6. Kutoka Katika Quran na Sunnah

Sayansi Mamboleo Na Mafunzo Mbalimbali Ambatanishi

SHEMU YA 8; Mpenzi msomaji, katika Hadithi ya Abuu Said al-Khud’riy, Mtume wa Allah siku moja aliambiwa na mtu mmoja kuhusiana na ndugu yake aliyekuwa amepata ugonjwa wa tumbo. 
Na hata ladha za asali pia hutofautiana kutokana na aina ya maua iliyotumika. Jambo jingine la ajabu ni ule ukweli kuwa nyuki humeza ile malighafi waliyoichukua kutoka katika maua na kisha huitema/ kuicheua kutoka katika matumbo yao wanapotengeneza asali.

Mtume alimuelekeza mtu yule amwambie ndugu yake, mgonjwa wa tumbo, anywe asali. Halafu mtu huyo akaja mara ya pili na ya tatu, akisema kuwa tumbo bado linamsumbua tena limezidi naye Mtume akawa akitoa jibu hilo hilo la kuwa anywe asali. Mara ya nne, Mtume akasema: “Allah kasema kweli (yaani asali dawa), lakini tumbo la ndugu yako linadanganya. Mwambie anywe tena asali.” Ndugu huyo akamwambia tena nduguye anywe asali, na hapo ndipo alipopona ugonjwa wake! (Bukhari). Mpenzi msomaji, Elimu na Sayansi ya Tiba inathibitisha ukweli wa Qur’an juu ya asali kuwa dawa pale Allah aliposema: “Ndani yake mna ponyo au shifaa kwa watu”. Elimu ya tiba imethibitisha pasina shaka yoyote kuwa asali ni tiba, tena ni tiba ya maradhi mengi. Katika kusadikisha na kuakisi ukweli wa Qur’an kuhusiana na asali kuwa ni dawa, Swahaba Abdallah Ibn Abbas amesimulia kuwa Mtume wa Allah amesema: “Ponyo lipo katika vitu vitatu;… miongoni mwa vitu hivyo Mtume akataja kinywaji kilichotengenezwa kwa asali..” Mpenzi msomaji, kabla hatujaliendea suala hili la asali kuwa dawa isiyo na shaka na kulieleza kwa kina, Allah kaeleza kuwa asali ina rangi tofauti, na ifahamike kuwa aina ya maua anayopitia nyuki ambayo ndiyo hutengeneza asali, ina athari katika kuipa asali rangi. Kwa hiyo, hili nalo ni jambo la ajabu hasa hasa kwa watu ambao wamewahi kuona asali ya rangi moja tu, wafahamu kuwa asali ina rangi mbalimbali kutokana na rangi za maua yaliyotembelewa na nyuki katika kukusanya malighafi ya kuitengenezea. Na hata ladha za asali pia hutofautiana kutokana na aina ya maua iliyotumika. Jambo jingine la ajabu ni ule ukweli kuwa nyuki humeza ile malighafi waliyoichukua kutoka katika maua na kisha huitema/kuicheua kutoka katika matumbo yao wanapotengeneza asali. Hili limeelezwa na Allah katika Qur’an: “Kinatoka katika matumbo yake (nyuki) kinywaji (yaani asali) chenye rangi tofauti ndani yake kuna shifaa ya maradhi ya watu”. Mpenzi msomaji, kinywaji bora kabisa cha mwanadamu (asali) kinatoka katika tumbo la mdudu (nyuki) na hata vazi zuri la mwanadamu ambalo ni hariri linatoka katika tumbo la mdudu (nondo). Daktari Muhammad Albanbii ambaye ni Profesa wa Elimu ya Nyuki katika Kitivo cha Kilimo katika Chuo Kikuu cha Aynu Ashamsi kilichopo nchini Misri katika kitabu chake, ‘Nyuki wa Asali katika Qur-an na Tiba’ amewahi kuielezea aya hii yaani: “Kinatoka katika matumbo yao (nyuki) kinywaji cha rangi mbali mbali ndani yake mna shifaa (ya magonjwa) kwa watu. Hakika katika hayo, bila shaka ni aya (ishara, dalili, zingatio) kwa watu wanaotafakari” (Qur’an, 16:69). Daktari Albanbii alisema: “Utaratibu wa maneno yaliyomo ndani ya aya hii na ilipofikia elimu ya sayansi mamboleo sasa, haimaanishi kuwa maksudio yake ni asali tu bali kinachokusudiwa ni kila kinachotoka katika mwili wa nyuki kama vile; asali, nta, sumu, royal jelly nk na imethibiti kuwa kila kimoja katika hivi kina faida ya kitiba kwa maradhi mbalimbali ya binadamu. “Kasisi/Mhubiri mmoja wa Kimarekani mnamo mwaka 1851 alibaini ukweli huo. Kwa hakika alichokifanya ni kuthibitisha Qur’an ilichosema zaidi ya miaka 1400 iliyopita!” Mpenzi msomaji, asali ni dawa ya kunywa na hata kupaka. Katika asili yake, asali inaweza kutibu maradhi mengi kwa mara moja na huu hakika ni muujiza kwani wakati dawa mbalimbali anazotengeneza mwanadamu zinatibu ugonjwa mmoja mmoja tu na hata kuacha madhara ‘side effects’ baada ya tiba, asali inaweza kunywewa na kutibu magonjwa zaidi ya 40 kwa mara moja! Jiulize ni dawa gani aliyotengeneza mwanadamu inayoweza kutibu magonjwa mengi kama hivi kwa wakati mmoja?! Hapa tunazungumzia asali halisi na asilia ambayo haijachakachuliwa. Kwa bahati mbaya sana asali nyingi siku hizi siyo asali halisi na asilia bali ni asali zilizochakachuliwa kwa hiyo zinaweza zisiwe na ubora stahiki kitiba kama asali asilia na halisi! Tulikuwa tunasikia asali kutoka Tabora, na Singida kuwa ni asali nzuri, lakini ukweli ni kwamba sasa hivi hali siyo hiyo. Asali imekuwa ikichakachuliwa sana siku hizi. Inachemshwa na hata kuchanganywa na vitu vingine ikiwemo sukari guru. Tena kunafanyika udanganyifu mkubwa sana siku hizi kwa kuwahadaa na kuwazuga watu pale wanapomuua nyuki mmoja au wawili na kuwaweka juu ya chupa ya asali ili watu waone na kudhani kuwa asali hiyo ni halisi kumbe hakuna chochote. Wauzaji wa asali, mcheni sana Allah. Msiharibu uasili wa asali kwa kutia mazagazaga humo, jambo linaloweza kupelekea kuifanya asali kuwa na madhara badala ya kuwa ponyo. Hata mabadiliko ya tabia nchi yanaweza kuchangia kupatikana kwa asali isiyo na ubora pale maua yanapokuwa yamechafuliwa na sumu zinazozalikana katika viwanda nk. Asali asilia ni dawa ya magonjwa mengi. Mimi na wewe tutafahamishana juu ya baadhi ya magonjwa yanayotibiwa kwa asali katika makala ijayo.. Itaendelea…

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close