwa wangelipeleka kwa Mtume na kwa wenye mamlaka kati yao, wale wanaochunguza wangelilijua. Na lau kuwa si fadhila ya Mwenyezi Mungu juu yenu na rehema yake mngelimfuata Shet’ani ila wachache wenu tu.”

Kitendo cha mtu kurushiana risasi na Jeshi la Polisi ambalo ndilo linalolinda usalama wa raia na mali zao hadi akasababisha watu kupoteza maisha kinaweza kusababishwa na itikadi potofu ya mhalifu, mtindio wa ubongo kwa muhusika au sababu nyinginezo.

Wanaoweza kung’amua hayo ni vyombo vyetu vya ulinzi na usalama ambavyo tunaviamini sana. Waachiwe wapeleleze, na sisi tuache kusema tusiyoyafahamu!

Tunasoma ndani ya Qur’an kuwa kuna watu waliweka azma ya kutaka wamvamie mmoja wa Mitume wa Allah (Nabii Swaleh) ghafla usiku na kumuua pamoja na ahli zake kisha waseme kumwambia walii wa damu yake (mrithi wake) kuwa wao hawajashuhudia kuuliwa kwake na kuwa wao wanasema kweli. Kisa hiki kiko katika Surat An-Naml (Sura ya 27) aya ya 49.

Tukisoma ndani ya Qur’an Surat Yusuf (Sura ya 12) aya ya 17, tunakuta ndugu zake Yusuf walimjia baba yao usiku hali ya kuwa wanalia wanadai Nabii huyo wa Mwenyezi Mungu kaliwa na mbwa mwitu, kumbe walikuwa wamemsweka kisimani!

Kama kuna dini ambayo imekataza kwa kemeo kali kuua basi ni dini ya Kiislamu, kiasi kwamba mtu akiua mtu mmoja au akisababisha kifo cha mtu mmoja asiye na hatia, ni kama vile ameua watu wote! Hii imekuja katika Suratul Maidah (Sura ya 5) aya ya 32.

Hata hivyo, hapa hatuzungumzii watu wanaokabiliana na wauaji. Hao hawako katika hukumu hiyo! Hapa tunazungumzia mtu anayekusudia au anaamua kuua nafsi zisizo na hatia au makosa. Hukumu ya mtu wa aina hiyo haiishii tu kwa mamlaka kumsimamishia hukumu ya kifo hapa duniani, bali hata Siku ya Kiyama muuaji atakuwa mtu mwenye marejeo mabaya sana.

Siku hiyo ya hukumu, nafsi zisizokuwa na hatia na makosa ambazo mtu huyo aliziua zitamng’ang’ania ili aeleze mbele ya Mola Aliyetukuka aliyekataza kuua nafsi, kwa nini aliziua!?

Mwisho, nikuache msomaji wangu kwa kuwataka tutafakuri maneno haya: “Iogopeni sana siku ya kurejea kwa Allah, kisha kila kitu kitabainishwa!” Hiyo ni mahakama ambayo tunapoitafakari nyoyo zetu zinatikisika! Poleni sana wafiwa, Mungu ibariki Tanzania.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close