6. Kutoka Katika Quran na Sunnah

Mwenye kujifananisha na watu yu pamoja nao

Kutoka kwa Abdullah bin Umar (Allah amridhie) amehadithia kwamba, Waislamu walipokwenda Madina, walikuwa wakikusanyika na kusubiri sala bila kuwapo adhana. Siku moja wakalizungumzia jambo hilo. Baadhi wakasema: “Tupigeni kengele kama wanavyofanya Manasara.” Wengine wakasema: “Tupulizeni tarumbeta kama wanavyofanya Mayahudi.” Umar (Allah amridhie) akawaambia: “Kwa nini msimpeleke mtu akaadhini?” Mtume (rehema za Allah na amani imshukie) akasema kumwambia Bilal: “Ewe Bilal! Simama uadhini.” [Muslim].

Mwanzo wa adhana wakati wa sala Tukio hili, kwanza linaonesha hali ngumu ya maisha waliyopitia Waislamu baada ya kuhamia Madina. Katika mji wa Makka Waislamu walikuwa wachache, na hawakuwa na uhuru wa kudhihirisha ibada zao kutokana na vitisho walivyokuwa wakivipata kutoka kwa maadui zao.

Hali hiyo iliwafanya Waislamu kutafuta njia ya kuwajulisha kwamba muda wa sala umewadia ili wapate wasaa wa kwenda msikitini na kuswali jamaa. Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alitoa ushauri kwa Maswahaba zake (Allah awaridhie wote) kutafuta njia ya kuwajulisha muda wa sala.

Katika mashauriano hayo, zilitolewa rai mbalimbali ambazo hata hivyo Mtume alizikataa.

Rai ya kwanza: Kunyanyua bendera

Mtume alikataa rai ya kunyanyua bendera, kwani ilionekana wazi kuwa haiwezi kuwasaidia watu wengi hasa wakati wa usiku.

Rai ya pili: Kupiga kengele

Pia Mtume alikataa katu katu rai ya kutumia kengele, kupuliza pembe na kuwasha moto kama njia ya kuwajulisha waumini muda wa sala. Mtume alipinga rai hizo kwa sababu kupiga kengele ni ada ya Manasara katika ibada zao, kupuliza pembe ilikuwa desturi ya Mayahudi na kuwasha moto ni ibada ya Wamajusi.

Kwa hivyo, Mtume akayakataa mambo yote hayo kwa sababu ya ubaya wa kujifananisha na wasiokuwa Waislamu katika ibada, tabia na desturi zao. Baada ya majadiliano kumalizika na watu wote kutawanyika, Abdullahi Ibnu Zaid (Allah amridhie) aliota ndoto akiwa anapiga adhana.

Abdullahi alimfahamisha Mtume suala hilo, naye akamwambia: “Hiyo ni ndoto ya kweli.” Kisha Mtume akamuamrisha Abdullahi amfundishe Bilal kupiga adhana. Bilal alikuwa na sauti nzuri ya kupiga adhana.

Ubaya wa kujifananisha na wasiokuwa Waislamu

Mtume (rehema za Allah na amani imshukie) alikataa matumizi ya kengele, pembe na moto kwa sababu kufanya hivyo ni kujifananisha na Mayahudi na Manasara.

Kwa bahati mbaya sana, wapo miongoni mwetu Waislamu ambao hawajiwekei mipaka katika mambo yanayofungamana na ibada, wanaiga mila na desturi za Mayahudi na Manasara ikiwamo salamu. Kutoa salamu, yaani kusema ‘Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh’ ni katika ibada zenye malipo makubwa mbele ya Allah. Hata hivyo, baadhi ya Waislamu wamekuwa wakiwatolea watu salamu zisizokuwa za Kiislamu.

Mfano wa salamu hizo ni ‘Bwana asifiwe’, Tumsifu Yesu kristo,’ na nyingine nyingi ambazo zinaashiria katika kuwaenzi na kuwatukuza Mayahudi na Manasara. Tatizo jingine linalowakabili Waislamu wengi, hasa vijana ni kuwaiga wasiokuwa waislamu katika tabia, mienendo na muonekano wao, mambo ambayo yanakwenda kinyume na mafundisho ya Uislamu.

