6. Kutoka Katika Quran na Sunnah

Sala ya Idd na hukumu za kuchinja (Udh-hiya)

Kutoka kwa swahaba Bara-a bin Azib, (Mwenyezi Mungu awe radhi naye), alihadithia kuwa Mtume (amani ya Mungu iwe juu yake), alipotoka kwenye siku ya Idd ya kuchinja, alianza na swala; kisha akatugeukia kwa uso wake, (na) akasema: “Ibada yetu ya kwanza katika siku hii tunaanza na kuswali, tukishamaliza swala tutakwenda kuchinja.”

Mtume (saw) akaendelea kusema: “Kwa mtu aliyeswali pamoja nasi na kufuata desturi yetu huyo ameipata sunna, na kwa aliyechinja udh-hiya wake kabla ya swala, huyo atakuwa amejipatia kitoweo cha nyama kwa familia yake, na hana alichokipata kwenye ibada ya kuchinja”. Na kwenye riwaya nyingine, Mtume amesema: “Mtu aliyeswali swala yetu na kuelekea qibla chetu asichinje mpaka amalize kuswali”.

Abu Burda bin Nayyar ambaye ni mjomba wa Bara-a akasema: “Ewe Mjumbe wa Allah, mimi nilijua kuwa leo ni siku ya kula na kunywa hivyo nilichinja kabla ya swala, na nilichokitaka ni kuwa, kondoo wangu awe ndiyo wa kwanza kuchinjwa nyumbani kwangu. Nilichinja kondoo wangu na kuilisha familia yangu na majirani zangu kabla ya kuja kuswali.” Mtume akamwambia: “Kondoo wako ni kondoo wa kitoweo.”

Abu Burda bin Nayyar akasema: “Ewe Mjumbe wa Allah, nyumbani tuna mbuzi mdogo (anayenyonya) ambae ni bora kuliko kondoo wa kitoweo (niliyemchinja), je, atanitosheleza?” Mtume akasema: “Naam, na kamwe hatotosheleza kwa mtu mwingine baada yako.” [Hadithi hii imepokewa na Imam Bukhari ndani ya Sahihi yake kwenye maeneo yasiyopungua 12].

Na amepokea hadithi nyingine yenye kisa kinachofanana na hicho kutoka kwa Anas (Allah amridhie), ambapo Mtume (rehema na amani ya Allah iwe juu yake) aliswali siku ya Idi ya kuchinja, kisha akahutubia, na kumuamuru kila mtu aliyechinja kabla ya swala akachinje tena (mnyama mwingine).

Bwana mmoja wa kabila la Answaar akasimama na kusema “Ewe Mjumbe wa Allah majirani zangu wahitaji (au alisema mafukara). Nami ndiyo nikachinja kabla ya swala. Nami nina kibuzi changu kidogo (ninachokipenda kuliko) huyo wa kitoweo niliyemchinja.” Mtume akamruhusu akachinje (licha ya kutokidhi sifa). Anas akasema: “Sikumbuki kama ruhusa hiyo ilimhusu yeye peke yake au iliwahusu wote.”

Hadithi hizi tatu zilizosimuliwa na Imamu Al-Bukhari kwa njia mbalimbali zinatuibulia masuala muhimu yafuatayo: Kwamba, katika Idi, swala hutangulia na mahubiri/hotuba ndiyo hufuata baadaye. Tofauti na swala ya Ijumaa, Ibada ya swala katika siku ya Idi ndiyo inayopewa kipaumbele cha kwanza. Mambo mengine yote yanayofanyika siku hiyo hutekelezwa katika mfumo wa kutekeleza sunna.

Swala ya Idi huswaliwa rakaa mbili na katika rakaa ya kwanza hutolewa takbira saba kabla ya kisomo. Na katika rakaa ya pili hutolewa takbira tano, pia kabla ya kisomo. Na Ibn Daqiq Al-id anaeleza: Swala zote zenye hotuba au mahubiri, huswaliwa kwanza, kisha ndiyo hufuatia hotuba, isipokuwa swala ya Ijumaa na siku ya Arafa.

