6. Kutoka Katika Quran na Sunnah

Toba ya mtu aliyeua watu mia moja

Baada ya kusoma simulizi iliyopita ambayo iliihusisha ndoto ya Mtume katika ziara yake ughaibuni akiwa na Malaika (swahiba wake) wawili na kufanya udondozi wa kina juu mafunzo yanayopatikana humo, bustani wiki hii tena inatukutanisha na simulizi nyengine ya kusisimua, nayo bila shaka ina mafunzo na mazingatio makubwa kabisa. Hiki ni kisa cha mtu aliyeua nafsi mia moja kisha akatubu.

Abu Said al-Khudri (Allah amridhie) amesimulia kwa kusema kwamba, Mtume wa Allah amesema: “Alikuwepo mtu katika watu waliopita kabla yenu aliua watu tisini na tisa (99) (akajuta na kutaka kutubu). Akaulizia mtu mwenye elimu zaidi, akaelekezwa kwa mtawa mmoja (aliyesifikana kwa wingi wa ibada). Akamwendea na kumueleza kwamba yeye ameua watu 99, je toba yake inakubalika? Yule mwanachuoni akasema, ‘Hapana.’Akamuua na kukamilisha mia.

“Kisha akaulizia tena mtu mjuzi kuliko wote (katika zama zile). Akaelekezwa kwa mwanachuoni fulani. Basi, akaenda na kumwambia kwamba ameua watu mia, basi je toba yake inakubalika? Yule mwanachuoni akamwambia, ‘Ndio na hakuna kizuizi chochote cha kuzui toba yako. Lakini sasa ondoka kwenye mji wako huo, nenda katika mji fulani kwani huko kuna watu wema wanamuabudu Allah. Abudu pamoja nao wala usirudi tena katika mji wako kwani mji wako ni mbaya sana.’

“Yule mtu akaondoka. Alipofika katikati ya safari akafikiwa na umauti. Malaika wa rehema na wa adhabu wakagombaniana (katika kuichukua roho yake). Malaika wa rehema wakasema, ‘Amekuja kwa moyo wake akiwa ameshatubia kwa Mola wake (kwa hiyo anastahiki kuwa katika waja wema). Malaika wa adhabu nao wakasema, ‘Ndio, lakini hajapatapo kufanya jema lolote (kwa hiyo roho yake haina haki ya kuwekwa katika kundi la watu wema)’

Mara akawatokea Malaika (mwenzao) kwa sura ya binadamu wakamfanya hakimu wao. Akasema, ‘Pimeni kati ya miji miwili (alikotoka na anakokwenda). Ulio karibu, ndio atakuwa wa mji huo. Wakapima, wakamkuta yuko karibu na mji anaokwenda, hapo Malaika wa rehema wakaichukua roho yake.” [Bukhari na Muslim].

Na katika mapokezi mengine:

“Allah aliuamrisha ule mji aliotoka akauambia: “jitenge” na ule mji anakokwenda: “jisogeze.” Yule mtu akawaambia: “Haya pimeni.” Wakamkuta yuko karibu na mji anaoufuata kwa shubiri moja tu, akasamehewa.

Mafunzo

Simulizi hii imebeba mafunzo mengi likiwemo ukubwa wa msamaha wa Allah kwa waja wake walioyafuja maisha yao kwa wingi wa madhambi. Katika Qur’an, Allah Aliyetukuka anasema:

“Sema, enyi waja wangu ambao mmezifuja nafsi zenu (kwa madhambi) msikate tamaa na rehema za Mwnyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu anasamehe madhambi yote, hakika yeye ni msamehevu mrehemevu.”

Kadhalika tumejifunza kutokana na hadith quds kwamba, lau dhambi za mja zingelilijaza anga la mbingu, kisha akatubu na kujuta, Allah atamsamehe, madhali dhambi si za ushirikina.

Madhara ya kuabudu bila ya elimu

Siku zote inasisitizwa kufanya ibada kwa elimu ya kutosha. Pia, inahimizwa Waislamu waache tabia ya kuiga na kufuata mkumbo tu. Tazama mtu wa kwanza aliyefuatwa na yule jamaa. Licha ya ibada nyingi alizokuwa akizifanya, hakuwa na maarifa ya kutosha juu ya Uislamu.

Mtu yule hata hakujua kwamba, mlango wa toba ni mkubwa zaidi kuliko madhambi wanayoyafanya binadamu na kwamba, Allah Aliyetukuka hupokea toba zao saa yoyote.

Tunajifunza hilo, sambamba na kujua hatari ya kujibu maswali bila ya elimu. Madhara yake ni kupotoka, kuupotosha umma na hata kuhatarishia maisha ya mhusika, kama tulivyoona katika hadith hii.

Miji mibaya ni hatari kwa dini ya mtu

Katika dunia hii, miji ama vijiji vinatofautiana. Kuna baadhi ya maeneo yana wakaazi hatari wenye kuendeleza vitendo vya uharamia na ufisadi, na wasiojua wema. Na maeneo mengine, hupata umashuhuri kwa kuwa na wakazi wengi wa kheri na wachamungu. Inaonekana wazi kwamba jamaa alikuwa anaishi katika mji hatari uliojaa maovu na dhuluma, kiasi cha kukosa hata mtu au watu wa kumkanya, na hatimaye akaua watu hadi kufikia tisini na tisa (99).

Basi Muislamu akijikuta katika mji muovu na akawa hana uwezo wa kugeuza uovu ule, anapaswa kuhama kabla ya kuathiriwa na yeye akawa kama wao. Waswahili wanasema “Mwanadamu ni mtoto wa mazingira” yaani huleleka kwa mujibu wa mazingira na watu anaoishi nao.

Katika simulizi hii, kuna ushahidi wa uwepo wa viumbe Malaika ambao huwafikia wanadamu wakati wa kukata roho. Jukumu kubwa la Malaika hao ni kuzitoa roho kwa idhini ya Mola wao, kuzichukua na kuzifikisha mahala zinapostahiki.

Waja wema, walioishi kwa mujibu wa maagizo ya Mola wao kupitia mitume wake, roho zao hutolewa na hubebwa kwa upole na heshima kubwa na Malaika wa rehema. Lakini roho za waovu walioishi kwa kuzipinga amri zake hutolewa kwa nguvu, hasira na masimango. Kazi hii hufanywa na Malaika wa adhabu. Tunajifunza hayo katika hadith hii na katika nususi nyingi za Qur’an na Sunna. Tunamuomba Allah atusamehe madhambi yetu yote na atupe radhi zake, amiin.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close