6. Kutoka Katika Quran na Sunnah

Nafasi ya Qur’an katika kuratibu mahusiano ya kiutu

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema na mwenye kurehemu. Rehema na amani zimuendee bwana wetu Muhammad pamoja na Maswahaba zake, na Jamaa zake.

Baada ya utangulizi huo, hakika hii Qur’an ndiyo msingi wa suala lolote linalohusiana na dini ya Kiislamu . Qur’an ni mfumo unaoafikiana na hali na zama zote, na wala hakuna shaka katika hili kwa wenye kutumia mantiki sahihi. Qur’an ina kila kinachohitajiwa na jamii ya Kiislamu katika kuimarisha mahusiano yanayowaunganisha wafuasi wake na jamii nyingine na katika mazingira yoyote.


Nyinyi mmekuwa bora ya umma waliotolewa (katika) watu, kwa kuwa mnaamrisha mema na mnakataza maovu, na mnamuamini Mwenyezi Mungu. Na lau kuwa Watu wa Kitabu nao wameamini ingelikuwa bora kwao. Wapo miongoni mwao Waumini, lakini wengi wao wapotovu.


[Qur’an 3:110].

Kwa kuanzia, Qur’an inaimarisha nyumba ya Muislamu kuanzia jamii ndogo inayoundwa na mume, mke na kuiwekea jamii hiyo misingi ya mahusiano katika hatua zote. Qur’an kwa kuweka misingi hiyo, inaifanya jamii iishi katika hali ya utulivu na upendo, kama Mwenyezi Mungu anavyosema: “Na katika Ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia upendo na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanaofikiri..” [Qur’an. 30: 21].

Hakika miamala ya mahusiano ya kiutu inasimamiwa Allah Aliyetukuka kama anavyotaja katika kauli yake: “Wala msisahau fadhila baina yenu. Hakika Mwenyezi Mungu anayaona mnayoyatenda.” [Qur’an, 2:237]. Hii ni ishara kuwa, Qur’an tukufu haisumbuliwi na kadhia yoyote ile bali huizungumza kulingana na wakati.

Ni kwa misingi hiyo ndiyo tunazikuta Aya nyingi zinazuizungumzia nyumba ya Muislamu kwa upande wa masuala ya kijamii na kisha kuzungumzia mahusiano na watu wengine. Kiunganishi cha mafungamano na mahusiano yote haya kati ya haya makundi ni kule Muislamu kutakiwa kila siku aishi kulingana na mazingira na watu mbalimbali.

Na tunapoyaangalia mahusiano kati ya jamii ya Kiislamu na jamii nyingine, tunaikuta Qur’an imeshatueleza na kutuelekeza. Kwa mujibu wa Qur’an, katika hatua ya awali, utaikuta jamii ya Kiislamu inafanya kazi ya kuongoa ikilingani kwenye njia ya Mwenyezi Mungu. Jukumu lake hili la kwanza ni kuwavuta watu kwenye njia ya Mwenyezi Mungu; na mtu mwenye jukumu hili, hawezi katu kugongana na wengine. Huyu atakuwa anafanya kazi ya kuzivuta nyoyo kwa wema. Ushahidi wa hili ni mwingi.

Kwa mfano kutoka katika Qur’an ni neno la Mwenyezi Mungu: “Nyinyi mmekuwa bora ya umma waliotolewa (katika) watu, kwa kuwa mnaamrisha mema na mnakataza maovu, na mnamuamini Mwenyezi Mungu. Na lau kuwa Watu wa Kitabu nao wameamini ingelikuwa bora kwao. Wapo miongoni mwao Waumini, lakini wengi wao wapotovu.” [Qur’an 3:110].