Wakati wa swala ya Idi

Ibn Battwaal (Allah amrehemu) ameeleza katika (Fat-h): “Wanazuoni wameafikiana kuwa; haifai kuswali swala ya Idi kabla ya kuchomoza jua au pale linapochomoza, bali ni sunna kuswali katika wakati ulioruhusiwa”.

Na Imamu Baghawiy anaeleza katika kitabu cha ‘Sher-hus Sunna’: “Ni sunna kuelekea katika uwanja wa swala ya Idd mara baada ya swala ya Alfajiri na watu wawe katika maeneo yao na waanze kutoa takbira.”

“Na Imam anatakiwa aelekee kwenye eneo la swala ya Idi unapokaribia wakati
wa swala, ambapo kufika kwake kunakadiriwa wastani wa kupanda kwa jua kiasi cha
ukubwa wa mkuki (yaani kiasi cha kama dakika ishirini hivi). Ikumbukwe pia kuwa
ni sunna kutoka mapema kwenye Idul Adh-haa, na kuchelewa kidogo kwenye Idul fitr”.

Mfumo wa swala ya idi na aina ya washiriki katika uwanja wa swala ya idi

Na swala ya Idi huswaliwa kwa mfumo wa jamaa, na haina adhana wala Iqamah, na hakuna sharti la lazima iswaliwe msikitini, na watu wahimizwe kushikiriki katika mjumuiko wa swala ya Idd, na hata wanawake pia wanaruhusiwa kuhudhuria kwenye swala ya Idd, hata walio katika ada zao (hedhi na nifasi) isipokuwa hawatoswali isipokuwa watakaa chonjo ya eneo la kuswalia kwa lengo la kuitikia dua na kushuhudia heri.

Na watu wanatakiwa siku hiyo wapige takbira na zirindime kwenye maeneo yote, kuanzia nyumbani, barabarani, sokoni na waendelee hivyo mapaka wafikapo kwenye uwanja wa swala ya Idd, na washiriki katika kuleta takbira na waliowatangulia kwenye eneo la swala ya Idd.

Na imekuja kutoka kwenye hadithi ya Ummu Atwiyah (Allah amridhie): “Mtume alituamuru kwenye Idi tuwatoe majumbani vikongwe na wanawari, na akawaamuru wenye hedhi wakae kando ya eneo la kuswalia.” Ibn Daqiq Al-id (Allah amrehemu) amesema: “Lengo ni kuonesha mjumuiko mkubwa na kudhihirisha ibada”.

Sunna kabla ya kutoka

Na Mtume (rehema na amani ya Allah iwe juu yake) katika Idul-fitri alikuwa anakula kabla ya swala. Imesimuliwa na Imamu Bukhari kutoka kwenye hadithi ya Anas (Allah amridhie), kwamba Mtume hakuwa akienda kwenye eneo la kuswalia Idd mpaka kwanza ale kiasi cha tende, na alikuwa akizila kwa witri.

Ama kuhusu hadithi ya Buraida kwamba: “Mtume hakuwa akitoka kwenye Idul-Fitri mpaka kwanza ale, na kwenye Idul Adh-haa hakuwa akila mpaka amalize kuswali,” pamoja na kuwa hadithi hii imetumiwa sana na wanazuoni, sanad yake ina walakini kama alivyoeleza Ibn Hajar kwenye (Al-Fath).

Halafu Ibn Munir akasema: “Mtume (rehema na amani ya Allah iwe juu yake) alikuwa anakula katika Idi zote mbili katika wakati alioruhusiwa kula ili apate fursa ya kutoa sadaka ihusuyo siku hiyo. Sadaka ya Idul-Fitri hutolewa kabla ya kwenda kuswali, na sadaka ya Idul-Adh-haa hutolewa baada ya kuchinja, kana kwamba kuna utangamano na kutofautiana kwa aina fulani.”

