6. Kutoka Katika Quran na Sunnah

Rudi kawafanyie wema wazazi wako

Ibnu Umar (Allah amridhie) amesimulia kuwa, mtu mmoja alikuja kwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshuke) akasema: “Nimekuja kukupa ahadi ya utii juu ya kufanya Hijra (kuhama) pamoja nawe kwenda kwenye Jihad.” Mtume akamuuliza: “Je, kati ya wazazi wako wawili yupo aliye hai?” Akasema: “Ndio, wote wapo hai.” Mtume akamuuliza: “Je, unatafuta ujira mkubwa kutoka kwa Allah?” Akasema: “Ndio.” Mtume akasema: “Rudi nenda ukawafanyie wema (wazazi wako).” (Bukhari na Muslim).

Katika Uislamu wazazi wamepewa nafasi, uzito na heshima ya kipekee. Mwenyezi Aliyetukuka anasema: “Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia uzee, naye yuko kwako, au wote wawili, basi usimwambie hata ‘Ah!’. Wala usiwakemee. Na sema nao kwa msemo wa heshima. Na uwainamishie bawa la unyenyekevu kwa kuwaonea huruma. Na useme, ‘Mola wangu Mlezi! Warehemu kama  walivyonilea utotoni.” (Qur’an, 17:23-24).

Hapa Allah Aliyetukuka anawakumbusha watoto kuwafanyia wema na ihsani wazazi wao kwa kuwa hiyo ni ibada inayopendwa na kuridhiwa na Allah. Mwenyezi Mungu Aliyetukuka ameahidi malipo makubwa duniani na Akhera kwa yeyote atakayechunga haki za wazazi wake wawili na kuwaheshimu. Ni ubaya ulioje kwa mtu anayepuuza jukumu hili.

Abdullah bin Abbas (Allah amridhie) amesema kuwa, aya tatu zimekutanishwa na mambo matatu, halitokubaliwa mojawapo pasi na mwenzake:

Kwanza, mtiini Allah na Mtume (Qur’an, 5:92). Maana yake, atakayemtii Allah pasi na kumtii Mtume; utiifu wake hautokubalika. Pili, simamisheni Swala na toeni Zaka (Qur’an, 2:43). Maana yake, atakayesimamisha swala na hakutoa Zaka hali ya kuwa uwezo anao, atajiweka katika mazingira magumu ya kukubaliwa ibada yake. Tatu, unishukuru mimi  pamoja na wazazi wako (Qur’an, 28:12). Maana yake, atakayemshukuru Allah na hakuwashukuru wazazi wake, shukurani hizo zitakuwa hazina maana.

Mafunzo ya tukio hili

Kutokana na uzito wa jambo hili, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alimkataza Swahaba wake kwenda kwenye Jihad na badala yake alimuamuru kurejea kwa wazazi wake ili akasimamie kikamilifu mahitaji yao.  Watu wengi wanapuuza haki hii ya msingi ya wazazi wawili. Na pia, ni ukweli kuwa wapo baadhi ya watu wanaowafanyia ubaya na kuwaasi wazazi wao.

Namna ya kuwafanyia wema wazazi

Kuna namna nyingi za kuwafanyia wema wazazi. Miongoni mwa hizo ni kuitika wito wao na kutekeleza mahitaji yao kadiri inavyowezekana na pia kuwafadhilisha na kuwapa heshima na hadhi ya juu. Usiwe mwenye kuwatembelea wazazi wakati wa  matukio maalumu, bali watembelee mara kwa mara na ujipendekeze kwao.

Namna nyingine za kuwafanyia wema wazazi wawili ni  kuwashauri katika mambo mbalimbali na kuthamini ushauri wao, kuwaombea dua kila wakati, kuwahimiza kudumisha swala na kufanya mambo mbalimbali ya heri kadiri watakavyoweza na kuwaheshimu wakati wote na katika mazingira yote, mbele za watu, hata mkiwa peke yenu.

Watunze wazazi wako kadiri inavyowezekana na kamwe usiwatelekeza au kuwaacha wafanyakazi wawahudumie pasi na juhudi zako kuonekana. Vilevile, waheshimu wazazi wako na uwaoneshe watu kuwa hiyo ni tabia yako na si maigizo.

Mambo yasiyofaa kufanyiwa wazazi

Haifai kuwaliza au kuwahuzunisha wazazi, iwe kwa kauli au vitendo. Hilo ni jambo baya mno mbele ya Mwenyezi Mungu. Haitakiwi mtoto awe  ndio chanzo cha wazazi wake kutokwa na machozi. Pia, ni dhambi kuwakemea, kuguna, kukiuka amri na maelekezo yao,  kuwakunjia uso au kunyanyua sauti juu yao.

Ni ukweli kuwa wapo baadhi ya watu wanaoonesha nyuso za bashasha kwa watu wengine lakini wanawakunjia uso na kuwakasirikia wazazi wao na kuwatazama kwa dharau hususan pale wanapowataka wawasaidie kazi mbalimbali.

Haifai, na pia ni haramu kubishana na wazazi, kuwatukana, kutowashauri katika mambo mbalimbali, kutothamini rai na mawazo yao, kuingia chumba au nyumbani mwao bila hodi, kuwavunjia  heshima kwa kufanya vitendo viovu kama wizi, kutukana au kuanzisha ugomvi na ndugu na jamaa. Kufanya hayo kunaweza kuwaingiza wazazi wako katika tuhuma mbalimbali na hivyo kuishi na majonzi na huzuni.

Pia, haifai kuwalipisha wazazi madeni yasiyowahusu au kufanya kosa litakalopelekea aitwe shule, kutaja aibu zao mbele ya watu wengine, kuwalazimisha wakununulie vitu wasivyo na uwezo navyo, kumfadhilisha mke juu yao, kuwapeleka kwenye nyumba za kulelewa wazee wakati una uwezo wa kuwahudumia, kuwafanyia ubahili na kufanya masimbulizi, yaani  kuhesabu mema uliyowafanyia.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close