6. Kutoka Katika Quran na Sunnah

Sheikh Kilemile: Suluhisho ni kufuata Qur’an na Sunna

Kufuata mafundisho sahihi yaliyoelekezwa katika Qur’an na Sunna ndio njia pekee ya kuondokana na kukithiri kwa michezo ya aibu, ikiwemo ile inayofanywa na wapiga dufu katika jiji la Dar es Salaam.

Hayo yameelezwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania (Hay-at), Sheikh Suleiman Amran Kilemile alipoulizwa maoni yake kuhusiana na makemeo yaliyotolewa na viongozi wa Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA) kuhusiana na michezo ya aibu ya ngoma za dufu iitwayo mziki moto.

Sheikh Kilemile alisema, dufu ni ngoma za wanawake wa Kiarabu. Kwa sababu hiyo, Sheikh alisema, suala hilo halipaswi kuwachukulia Waislamu muda mwingi kulijadili. Sheikh Kilemile alisema, ni vema Waislamu wakatumia muda wao kufanya vitu vya msingi ikiwemo kufundisha Uislamu sahihi utakaoleta tija kwa watu wengi, kwa mujibu wa Kitabu cha Mwenyezi Mungu (Qur’an) na Sunna sahihi za Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie).

“Sisi tumechukua utamaduni wa watu na kuuingiza katika dini! Dufu ni miongoni mwa taarabu zinazopigwa na wanawake wa Kiarabu. Dufu aliwahi kupigiwa Mtume na wanawake hao baada ya kurudi kwake Madina salama alipotoka vitani, liweje lifanywe kuwa ni jambo la dini?” alihoji Sheikh Kilemile akionesha kushangazwa.

Lakini kwa mujibu wa Sheikh Kilemile, huko Uarabuni dufu zinapigwa na wanawake wakiwa majumbani mwao na sio wanamume.

“Tuna mambo mengi ya kufanya katika kuutangaza Uislamu ikiwemo kufundisha mafundisho sahihi. Ni bora tuwekeze nguvu huko kuliko kujadili taarabu za Uarabuni,” alisema Sheikh Kilemile.

Hivi karibuni, Sheikh wa mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Musa Salum alitoa kauli ya kukemea upigaji wa dufu kwa mtindo wa muziki moto, kauli ambayo ilitiliwa mkazo baadaye na Mufti Abubakar Zubeir katika tamko jingine ambapo alisema amezuia na kupiga marufuku kote Tanzania upigaji dufu na qasida zinazojulikana kama mziki moto ambazo zinaaibisha na kuchafua maadili mazuri ya Uislamu.

Sheikh Barahiyan

Msimamo kama huo wa Sheikh Kilemile pia ulitolewa na Sheikh Salim Barahiyan wa Tanga ambaye aliwataka Masheikh wasiishie kuzuia kucheza na kupiga dufu kwa mtindo wa muziki moto tu, bali wakemee hata tendo la wanaume kusherehekea kwa njia ya kupiga madufu.

Sheikh Barahiyan alisema, kazi ya kupiga madufu kwenye sherehe ilifanywa na wanawake katika sherehe maalum kama vile harusi au sikukuu za Idd; na sio wanaume. Sheikh Barahiyan alisema, hata aina ya upigaji pia haikuwa kama ilivyo sasa, na kwamba wanawake hao walikuwa hawapigi na kucheza kwa kushikana viuno au kucheza pamoja na wanaume.

Hata hivyo, Sheikh Barahiyan pia alisema amepokea kauli za viongozi wa BAKWATA kwa mikono miwili kwani viongozi hao wanatekeleza wajibu wao wa kukemea maovu.

Alisema, yeye alisikia wito huo kupitia mitandao ya kijamii, na kwamba anafikiria matamko hayo yamechelewa kutolewa na BAKWATA, ingawa Waislamu hawana budi kuunga mkono juhudi hizo ili kupunguza maasi.

Sheikh Barahiyan alisema, kama jamii haikemei maovu, Mwenyezi Mungu huwapa adhabu kwa kuwaletea dhiki ya kimaisha, njaa, majanga na magonjwa.

“Tunaweza kulalamikia serikali iliyopo madarakani kuhusu hali mbaya ya kimaisha kumbe sababu ni raia wenyewe kukithirisha maovu,” alionya Sheikh Barahiyan.

Sheikh Barahiyan alitaka juhudi hizo za kukemea maovu ziendelee katika maovu mengine. Kwa mujibu wa Sheikh Barahiyan, uchezaji madufu umekuwa kero ya muda mrefu na kufafanua kwamba,

Masheikh wa Sunna wamekuwa wakijitahidi kukemea hali hiyo kwa miaka mingi sasa. “Tunawaunga mkono. Kwa historia, sisi tunaifanya kazi hiyo kwa miaka mingi lakini wenzetu wengine walikaa kimya na kuonekana kuyaunga mkono. Ni vizuri wakajiepusha na vitendo hivyo ili jamii ya Kiislamu ione kuwa havifai,” aliongeza.

Viongozi wasijihusishe na waovu Katika hatua nyingine, Sheikh Barahiyan amewataka viongozi wa dini, hususan Masheikh kuacha tabia ya kujihusisha na waovu, wakiwemo wasanii ambao wamekuwa wakiudhalilisha Uislamu.

Katika moja ya mambo ambayo amewarai Masheikh waache kushiriki katika sherehe za wasanii hao. “Kuna wasanii humu Tanzania wanafanya maovu halafu bahati mbaya hao Masheikh ndio wamekuwa mstari wa mbele kuwaunga mkono kwa kuhudhuria sherehe zao.”

Sheikh Barahiyan aliwataka Masheikh hao waache tabia hiyo kwa sababu Waislamu wanaowatazama wanadhani kuwa jambo linalofanyika linafaa kumbe halifai kwa mujibu wa mafundisho ya dini.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close