Namna ya kuswali swala ya idi

Swala ya Idi ni swala ya rakaa mbili bila ya Adhana wala Iqama. Pia hakuna swala inayoswaliwa kabla (qabliya) au baada ( ba’adiya). Kwenye rakaa ya kwanza na baada ya takbira ya kuhirimia, utaleta takbira saba, na kwenye rakaa ya pili utaleta takbira tano na utainua mikono kwenye kila takbira.

Kisha Imamu atasoma ‘Suuratul Faatiha’ kwenye rakaa ya kwanza na ‘Qaaf wal- Qur-anil Majid.’ Kwenye rakaa ya pili, atasoma ‘Faatiha’ na kisha ‘Iqtarabatis Sa-ah…’. Au atasoma baada ya ‘Faatiha’ kwenye rakaa ya kwanza ‘Sabbihis ma rabbikal A’laa’, na kwenye rakaa ya pili ‘Hal ataaka hadiythul ghaashiya’. Na ni sunna kwenda kwenye swala ya Idd kwa kutumia njia tofauti wakati wa kwenda na kurudi.

Na hadithi inatuamuru kuchinja na kutuonesha hukumu na fadhila za kuchinja, ama kuhusu thawabu na fadhila za kuchinja, Imepokewa na Imam Tirmidhi na Ibn Majah kutoka kwa Bi. Aisha kuwa Mtume (rehema na amani ya Allah iwe juu yake), anasema: “Hajapata mwanadamu kufanya amali inayopendwa zaidi na Allah siku ya Idi kuliko kuchinja. Na hicho kilichochinjwa kitakuja siku ya kiyama na pembe zake, kwato zake na manyoya yake (yaani kamili kama kilivyokuwa duniani), na damu yake huanguka kwanza kwenye ridhaa ya Allah kabla haijamwagika ardhini. Basi chinjeni kwa hiari yenu”.

“Kamwe hamtafikia wema mpaka mtoe katika vile mnavyovipenda. Na kitu chochote mnachokitoa basi hakika Mwenyezi Mungu anakijua”.
(Qur’an, 3:92)

Hukumu ya udh-hiya

Wanazuoni wametofautiana sana kuhusu hukumu ya udh-hiya. Kuna wanaoona ni wajibu, na wapo wanaoona ni sunna. Kuhusu Dhabihu/Udh-hiya, Aqiqa, hidaya ni bora kuliko kutoa thamani ya mnyama. Na hii ni katika masurufu/sadaka zinazojulikana kisharia.

Yatima anaweza akachinjiwa kutoka katika mali yake. mke anaweza akachinja kutoka kwenye mali ya mumewe na kuwachinjia watu wa nyumbani kwake hata bila ya idhini ya mumewe. Na mdaiwa kama hasumbuliwi katika kulipa deni naye anaweza akachinja.

Al-a’yn alieleza katika kitabu cha ‘Al-Umda’ Said bin Musayyib na Ata ibn Abi Rabah Al- Qamah, Al-As-wad, Shafi’i na Abu Thaur, walisema kwamba: si wajibu lakini ni sunna. Atakayefanya atapata thawabu, na atakayeacha hapati dhambi.

Na ameyapokea hayo kutoka kwa Abubakr, Umar na Abi Masoud Al-Badriy na Bilal. Na Allaith na Rabi’ah wanasema: “Hatuoni sababu kwa mtu aliye na uwezo na anayemiliki udh-hiya kuacha kuchinja.” Na Malik anasema: “Asiache kuchinja, na akiacha atakuwa amefanya kitendo kiovu, isipokuwa kama ana udhuru.”

Baada ya kuyasema hayo ndiyo Al-a’yn katika kufanya majumuisho ya madhehebu ya Hanafi akasema yaliyosemwa na mwenye kitabu, ‘Al-hidaya’: “Kuchinja udh-hiya kwa ajili yake, familia yake na wanawe wadogo siku ya Idi, ni wajibu kwa kila Muislamu huru, aliye na uwezo na mkazi wa mji”.

Na ushahidi unaotumiwa na wale wanaoona kuwa ni sunna, ni hadithi ya Ummu Salama, kutoka kwa Mtume isemayo: “Mtu atakayeuona muandamo wa Dhul-Hijja, na akataka kuchinja, na aache kukata kucha na kunyoa nywele”. Na kuwepo suala la kutaka, ni ishara ya kwamba si wajibu.

