6. Kutoka Katika Quran na Sunnah

Mtazamo wa Uislamu juu ya misiba

Katika maisha ya kila siku hapa ulimwenguni mwanadamu hupitia vipindi mbalimbali vyenye sura na hali tofauti. Maisha yamefumwa kwa mtindo wa shida na raha, misiba na furaha, kupata na kukosa, maradhi na uzima, njaa na shibe na mengine yenye vinyume kama hayo.

Ni kutokana na hali hii ya maisha ya dunia ndiyo inadhihirika thamani ya maisha ya peponi ambako kila anayoyatamani binadamu ya kumburudisha hayana vinyume vyake. Yaani yote ni mazuri tu.

Misiba, huzuni na misukuosuko ni maumbile ambayo Allah amewaumbia waja wake na kamwe binadamu hana namna ya kuyakwepa, hata kama hawaipendi misukosuko hiyo na hata kama wakifanya jitihada kubwa ya kutaka kuizuia.

Mara nyingine, misukosuko husababishwa na mwanadamu mwenyewe. Katika Qur’an tunasoma:

“Kwa hakika tutakujaribuni kwa mambo mbalimbali kama vile hofu, njaa, na upungufu wa mali, na vifo, na upungufu wa matunda. Na wape habari njema wavumilivu, ambao msiba unapowafika husema, ‘Sisi ni wa Allah na kwake tutarejea.” [Qur’an 2:155-156].

Naye Mtume (rehema za Allha na amani zimshukie) amesema:

“Mabalaa yataendelea kwa Muislamu mwanamume na Muislamu mwanamke, (kwa) yeye mwenyewe, wanawe na mali yake mpaka akutane na Mwenyezi Mungu akiwa hana dhambi.” [Tirmidhi].

Na katika hadith iliyopokelewa na Suhaib Rumi (Allah amridhie) amehadithia kwamba Mtume wa Allah (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema:

“Ni furaha kubwa iliyoje ya mambo ya Muislamu. Hakika, mambo yake yote kwake ni kheri. Akipata kheri hushukuru na inakuwa kheri kwake, na akipatwa na msiba husubiri na huwa kheri kwake pia.” [Muslim].

Ukweli huu unatakiwa utue vyema katika moyo wa mja. Muislamu asipokubali ukweli huu, atatawaliwa na fikra potofu za kukata tamaa ya maisha kila linapomfika tatizo hadi atamani aukimbie uhai huu kwa kujiharakishia kifo, kama dunia inavyoshuhudia matukio hayo kila uchao.

Kutoka kwa Abi Said na Abu Huraira (Allah amridhie) wamemsikia Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) akisema:

“Kwa balaa lolote linalomkuta Muislamu, iwe usumbufu, maradhi, huzuni, adha na sononeko la nafsi, hata mwiba unaomchoma, Mwenyezi Mungu humfutia makosa yake kwayo.” [Bukhari na Muslim].

Pia, tusome hadith ifuatayo:“Hakika, ukubwa wa malipo hutegemea ukubwa wa mitihani. Na Allah Aliyetukuka akiwapenda watu fulani huwatia majaribuni. Basi, atakayeridhia atapata ridhaa (za Allah) na atakayechukia, atapata hasira (za Allah).” [Tirmidhi].

Muongozo wa Uislamu wakati wa msiba (kifo)

Kama ambavyo Uislamu umeweka muongozo wa jinsi ya siyo tu kuitumia neema, bali pia kuifurahia familia inapokuwa salama; kadhalika dini hii tukufu imewaelekeza wahusika namna bora ya kuipokea misiba na kuamiliana nayo ili wanadamu, licha ya majaribu hayo, wabaki katika utiifu kamili kwa Allah na kujenga matumaini.

Kwa mujibu wa mafunzo ya Uislamu, misiba siyo shari, mapungufu au ghadhabu za Allah juu ya familia husika, bali ni tukio lenye mantiki linaloweza kuwapatia thawabu nyingi wafiwa iwapo watajielewa na kulipa tukio hilo haki zake inavyostahiki.

Hebu tuzizingatie hadith zifuatazo za Mtume (rehema za Allah na amaini zimshukie).

Kutoka kwa Ummu Salama (Allah amridhie) amehadithia kwamba Mtume aliingia kwa (Swahaba Mtukufu) Abu Salama akiwa amekodoa macho (ameshafariki). Akayaziba na kusema:

“Roho inapotolewa jicho huifuata”Watu (wafiwa) wakapiga makelele (wakilia kwa uchungu wa msiba). Basi hapo Mtume akasema: “Msijiapize (lieni lakini msijiombee mabaya) kwani Malaika huitikia ‘aamin’ kwa mnayoyasema.”

Kisha Mtume akasema: “Ewe Allah, msamehe Abu Salama, na tukuza daraja zake miongoni mwa walioongoka, na kuwe badala yake katika jamaa zake waliobakia, na utusamehe sisi na yeye ewe Bwana wa viumbe, na litanue na litie nuru kaburi lake.” [Muslim].

Katika hadith nyingine iliyosimuliwa na Ummu Salama Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema:

“Mnapofika kwa mgonjwa au maiti semeni maneno ya kheri kwa sababu Malaika huitikia amiin..” [Abu Daud].

Pia, amesema Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie):

“Yoyote atakayefikwa na msiba akasema, ‘innaa lillahi wa innaa ilaihi rraajioun. Ewe Allah, nilipe ujira katika msiba wangu, na unipe badala njema zaidi,’ Mwenyezi Mungu humlipa ujira na humpa badala njema…” [Muslim].

Katika hadith hizi, Mtume (rehema za Allah na amanizimshukie ) anawaagiza Waumini kuwa na subira na waseme maneno ya kumshukuru na kumridhisha Mwenyezi Mungu.

Pia, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amewaagiza Waumini waridhike na maamuzi ya Mwenyezi Mungu kwa kumuondoa jamaa yao wampendae. Si hivyo tu, Mtume ametahadharisha dhidi ya kuropoka ovyo maneno ya kumuudhi Allah.

Utasikia baadhi ya watu wanasema: “Jamani kwa nini sisi tu?” “Tumemkosea nini sisi Mungu?” “Bora ningekufa mimi…” na kauli nyingine kama hayo.

Wakati ndugu wanatoa kauli hizi za kuchupa mipaka, waelewe kuwa Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ametahadharisha kwamba ujumbe wa Malaika unakuwepo na kusikiliza wayasemayo.

Hebu turejee kauli nyingine ya Mtume (rehema za Allah na amani zishukie). Kutoka kwa Abu Musa (Allah amridhie) amesimulia kuwa Mtume wa Allah amesema:

“Anapokufa mtoto wa mja (Muislamu), Allah huwaambia Malaika wake, ‘Mmechukua roho ya mtoto wa mja wangu?’ Malaika husema, ‘Ndio, Mola wetu.’ Allah husema, ‘Mmelichukua tunda la moyo wake?’ Malaika husema, ‘Ndio, Mola wetu.’ Huwauliza tena, ‘Basi nini amesema mja wangu?’ Husema, ‘Amekushukuru na kutaka ujira.’ Mwenyezi husema, ‘Mjengeeni mja wangu nyumba peponi na muiite nyumba ya shukran.’”

Katika hadith hii, tunafahamishwa kwamba, Allah hutuma ujumbe mtukufu na maalumu wa Malaika kama tume kwenda nyumba ya familia iliyofiliwa kusikiliza wanachokisema kuhusu msiba wao. Kadhalika tumejifunza kwamba, msiba unaweza kuwa sababu ya wahusika aidha kuingia peponi au motoni

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close