Hapa, jamii ya Kiislamu haikujitoa yenyewe bali imejitoa kwa lengo la kuwalingania watu katika katika njia njema. Ushahidi mwingine ni neno la Mwenyezi Mungu: “Sema, ‘Hii ndiyo Njia yangu – ninalingania kwa Mwenyezi Mungu kwa kujua – mimi na wanaonifuata. Na ametakasika Mwenyezi Mungu! Wala mimi si katika washirikina.’” [Qur’an, 12:108]

Jamii inayolingania katika andiko na njia ya Mwenyezi Mungu katu haiwezi kulingania katika vita. Na katika Sunna, Mtume [rehema za Allah na amani zimshukie), amesema: “Kwa hakika ninyi mmeletwa kuja kuwawepesishia mambo watu, wala hamkuletwa kuja kuwatilia watu uzito.” Ni katika andiko hili ndipo unapopatikana uteule wetu kama Waislamu unaofanana na ule wa Manabii. Hivyo basi, kwa kuwa Uislamu unaendelea kuwepo, utaendelea kubaki sambamba na wanaoulingania.

Pia katika Sunna za kivitendo kutoka kwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ni kuwa, Mtume alikuwa mpole kwa watu aliokuwa akijadiliana nao mongoni mwa Mayahudi, Manaswara na makabila ya Kiarabu kwa yale aliyokuwa anayalenga katika kuzivuta nafsi. Ni kwa sababu hii ndio maana tunakuta kwenye Qur’an: “Sema, ‘Enyi Watu wa Kitabu! Njooni kwenye neno lilio sawa baina yetu na nyinyi, Ya kwamba tusimuabudu yeyote ila Mwenyezi Mungu, wala tusimshirikishe na chochote, wala tusifanyane sisi kwa sisi kuwa Walezi badala ya Mwenyezi Mungu.’ Na wakigeuka basi semeni, ‘Shuhudieni ya kwamba sisi ni Waislamu.’” [Qur’an, 3:64].

Mtindo huu wa wito umesheheni huruma na unadhihirisha kuwa msingi wa mahusiano kati ya Waislamu na watu wengine ni amani na wala siyo vita, uhaini, vurugu na wala pia siyo migogoro. Jambo hili ndiyo linasisitiz-wa katika Aya nyingi za Qur’an, ikiwemo kauli yake Mwenyezi Mungu: “Anayekushambulieni nanyi mshambulieni, kwa kadri alivyokushambulieni. Na mcheni Mwenyezi Mungu. Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu yu pamoja na wachamungu.” [Qur’an, 2:194].

Basi, kwa mtu yeyote anayedai kuwa uhusiano kati yetu na makafiri ni uhusiano wa kimapambano na mapigano huyu ni miongoni mwa wahalifu wa dini waliofurutu ada. Hawa wanaohubiri mapambano wanapaswa kuielewa dini yao kabla ya kuitangaza au vinginevyo waachane na fatwa, ili wasiuharibu Uislamu kama ilivyo leo.

Ama aliyepanda hoja kwa kutumia kauli ya Mwenyezi Mungu: “Na piganeni na washirikina wote kama wao wanavyopigana nanyi nyote. Na jueni kuwa Mwenyezi Mungu yu pamoja na wachamngu.” [Qur’an 9:39], amepuuza kwa makusudi sababu, nayo ilikuwa “…kama wanapigana nanyi nyote.”

Sababu ya vita ni vita. Sababu inapokosekana, vita hutoweka. Ushahidi wa hilo ni kutoka katika Sunna ya Mtume na sira inayoonesha kuwa aliwaacha Wakristo wa Hajar na Toghlob na dini yao, kama alivyowaacha wapagani wa Aman na Hajar katika upagani wao.

Kadhalika, Aya ya Surat An – Nisai imewafanya watu wote kuwa ni watu wanaotoka katika uzao mmoja. Ni Aya hii ndiyo inayojenga mahusiano kati ya watu, kwa msingi wa wema, uchamungu, kusaidiana, na kubadilishana maslahi, jambo ambalo ndiyo tegemeo la maisha ya watu.

Mwenyezi Mungu anasema: “Enyi watu! Mcheni Mola wenu Mlezi aliyekuumbeni kutokana na nafsi moja, na akamuumba mkewe kutoka nafsi ile ile. Na akaeneza kutokana na wawili hao wanaume na wanawake wengi. Na tahadharini na Mwenyezi Mungu ambaye kwaye mnaombana na jamaa zenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwaangalieni.” [Qur’an 4:1].

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close