6. Kutoka Katika Quran na Sunnah

Sayansi Mamboleo na Mafunzo Mbalimbali Ambatanishi

SEHEMU YA 9 Mpenzi msomaji, Allah aliyetukuka anasema ndani ya Kitabu Kitukufu, Al Qur’anul Majiidu: “Na Mola wako alimtia ilhamu nyuki kwamba, ‘Jitengenezee nyumba katika majabali, na katika miti, na katika wanavyojenga (wanadamu). Kisha kula katika kila matunda, na fuata njia za Mola wako zilizofanywa nyepesi (kuzipita)’. Kinatoka katika matumbo yao kinywaji cha rangi mbali mbali ndani yake mna shifaa (ya magonjwa) kwa watu. Hakika katika hayo, bila shaka ni aya (ishara, dalili, zingatio) kwa watu wanaotafakari,” (Quran, 16: 69).

Mpenzi msomaji, Allah kamtaja nyuki katika kitabu chake kitukufu. Vilivile ameiita sura kamili miongoni mwa sura 114 za Qur’an Tukufu kwa jina la ‘nyuki’ (Annahl). Suratul Nnahl kimpangilio wa sura za Qur’an ni sura ya 16. Kwa kuipa sura hii jina hili, Allah anataka tuzinduke na kumtafakari kiumbe huyu mdogo (nyuki) lakini afanyaye jambo kubwa na linaloonyesha uwezo na kudra ya Allah Muumba aliyetukuka. Aya tulizotangulia kuzitaja zinaonyesha nyanja mbalimbali za kisayansi katika maisha ya mdudu nyuki; kuna nyuki ambao huishi katika majabali na kujitengenezea nyumba zao humo, huku wengine wakijitengenezea nyumba zao katika sehemu zenye mashimo katika miti nk. Nyuki huziendea na hujenga katika sehemu hizi na nyingine kwa namna ya kimaumbile zaidi yaani hawana anayewafunza au kuwaelimisha kufanya hivyo. Bila shaka huu ni ufunuo kutoka kwa Allah (ilhamu) kwa viumbe hawa. Na hili ndilo Allah analobainisha katika kauli yake aliposema” “Na Mola wako alimtia ilhamu nyuki..”. Ilhamu maana yake ni kujuza kwa njia ya siri. Ujulisho huu huleta msisimko na msukumo wa kufanya jambo fulani kwa ufanisi usiomithilika na hili haliwezekani isipokuwa ni kwa muongozo wa Allah Muumba Aliye juu na Anayepasa kutukuzwa. Allah anasema: “Litukuze Jina la Mola wako Aliye juu kabisa (Ametukuka kabisa kuliko vyote). Ambaye ameumba (kila kitu) kisha akasawazisha. Na ambaye amekadiria na akaongoza,” (Qur’an, 87:1-3). Mpenzi msomaji, nyuki hutoka katika mzinga wake na kwenda kutafuta ungaunga, nta na majimaji yaliyopo katika maua umbali wa maelfu ya mita na kilomita kisha hurudi baada ya kitambo kifupi, pasina kukosea na kuingia katika mzinga ambao si wake, hata kama kutakuwa na mizinga elfu moja iliyoambatana kwa karibu na yenye kufanana! Hii inaonyesha namna Allah alivyowapa milango ya fahamu ya hali ya juu iwe ni macho au milango ya kunusia na kutofautisha harufu. Na hili ndilo Allah analozungumzia anaposema; “…..na fuata njia za Mola wako zilizofanywa nyepesi (kuzipita)….” Yaani pita katika njia ambazo kakuwepeshia Mola wako kwa kutumia milango ya fahamu ya kipekee aliyokupa Mola wako pamoja na ujuzi uliopewa. Mpenzi msomaji, Allah aliyetukuka kawapa nyuki milango ya fahamu yenye uwezo wa hali ya juu katika kuwasaidia kwenye safari ya kutafuta malighafi ya kutengenezea asali inayopatikana katika maua ya mbali na ya karibu. Nyuki wana uwezo mkubwa sana wa kunusa kwa kupitia ‘antenna’ (pua) mbili zilizopo mbele ya kichwa chake. Vile vile, Allah kawazadia macho yenye uwezo mkubwa sana wa kuona kiasi wanaona yale ambayo macho ya mwanadamu hayawezi kuona. Nyuki wanaweza kuona njia na rangi zinazoonyesha pahala maua yalipo ambavyo mwanadamu hawezi kuona isipokuwa kwa kutumia vifaa maalumu ya kutazamia. Nyuki wana macho ya aina mbili; aina ya kwanza ni macho ‘compound eyes’ ambayo yana uwezo mkubwa sana wa kuona. Nyuki huyatumia macho haya anapotoka kutafuta malighafi ya kutengenezea asali kwa kuonea mbali sana kutokana na namna yalivyoumbwa. Wanadamu hawana aina hii ya macho. Mwanadamu anapotaka kuona vitu vya mbali sana huweza kufanya hivyo kwa msaada wa kionea mbali (darubini). Nyuki wao, wamebarikiwa na macho yenye uwezo huu wa kidarubuni. Aina ya pili ya macho ya nyuki ni macho ya kawaida na idadi yake ni matatu. Macho haya yako juu ya kichwa cha nyuki. Nyuki huyatumia macho haya kwa kutizamia vitu vya karibu kama ndani ya mzinga kwani yana uwezo wa kutoa aina fulani ya mwanga. Vilevile, nyuki wana milango ya kuonjea ya hali ya juu. Kwa kutumia mlango huu wanapoingia katika ua, nyuki wanaweza kutambua kiwango cha sukari na kiwango cha maji kilichopo. Mambo haya mwanadamu hawezi kuyafanya isipokuwa kwa kutumia vifaa maalumu tena kwa kufanya utafiti wa kuchosha katika maabara. Ni nani aliyewafundisha nyuki haya? Huu ni uumbaji wa Allah. Basi nionyesheni nini walichokiumba wasiokuwa Yeye? Bali madhalimu wamo katika upotofu bayana. (Qur’an, 31: 11). Mpenzi msomaji Imamu Abuu Dawud amesimulia Hadithi Sahihi kwamba Swahaba wa Mtume, Ibn Abbas amesema kwamba Mtume wetu Muhammad alikataza kuua wadudu kadhaa akiwemonyuki. Zaidi juu ya hekima ndani ya agizo hilo la Mtume, endele kufuatilia mfululizo wa makala hizi za Qur’an na Hadithi za Mtume juu ya sayansi mamboleo na maf u n z o mbalimbali ambatanishi. Itaendelea…

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close