Kuiga nyendo za Mayahudi na Manasara ni jambo linaloharibu maadili na tabia zilizojengwa katika misingi ya Uislamu.

Imepokewa kutoka kwa Abu Sa’iyd al–Khudriyy (Allah amridhie) kwamba, Mtume (rehema za Allah na amani imshukie) amesema: “Mtafuata nyendo za wale waliokuja kabla yenu hatua kwa hatua mpaka itafika hatua wakiingia katika shimo la kenge, na nyinyi mtaingia pia.” Maswahaba wakauliza: “Ewe Mjumbe wa Allah! Unamaanisha Mayahudi na Manasara?” Mtume akasema: “Ni nani wengine kama si wao?” [Muslim].

Ukii rejea Qur’an Tukufu utaona aya nyingi zinazowakataza Waislamu kujifananisha na Mayahudi na Manasara katika mambo yanayofungamana na dini.

Mathalan katika Suratul Jaathiya [Qur’an, 45:18–19], Mwenyezi Mungu anasema: “Kisha tukakuweka wewe juu ya njia ya haya mambo (kwamba kila kilichomo ndani ya Qur’an na Sunna), basi ifuate, wala usifuate matamanio ya wasiojua kitu. Kwa hakika hao hawatakufaa kitu mbele ya Mwenyezi Mungu. Na hakika wenye kudhulumu ni marafiki wao kwa wao. Na Mwenyezi Mungu ni rafiki wa wamchao (Yeye).” Allah akasema tena: “Basi simameni sawa sawa, wala msifuate njia za wale wasiojua.” [Qur’an, 10:89].

Na katika hadith iliyosimuliwa na Ibn Umar (Allah amridhie), Mtume (rehema za Allah na amani imshukie) amesema:

“Mwenye kujifananisha na watu, naye ni kama wao.” [Abu Daud].

Pia Jaabir (Allah amridhie) amesimulia kwamba, siku moja Mtume aliwajulisha kuwa anaumwa, Maswahaba wakaswali nyuma yake akiwa amekaa huku Abubakr akiwasikilizisha watu takbira ya Mtume. Sekunde chache baadaye, Mtume aliwageukia Maswahaba zake akaona wamesimama, akawaashiria, wakakaa na kuswali nyuma yake hali ya kuwa wamekaa.

Baada ya kutoa salamu Mtume akawaambia: “Mmekaribia hivi punde kufanya kitendo cha Wafursi (Wamajusi waliokuwa wakiabudia moto) na Warumi. Wao wanawasimamia wafalme wao wakiwa wamekaa, basi msifanye hivyo. Wafuateni maimamu wenu. (Imam) akiswali kwa kusimama, nanyi swalini kwa kusimama, na akiswali kwa kukaa nanyi swalini kwa kukaa.” [Muslim].

Neema ya Uislamu

Hakuna neema kubwa hapa duniani kama Uislamu. Hakika amefaulu mwenye kusilimu na akashikamana na mafundisho ya dini na kumfuata kikamilifu Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) katika ibada, tabia na mwenendo wake.

Waislamu wa mwanzo waliposhikamana na dini na kumfuata Mtume kisawasawa walipata ushindi dhidi ya maadui zao, pia walifanikiwa kukomboa miji mingi na kuifikisha haki katika maeneo mbalimbali ulimwenguni. Lakini kwa sababu ya kuacha mafundisho ya dini yao na kujifananisha na wasiokuwa waislamu katika ibada, tabia na desturi zao, Waislamu wa zama hizi wamekuwa dhaifu, wanyonge, na wakati mwingine wanalazimika kujidhalilisha na kujipendekeza kwa watu ilimradi wapate chochote.

Kutafuta nguvu, heshima na cheo hakupatikani ila kwa kufuata mafundisho ya Allah na Mtume wake. Qur’an Tukufu inasimulia habari ya wanafiki:

“Wanasema: Tutakaporudi Madina, mwenye hadhi zaidi bila shaka atamfukuza humo aliye dhalili, ilihali utukufu ni wa Allah na Mtume wake na wa Waumini, lakini wanafiki hawajui.” [Qur’an, 63:8].

Naye Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Si katika sisi (Waislamu) mwenye kujifananisha na wasiokuwa sisi. Msijifananishe na Mayahudi na Manasara.” [Tirmidhiy].

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close