Na ushahidi wa wanaosema kuchinja ni wajibu ni hadithi ya iliyopokewa na Ibn Majah kutoka kwa Abi Hureira kutoka kwa Mtume akisema: “Mtu aliye na uwezo na akaacha kuchinja, asikaribie, tena asikaribie eneo letu tunaloswalia”. Mithili ya onyo kama hili huwa haliji isipokuwa kwa kuacha jambo la wajibu.

Swala ya Idi ni swala ya rakaa mbili bila ya Adhana wala Iqama. Pia hakuna swala inayoswaliwa kabla (qabliya) au baada (ba’adiya).

Sheikhul Islam Ibn Taymiya amesema: “Kilicho dhahiri kuhusu suala la udh-hiya ni wajibu.” Halafu akasema: “Watu wanaopinga uwajibu wa udh-hiya hawana andiko.

Hoja yao ni neno la Mtume (rehema na amani ya Allah iwe juu yake), ‘Mtu anayetaka kuchinja’. Wao wanasema, ‘Wajibu hauambatani na hiyari’” “Na hili neno lipo kijumla mno. Halina tofauti na neno la Allah, ‘Enyi mlioamini! Mnaposimama kwa ajili ya Swala basi osheni nyuso zenu, na mikono yenu mpaka vifundoni, na mpake vichwa vyenu, na osheni miguu yenu mpaka vifundoni’. (Qur’an, 5:6), ambapo wanazuoni wameukadiria msemo huo kwa kusema, “Mnapotaka kuswali…”.

“Na ukisoma Qur’an, muombe Mwenyezi Mungu akulinde na Shetani maluuni (Qur’an 16:98). Na wamekadiria pia, ‘Mnapotaka kusoma Qur’an jikingeni kwa Allah’, wakati kuna twahara na kuwa na twahara ni wajibu. Neno lake, ‘Mtu anayetaka kuchinja,’ halina tofauti na ‘Anayetaka kuhiji aharakishe’.

Mtume (saw) aliruhusu aina ya wanyama wanaotakiwa katika udh-hiya, a’qiqah
na kafara ambao ni; kondoo, mbuzi, ng’ombe na ngamia.

“Ili upate hoja ya uwajibu wa kuchinja ni lazima ukadirie sharti, nalo ni kusema, kilichozidi kwenye mahitaji yake ya asili. Kama ilivyo kwenye sadaka/zaka ya fitri, na kuchinja/udh-hiya si wajibu kwa kila mtu bali ni kwa mwenye uwezo wa kufanya hivyo.

Kutoa dhabihu maksai

Imepokewa na Bi Aisha na Abi Hureira (Allah awaridhie) kuwa: “Mtume (rehema na amani ya Allah iwe juu yake) alipotaka kuchinja dhabihu alikuwa akinunuwa
kondoo wakubwa, walionona na maksai. Mmoja humchinja kwa ajili ya waliompwekesha Allah na kushuhudia ufikishaji wake miongoni mwa umati wake, na
huchinja wa pili kwa ajili ya Muhammad na familia yake.” (Imesimuliwa na Ibn Majah).

Imam Baghawiy anaeleza: “Kuna baadhi ya wanazuoni hawapendezwi na maksai (mnyama aliyehasiwa) kwa sababu ya upungufu wa kiungo. Isipokuwa sahihi ni kuwa hakuna chukizo. Na kuhasiwa kuna tija katika kuiongezea ubora nyama, kuondoa shombo, harufu mbaya na ni kiungo kisicholiwa”.

Kuchagua dhabihu

Ibn Qayyim anaeleza: Ilikuwa desturi ya Mtume kuchagua mnyama anayetaka kumchinja kwa kuangalia anayependeza na aliyesalimika na dosari. Mtume
alikataza kuchinja chongo, aliyekatwa au kutobolewa masikio, aliyevun-
jika pembe, au kuwa na mkia kipisi.

