6. Kutoka Katika Quran na Sunnah

Tuzidishe Wema Siku 10 za Dhul-hijja

Tumo ndani ya siku 10 tukufu za mwezi wa Dhul-Hijja. Allah Mtukufu ameziapia siku hizi 10 ndani ya kitabu chake kitukufu cha Qur’an pale aliposema: “Naapa kwa alfajiri. Na kwa siku 10.” [Qur’an, 89:1-2].

Wanazuoni wengi wa tafsiri ya Qur’an wamesema kilichoapiwa katika aya hii ni siku 10 za mwanzo wa Dhul-Hijja, yaani Mfungo tatu, na mtazamo huu pia wameusema Ibn Jariri Twabariy na mwenzake Ibn Kathir (Allah awarehemu Wote).

Siku 10 hizi zinajumuisha ndani yake fadhila na baraka mbalimbali. Kutenda amali njema katika siku hizi ni bora kuliko amali njema katika siku nyingine za mwaka, kama alivyotuambia Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie): “Hakuna siku amali inakuwa bora zaidi kushinda siku hizi 10 za Dhul-Hijja (Mfungu0 tatu).”

Maswahaba wakasema: “Hata amali ya Jihad?” Mtume (S.A.W) akasema: “Hata Jihad, ila mtu aliyetoka Jihad akaiweka rehani nafsi yake na mali yake, na kurejea bila ya chochote.” [Bukhari].

Wanazuoni wameitaja hadithi hii kama ushahidi juu ya ubora wa funga ya siku 10 za Dhul- Hijja, isipokuwa haitakikani kufunga siku ya Iddi, kwani kufunga siku hiyo ni haramu.

Sanjari na kufunga, pia ni sharia katika siku 10 hizi kuleta takbira, kwa ushahidi wa hadithi katika Sahihi Bukhari: “Ibn Umar na Abuu Huraira (Allah awaridhie wote wawili) walikuwa wakitoka kuelekea sokoni huku wakileta takbira katika siku 10 za mwanzo wa Dhul- Hijja; watu nao huleta takbira kwa kuwafuatishia wawili hao.”

Kuna ubora, fadhila na baraka nyingi na za kipekee za siku ya tisa katika siku hizi 10, yaani siku ya Arafa. Katika siku hii, mahujaji wote, husimama katika viwanja vya Arafa ambayo ni nguzo tukufu miongoni mwa nguzo za Hijja.

Miongoni mwa fadhila za siku ya Arafa ni kwamba Allah Ta’ala hufuta dhambi za muda wa miaka miwili kwa mtu aliyefunga siku hiyo. Sunna ya kufunga siku hii ni kwa watu wasiokuwepo katika kisimamo cha Arafa. Kwa walio katika kisimamo cha Arafa, muongozo wa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ni kutokufunga siku hii.

Imepokewa Hadithi kutoka kwa Bi. Aisha (Allah amridhie) akimnukuu Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) kuwa amesema: “Hakuna siku ambayo Allah huwaacha huru watu wengi na moto kuliko siku ya Arafa. Hakika yeye hukurubia hadi mbingu ya dunia, kisha hujifaharisha kwa Malaika kwa kusema, ‘ni jambo gani wanataka watu hawa? [Muslim].

Hivyo, tunawahimiza waislamu watumie muda wao katika siku 10 hizi kufanya yaliyo mema kadiri wawezavyo ikiwa ni pamoja na kusoma Qur’an, kumdhukuru Allah, kutoa sadaka, kuwafanyia wema wazazi wawili na kuunga undugu. Sanjari na hivyo, pia ni juu ya kila muislamu kuamrisha mema na kukataza mabaya na yasiyokua hayo katika njia za kheri.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close