6. Kutoka Katika Quran na Sunnah

Shikamana na tabia njema, ni uzuri usiokwisha

Hakika tabia njema ni katika amali nzito atakayoikuta Muislamu katika mizani ya matendo yake Siku ya Kiyama. Kimantiki, sifa ya tabia njema kwa mwanadamu, ni kama vazi. Wakati mwingine, tabia njema, hata huchukuliwa kuwa ndiyo ndio kipimo cha utu na ustaarabu.

Mwenyezi Mungu anasema: “Enyi wanadamu tumeteremsha kwenu mavazi na mapambo na vazi la uchaMungu hilo ndiyo bora zaidi.” (Qur’an, 7:26).

Kwa kulitambua hilo, Mwenyezi Mungu amewatuma Mitume na Manabii ulimwenguni ili waje kufundisha jamii zao adabu na tabia njema. Umma wa Kiislamu umebahatika kulelewa katika misingi ya viwili hivyo. Allah Ta’ala anatuambia:

Hakika nyinyi mnacho kiigizo chema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwa anayetaraji kukutana na Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho…” (Qur’an, 33:21).

Pia, katika hadithi, Mtume (rehema za Allah na amani zimfikie) amesema: “Nimetumwa kukamilisha tabia njema.” (Ahmad).

Tunapotafakari kwa kina juu ya mafundisho haya ya Qur’an na Sunna, tunagundua kuwa hakuna pambo nadhifu kwa Muislamu zaidi ya tabia njema. Maana pana zaidi ya tabia njema ambayo kila Muislamu anatakiwa kuwa nayo ni kuepuka kufanya mambo maovu na ya upuuzi ambayo hayamletei faida katika Dini, Dunia na Akhera yake.

Ijulikane kuwa, kinachoupa nguvu na kuupandisha daraja Uislamu kutoka kuwa nadharia hadi utekelezaji, ni kuwapo kwa tabia njema na mifano elekevu kutoka kwa waja wema waliotangulia. Hata hivyo, limekuwa ni jambo la kawaida kwa Waislamu wengi wa zama hizi kujihusisha na mambo ya upuuzi badala ya kujipamba
na tabia njema za Kiislamu.

Jambo kubwa linalopelekea kudumu na mwenendo huu ni Waislamu kutoifahamu dini yao hali inayowafanya wakhalifu amri za Allah Ta’ala sambamba na Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie). Binadamu wanasahau kuwa maisha yao yapo kwenye himaya ya Muungu Muumba na kwamba muda mfupi waliopewa kuishi hapa ulimwenguni ndio utakaoamua makazi yao ya milele huko Akhera.

Vipi tutaweza kuwa na tabia njema
Tutakuwa na tabia njema kwa kufanya mambo kadhaa. Mosi, ni kutambua utukufu wa Mwenyezi Mungu kwa kusoma Qur’an na kuifahamu vema maana yake sanjari na kusoma Sunna ya Mtume (rehema za Allah na amani zimfikie) kwani hakuna namna nyingine ambayo Allah Ta’ala anaweza kutusemesha ila kwa kusoma Qur’an. Hii ni dalili kwamba tunapoisoma Qur’an na kufahamu mafunzo yake tutatii kwa ukamilifu sharia
za Mwenyezi Mungu na kuepuka makatazo yake hivyo uhusiano baina yetu na yeye utazidi na kuwa imara.

Pili, tutasimamisha tabia njema kwa kuepuka marafiki waovu. Hii ni kwa sababu katika watu pia kuna mashetani wanaotuhimiza kufanya maovu. Kilicho muhimu kwetu ni kuchagua marafiki wazuri watakaotuongoza au kutukumbusha njia sahihi ya kupita pindi tunapokwenda kinyume na maadili ya
dini.

Katika Hadithi iliyopokelewa na Abu Dardaa ( Allah amridhie), Mtume (rehema za Allah na amani zimsh u k i e ) amesema:
Hakuna kitu kizito katika mizani ya Muumini Siku ya Kiyama kuliko tabia njema. Hakika Mwenyezi Mungu humchukia mtu muovu mwenye tabia mbaya.” (Tirmidhi).

Akasema tena Mjumbe wa Allah: “Moja ya sifa nzuri za Muislamu ni kutoshughulika na yale yasiyomuhusu.” (Tirmidhiy). Hizi ni baadhi ya Hadithi zinazotilia mkazo adabu, tabia njema na heshima katika Uislamu. Katika kuyafanikisha yote haya kila Muislamu anapaswa kumuomba Allah Ta’ala amthibitishe katika Uislamu na kuhakikisha haupotezi moyo wake baada ya kuuongoa sambamba na kuzingatia umuhimu wa kukumbuka mara kwa mara tukio la umauti. Mola wetu Mtukufu ameahidi kutulipa pepo yenye uzuri usiokwisha, lakini ili tuipate pepo hiyo hatuna budi kuingiza tabia njema ndani ya maisha yetu ya kila siku.

Abuu Huraira (Allah amridhie) alimsikia Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) akiulizwa: “Ni kitu gani kitakachowaingiza watu kwa wingi peponi?” Akasema: “Kumcha Allah na tabia njema.” Na akaulizwa tena ni kitu gani kitakachowaingiza watu wengi kwa wingi motoni? Akasema: “Kinywa (mdomo) na utupu,” (Tirmidhi).

Je, unatatizika kupata mifano ya watu wenye tabia njema? Kama jawabu ni ndiyo, basi isome na uielewe Qur’an, Sunna ya Mtume sambamba na vitabu vya kihistoria yaani Tarekh. Ukifanya hivyo,
utaweza kuchota mifano ya tabia njema kutoka kwa Manabii na wengineo katika waja wema waliopita (Salafi).

Kwa hakika hawa ni walimu sahihi wa masomo ya imani, tabia njema na maisha. Hivyo, ukiwasoma barabara wataweza kukuokoa kutoka kwenye dimbwi la maisha ya kijahili, upotevu na dhulma. Na kwa sababu tabia njema ni jambo muhimu lenye thamani kubwa kuliko dhahabu, daima Muislamu anapaswa kuonesha tabia njema katika kila nyanja ya maisha yake.

Tunamuomba Mwenyezi Mungu atujaalie kuwa miongoni mwa wanaoutekeleza Uislamu kivitendo kwa ukamilifu wake. Aamiin

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close