Allah anasema: “Ndio hivyo! Na anayetukuza ibada za Mwenyezi Mungu, basi  hayo ni katika unyenyekevu wa nyoyo”(Qur’an, 22:32). Na katika kutukuza ni kuteua aliye na sifa timilifu. Allah anasema: “Kamwe hamtafikia wema mpaka mtoe katika vile mnavyovipenda. Na kitu chochote mnachokitoa basi hakika Mwenyezi Mungu anakijua”. (Qur’an, 3:92)

Mifugo inayofaa kutolewa dhabihu katika udh-hiyah

Wanyama wanaokidhi katika udh-hiya kwa makubaliano ya wanazuni ni kondoo, mbuzi, ng ’ombe na ngamia. Lakini wametofautiana wanazuoni juu ya ubora. Kwa upande wa madhehebu ya Shafii, wamefadhilisha ngamia, ng ’ombe halafu ndiyo kondoo au mbuzi.

Madhehebu ya Maliki wameafikiana na Shafii kwenye kafara na wakatofautiana kwenye udh-hiya. Wao, kwenye udh-hiya, wanafadhilisha kondoo na mbuzi, ng ’ombe halafu ndio ngamia. Na sababu ya kutofautiana kwao ni yale yaliyopokewa kutoka kwa Mtume kuwa alichinja kondoo, na Allah alimkomboa Ismail kwa kumletea Nabii Ibrahim kondoo.

Umri na aina ya wanyama wanaokubalika

Mtume aliruhusu aina ya wanyama wanaotakiwa katika udh-hiya, a’qiqah na kafara ambao ni; kondoo, mbuzi, ng’ombe na ngamia. Na umri wao, kwa ngamia awe amefikisha miaka mitano, ng ’ombe miaka miwili, na kadhalika mbuzi. Na kuna wanaosema mbuzi awe na mwaka mmoja, lakini kondoo kwa uchache awe na miezi sita.

Namna ya kuchinja

Kwa ngamia ni sunna kumchinja akiwa amesimama wima akielekea qibla na kumfunga mguu wake wa kushoto kwa kumkata koo. Mbuzi na kondoo huchinjwa kwa kulazwa ubavu na kuelekezwa qibla. Mchinjaji husema mfano wa maneno yafuatayo: “Bismillah, Wal-lahu Akbar, Allahumma minka walaka,
Allahumma taqabbal minniy kamaa taqab-balta min Ibrahim.”

Na kama anaweza kuchinja ni sunna kuchinja mnyama wake yeye mwenyewe, na kama hawezi, basi angalau awepo wakati wa kuchinja.

Nyama ya udh-hiya inaweza kugawanywa katika mafungu matatu. Fungu la kwanza atachukua mchinjaji na familia yake, fungu la pili awagawie ndugu, jamaa au majirani zake na tatu atoe sadaka.

Hekima ya mafungu haya matatu:

Mosi, kufurahia neema ya Allah, na ambayo ni kula sehemu ya nyama ya hilo dhabihu wewe na familia yako. Pili, kutaraji thawabu kwa kuwagawia ndugu na majirani sehemu ya nyama hiyo). Na tatu, kuimarisha upendo na uhusiano kwa kuwatunukia waja wa Mwenyezi Mungu (yaani kutoa sadaka) hata kwa kuwagawia matajiri.

Wakati unaoruhusiwa kunyoa nywele na kukata kucha

Imepokewa na Imamu Muslim kutoka kwa Bi. Aisha kuwa mtu atakayekuwa na kichinjo na anataka kukichinja, utakapoandama mwezi wa mfunguo tatu, asikate
kucha wala asinyoe nywele mpaka achinje. Imamu An Nawawiy, Said bin Musayyib,
Rabia, Ahmad, Is-haq, na Daudi, na baadhi ya wafuasi wa madhehebu ya Shafii
walisema ni haramu kukata chochote mwilini mpaka amalize kuchinja na tena iwe katika wakati wa kuchinja. Na Imam Shafii anasema: “Ni Makuruhu na karaha yenyewe ni ya utakaso”. Na Abu Hanifa naye amesema: “Ni makuruhu.”
Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close