6. Kutoka Katika Quran na Sunnah

Tumuadhimishe Mtume kwa kufanya mageuzi ya kida’awa

Uislamu unamtaka kila Muislamu aitakidi (aizingatie) kuwa, Hakuna Mola apasaye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu na Muhammad ni Mjumbe wake (Mwenyezi Mungu).

Hii ndiyo Shahada, ya kwanza miongoni mwa nguzo tano za Uislamu. Ni rahisi kuitamka Shahada, lakini kuitekeleza, ambao ndiyo ukamilifu wa Uislamu, ni shida kwa watu wengi.

Kwa kulijua hilo, Allah ‘Azza Wajallah’ alimtuma Nabii Muhammad kuja ulimwenguni ili awahubuirie watu ibada ya Muabudiwa Mmoja. Allah Aliyetukuka alimwambia Nabii Muhammad: “Na hatukukutuma
(hatukukuleta ewe Muhammad) ila uwe rehema kwa walimwengu.”
[Qur’ an, 21:107].

Ni kwa mukatdha huo, Waislamu wana mengi ya kujifunza katika mwezi
huu wa Mfunguo Sita (Rabiul Awwal) ambao kihistoria unadhaniwa
kuwa ndiyo alizaliwa Mtume (rehema za Allah na amani ya zimshukie).

Katika mwezi huu, baadhi ya Waislamu hukusanyika kwenye maeneo mbalimbali kwa kutukuza mazazi ya Mtume wakifanya jitihada kuwahamasisha wafanyabiashara na watu wengine kuchangia
pesa, na mahitaji mengineyo ili kusaidia hafla za Maulid.

Hata hivyo, ifahamike kuwa, kumpenda Mtume siyo kumkumbuka kwa kumsifu mara moja kwa mwaka, bali kutekeleza yote aliyotuamrisha ikiwa ni pamoja na kujitolea katika kulingania dini ya Allah.

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ametuambia: “Fikisheni kutoka kwangu japo Aya (moja), na hadithieni habari za Bani Israil wala hakuna kosa.” [Bukhari]. Kwa kuzingatia Hadithi hii, Muislamu anapaswa kujitathmini kwa kiwango gani anawalingania ndugu zake Waislamu na wasio Waislamu kuielekea njia ya Allah.

Kumsifu Mtume kwa kusoma na kughani mashairi bila ya kufanya bidii ya kumfuata kivitendo ili kujikurubisha kwa Allah Ta’ala ni jambo lisilo na tija. Allah Ta’ala anatuonya na hilo kwa kusema: “Enyi mlio amini! Kwa nini mnasema msiyoyatenda.” [Qur’an, 61:2].

Na katika Hadithul Qudsy Allah anasema: “Yeyote anayemdhalilisha kipenzi changu (walii) basi ajue nimemtangazia vita. Mwanadamu hutaweza kuyafikia yaliyoko kwangu ila kwa kutekeleza yale niliyokufaradhishia juu yako, wala hatajikurubisha kwangu kwa Sunna ila nitampenda…” [Bukhari].

Aya na Hadithi vinasisitiza umuhimu wa kuyatekeleza tuliyofaradhishiwa na Allah na yale aliyokuja nayo Mtume Muhammad ili tupendwe na Allah Ta’ala. Hivyo, na sisi hatuna budi kufanya da’awa kama alivyoelekeza Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie), na hapo tutakuwa tunamfuata Mtume kisawasawa.

Hata hivyo, lazima tukubali kuwa, kumtii Mtume ni jambo la wajibu, na ni sehemu ya kuchuma thawabu ili zitusaidie katika maisha yetu ya Akhera ambayo ni ya uhakika na ya kudumu. Kulingania dini ni msingi ambao Waumini wanapaswa kuuendeleza kwa masilahi ya dini na watu wake. Ni vema maadhimisho ya kumbukizi ya kuzaliwa Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) ya kila mwaka yakatumika
kama njia ya kuwahimiza watu wafanye da’awa hasa katika maeneo ya mijini na vijijini ili kuwasaidia watu wengine wautambue Uislamu na waione nuru ya Allah

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close