6. Kutoka Katika Quran na Sunnah

Niliogopea nafsi yangu ewe Khadija

Mara baada ya kujiwa na Malaika Jibril kwa mara ya kwanza katika pango la Hiraa, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alipatwa na hofu kubwa na kuamua kurudi kwa Bi. Khadija bint Khuwaylid (Allah amridhie). Mtume aliwaambia watu waliokuwa nyumbani kwa Bi. Khadija:

“Nifunikeni nifunikeni.” Baada ya hofu kumuondoka akamsimulia mkewe (Bi. Khadija) yote yaliyotokea katika pango la Hiraa. Mtume alimwambia Bi. Khadija: “Niliogopea nafsi yangu (ewe Khadija), kuna kitu (kibaya) kinaweza kunitokea.” Bi. Khadija akamwambia: “Hapana! Naapa kuwa Allah hatokudhalilisha kamwe. Wewe una uhusiano mzuri na ndugu na marafiki, utakuwa mkweli kwa watu, utawasaidia masikini na mafukara, utawakirimu wageni wako na utawasaidia watu katika mambo ya kheri.” [Bukhari na Muslim].

Mafunzo ya tukio hili: Tukio hili, kwanza linaonesha namna Bi. Khadija (Allah amridhie) alivyoshirikiana na mumewe (Mtume Muhammad – rehema za Allah na amani zimshukie) katika kuiendeleza dini ya Allah.

 Bi. Khadija alikuwa mwanamke mwema, mpole, mchamungu na alitumia kiasi kikubwa cha mali yake kuihami dini ya Allah (Uislamu). Bi. Khadija hakuishia hapo, alihakikisha pia kuwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) anapata utulivu wa moyo ili aweze kutekeleza majukumu yake ya msingi likiwamo la kuwafundisha watu tauhidi.

Bi. Khadija alimpa Mtume nguvu na hamasa kubwa ya kuendelea kulingania dini ya Allah na kumtaka ategemee mazuri kutoka kwa Allah. Baada ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) kufika nyumbani akiwa anatetemeka, Bi. Khadija (Allah amridhie) alilitafsiri tukio hilo kama ishara na muujiza kutoka kwa Allah.

Bi. Khadija alimpa matumaini Mtume na kumtabiria mafanikio makubwa katika kazi ya da’awa. Uwepo wa Bi. Khadija katika ardhi ya Makka uliletatija kubwa katika mchakato wa kuiendeleza dini ya Allah. Baada ya Bi. Khadija kufariki, Mtume alisema:

“Hakika Allah hajanipa badala yake mke bora kuliko Khadija. Wallahi (Khadija) aliniamini wakati watu waliponikataa, na akanihifadhi wakati watu waliponifukuza.”

Hali ilivyo sasa

 Bahati mbaya sana, wanaweke wengi katika zama hizi wametawaliwa na fikra finyu ambazo k w a kiasi kikubwa zinaelemea kwenye maslahi ya kidunia. Baadhi ya wanawake wamesahau majukumu yao ya malezi pamoja na kuwasaidia waume zao kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo katika familia.

Pia wapo wanawake wanaowalazimisha waume zao kufanya mambo yenye maslahi ya kidunia. Aghalabu wanawake wa namna hii huhangaika kila uchao kutafuta pesa kuliko waume zao. Asubuhi wanakwenda mjini na jioni wanarudi nyumbani kama wafanyavyo wanaume.

Wanawake wengi wa kizazi cha sasa hawazingatii mipaka iliyowekwa na sharia ya Kiislamu ambayo inamtaka mwanamke kuvaa hijab ya kisharia anapokuwa kazini au nje ya nyumba yake na kuepuka kuchanganyika na wanaume ambao si maharim wake.

Wanawake wengi wameyapuuza maagizo haya mema kutokana na tamaa ya kuishi maisha mazuri. Ukiwauliza uzuri wa dunia ni upi wanatoa majibu mepesi yatokanayo na mawazo ya kubuni.

Vipaumbele vya maisha ya mwanamke

Mwanamke ameumbwa na mahitajio mengi ambayo hana budi kuyapata ili aweze kuishi kwa furaha na amani hapa ulimwenguni. Hata hivyo, Uislamu unamtaka mwanamke kuzingatia vipaumbele vilivyojikita katika majukumu yake ya msingi ambayo yanawiana na maumbile yake.

Mwanamke wa Kiislamu anapaswa kujituma na kujitoa kwa ajili ya dini yake sambamba na kutafuta mali kwa njia ya halali. Allah anasema:

“Wanaume wanayo sehemu kamili ya vile walivyochuma na wanawake wanayo sehemu kamili ya vile walivyovichuma. Na muombeni Mwenyezi Mungu fadhila zake hakika ya Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa kila kitu.” [Qur’an, 4:32].

Uislamu umeweka sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya kuchuma mali, ambayo ina uhusiano wa moja kwa moja na dhana ya ibada. Hivyo, mwanamke wa Kiislamu ana haki ya kuchuma mali kwa kuchunga mipaka ya haramu na halali katika kuchuma huko ili aweze kusimamia na kutekeleza amri ya dini yake pamoja na mambo ya kidunia yanayomkabili.

Khadija bint Khuwaylid, kigezo chema kwa wanawake

Khadija bint Khuwaylid (Allah amridhie) anazingatiwa kama mwanamke wa kutolewa mfano katika dini ya kiislamu. Kwa hakika Bi. Khadija alijipamba kwa sifa za kipekee ambazo zinamtofautisha na wanawake wengi wa zama hizi. Khadija alijipamba na sifa zote njema na kufikia daraja ya juu ya uchaji Mungu.

 Mke mwema

Bi. Khadija (Allah amridhie) alisifika sana kwa uzuri wa tabia na maumbile. Mja mwema huyu (Bi. Khadija) aliishi kwenye ndoa na mume wake (Mtume Muhammad rehema za Allah na amani imshukie) kwa utulivu na amani. Khadija alitumia muda wake mwingi kumliwaza Mtume baada ya tabu na mihangaiko mingi ya mchana na alijitahidi sana kuepuka mifarakano baina yake na mumewe (Mtume).

Katika kutilia mkazo suala hili, Mtume (rehema za Allah na amani imshukie) amesema:

“Mwanamke atakaposwali sala zake tano, akafunga mwezi wake (Ramadhan), akahifadhi utupu wake (asifanye uzinifu) na akamtii mumewe, ataingia peponi kupitia mlango autakao.” [Ibnu Hibban].

Hadith hii inatoa bishara njema kwa mwanamke atakayemtii mumewe na kutekeleza kikamilifu ibada tulizozitaja hapo juu. Pepo ya Mwenyezi Mungu ipo wazi. Hivyo, wanawake wa Kiislamu hawana budi kuwatii waume zao na kutekeleza kikamilifu ibada za Allah ili waingie peponi bila ya kuhesabiwa.

Bi. Khadija na malezi ya familia

Bi. Khadija (Allah amuwie radhi) aliwalea watoto wake katika maadili ya dini na kuwaamrisha kutekeleza ibada za wajibu na Sunna. Mtume (rehema za Allah na amani imshukie) amelipa kipaumbele suala la maadili pale aliposema:

“Hakika nimetumwa kwa ajili ya kutimiza tabia njema.” [Buhkari].

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close