6. Kutoka Katika Quran na Sunnah

Misingi ya Haki za Binadamu Katika Uislamu

Uislamu umeweka kanuni na sharia zinazolinda haki za binadamu kwa ukamilifu. Allah Mtukufu aliwaleta Mitume na Manabii ulimwenguni ili wawalinganie watu katika dini yake (Uislamu), lakini pia kuchunga na kulinda maslahi na haki za binadamu.

Haki za binadamu kwa mtazamo wa Qur’an

Allah Mtukufu anasema: “Bila ya shaka tumemuumba mwanadamu kwa umbo lilio bora kabisa.” [Qur’an, 95:4].

Kwa kuzingatia ubora huu wa mwanadamu, Uislamu unakataza mtu kujinyonga na unachukulia kitendo hicho kama kosa kubwa na uvunjaji wa haki za binadamu.

Hii ni kwa sababu, roho haimilikiwi na mwandamu na wala hakuiumba yeye, bali ni milki ya Allah, Muumba wa mbingu na ardhi. Kwa kuzingatia hilo, Imam Ash–Shaatib (Allah amrehemu) amesema katika kitabu chake kiitwacho Al–Muwafaqat:

“Nafsi ya mwanadamu inaingia katika haki ya Allah Muumba, hivyo mwanadamu haruhusiwi kuipeleka kwenye maangamizi.”

Kwa mantiki hiyo ni sahihi kusema kuwa, Muislamu hata akiwa mwema vipi iwapo ataishi kinyume na mafundisho ya Qur’an na Sunna, basi wema wake utakuwa hatarini kughiribika. Hebu sasa tutaje misingi mikuu ya haki za binadamu kwa mujibu wa Uislamu.

Mosi: Haki ya kutukuzwa

Binadamu ni kiumbe aliyetukuzwa na kufadhilishwa kuliko viumbe wote, ndio maana Allah Muumba amemuwekea sharia, taratibu na kanuni ili zimuongoze kufikia kilele cha maisha bora hapa Duniani na Akhera aendako.

Mwenyezi Mungu anasema: “Na hakika tumewatukuza wanadamu, na tumewapa vya kupanda nchi kavu na baharini, na tumewaruzuku vitu vizuri vizuri, na tumewafadhilisha kwa fadhila kubwa kuliko wengi miongoni mwa tuliowaumba.” [Qur’an, 17:70].

Uislamu, ambao ni dini ya uadilifu na huruma umeweka adhabu za kisharia ili kuilinda jamii kutokana na maovu. Miongoni mwa adhabu ambazo Uislamu umezipitisha ni ile ya mzinifu aliye katika ndoa kupigwa mawe hadi kufa.

Mwenyezi Mungu ameamuru hivyo ili kukomesha tabia hiyo chafu inayodunisha utu na hadhi ya ubinadamu. Mungu anatuambia:

“Wala msikaribie zinaa. Hakika (hiyo zinaa) ni uchafu na ni njia mbaya.” [Qur’an, 17:32].

Miongoni mwa madhara ya zinaa katika jamii ni kusambaratika kwa mfumo wa kifamilia na kuchanganyika kwa nasaba. