6. Kutoka Katika Quran na Sunnah

Sala, amali ya kwanza kuhesabiwa siku ya kiyama

Neno Swala, kwa lugha ya Kiarabu linamanisha kuomba dua. Katika muktadha wa sharia ya Kiislamu, Swala ni kumuelekea Allah Mtukufu kwa kauli na vitendo mahsusi, vinavyoanza na takbira na kuhitimishwa na utoaji salamu.

Swala ina nafasi kubwa na adhimu katika Uislamu. Swala inachukua nafasi ya pili katika mpangilio wa nguzo za Uislamu, ikitanguliwa na tamko la shahada mbili. Na Allah Mtukufu ameiweka Swala miongoni mwa ibada zinazomuwajibikia Muislamu kila siku ili mja apate kuwa katika mawasiliano na Mola wake siku zote.


Na kudumisha utekelezaji wa Swala kunaufanya moyo utambue Utukufu wa Allah, Muumba mbingu na ardhi, na vyote vilivyomo ndani yake, kwa kumnyenyekea yeye na kukiri utukufu wake pamoja na izza yake

Na Allah amezifaradhisha Swala tano, wakati Mtume (rehema na amani za Allah ziwe juu yake) bado akiishi katika mji wa Makka, ukiwa umebakia mwaka mmoja tu kabla ya kuhamia Madina. Allah alizifaradhisha Swala tano kwa waja wake ili wamuabudu yeye peke yake, na wala asimshirikishe na kitu chochote katika ibada zake, kwa kauli yake Allah mtukufu: “Hakika Swala kwa waumini ni faradhi iliyowekewa nyakati maalumu.” (Qur’an, 4:103). Na Allah Mtukufu amezijaalia Swala tano kuwa ni sababu ya kuzitakasa roho na nafsi kutokana na athari mbaya za madhambi.

Na Mtume (rehema na amani za Allah ziwe juu yake) amezimithilisha Swala tano na taswira nzuri yenye kufahamika kirahisi akilini mwa wanadamu. Mtume aliwaambia Maswahaba: “Hivi mnaonaje, lau kwamba mto wa maji unakuwa mlangoni mwa mmoja wenu, huoga katika mto huo kwa siku mara tano, je utabakia uchafu katika mwili wake?” Maswahaba wakajibu: “Hauwezi kubaki aina yoyote ya uchafu katika mwili wake”.
Mtume akasema: “Basi hivyo ndivyo zinavyofanya kazi Swala tano, Allah hufuta madhambi kwa sababu ya Swala tano.” (Muslim).

Na Swala ndio amali bora na tukufu zaidi katika Uislamu, ni nguzo kubwa ya dini, na ni wajibu wa kwanza uliolazimishwa na Allah katika ibada.
Swala pia ni amali ya kwanza itakayoanza kuhesabiwa na Allah siku ya kiyama. Pia, isitoshe Swala ndio ibada pekee iliyopata bahati ya kuwekewa sheria na Allah, hali ya kuwa Mtume akiwa yupo mbinguni katika safari
yake ya Israai na Mi’raj.

Aidha, umuhimu wa Swala unadhihirika kwa uwazi katika upande wa utekelezaji wake, kwa kuwa amri ya kudumu juu ya utendaji wake imekuja kwa kuzingatia hali zote – ile ya nyumbani na ugenini. Allah anasema:
“Na mnaposafiri katika nchi si vibaya kwenu kama mkifupisha Swala…” (Qur’an, 4:101). Vilevile , Swala imefaradhishwa katika hali ya amani au vita na hofu, kwa kauli yake Allah Mtukufu: “Na unapokuwa pamoja nao,
ukawasalisha, basi kundi moja miongoni mwao wasimame pamoja nawe na wachukue silaha zao.” (Qur’an, 4:102).

Na Qur’an imeipa Swala hadhi na taadhima ya juu, kwani haikuitaja Swala ila imeikutanisha pamoja na jambo zito. Kwa mfano Swala imetajwa
sambamba na Dhikri, kwa kauli yake Allah Ta’ala: “Soma uliyofunuliwa katika kitabu, na usimamishe Swala. Hakika Swala inazuilia mambo machafu na maovu. Na kwa yakini kumdhukuru Allah ndilo jambo kubwa
kabisa.” (Qur’an, 29:45). Na mara nyingine Qur’an inaitaja Swala kwa kuikutanisha pamoja na Zaka, kwa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na shikeni, Swala na toeni Zaka..” (Qur’an, (2:43) Na kuna wakati Qur’an
inaikutanisha Swala pamoja na subira, kwa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: “Na tafuteni msaada kwa kuswali na kusubiri.” (Qur’an, 2:45).

Na kudumisha utekelezaji wa Swala kunaufanya moyo utambue Utukufu wa Allah, Muumba mbingu na ardhi, na vyote vilivyomo ndani yake, kwa kumnyenyekea yeye na kukiri utukufu wake pamoja na izza yake. Kwa hiyo siku zote mja anakuwa katika hadhari, anafuata maamrisho yake, na kuacha makatazo yake. Vilevile, Swala ina athari chanya katika kuifundisha
adabu nafsi ya Muislamu kwani huinyoosha tabia yake, huongeza chamungu na imani ndani ya moyo, hufundisha nidhamu na kuchunga ahadi na utekelezaji wa mambo kwa kuzingatia muda wake.
Pia, utekelezaji wa Swala unamfanya mja awe na mawasiliano na mola wake moja kwa moja, na husimama mbele yake akinong’ona naye kwa unyenyekevu, huku akijenga matumaini ya kupata rehema zake na kujiepusha na adhabu yake. Na mawasilano haya na Allah yanajirudia kwa kule kujirudia kwa nyakati za Swala na hivyo basi humliwaza mtu kutokana na uchovu wa kazi na hujenga matumaini yenye nguvu kwa Mola wake. Imepokewa kauli kutoka kwa mmoja wa watu wema waliotangulia:
“Ninapokuwa na shida ya kutaka kunong’ona na Mola wangu, basi huingia
katika utekelezaji wa ibada ya Swala, na iwapo Allah anataka kuongea nami, basi huanza kuisoma Qur’an.”

Aidha, Swala ni sehemu ya mazoezi ya kiroho na viungo vya mwili. Usafi wa moyo na mwili ni sharti katika kusihi kwa Swala. Allah Mtukufu amesema: “Na mkiwa na janaba basi ogeni.” (Qur’an, 5:6). Na miongoni mwa athari nzuri za kiroho zanazosababishwa na Swala ni hisia nzuri ya ladha anayoipata mja anayetekeleza Swala ndani ya nafsi yake. Mtume (rehema na amani za Allah ziwe jua yake) amesema: “Ukaribu anaoupata mja kutoka kwa Mola wake, ni pale anapokuwa katika hali ya kusujudu.” (Muslim)

Na athari nzuri ya Swala haiishii kwa mtu mmoja mmoja tu, bali Swala kama ambavyo imeelezwa na Uislamu ni mfumo kamili wa malezi ya umma, hasa uizingatia vitendo vyake vya dhahiri na uhalisia wake wa ndani.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close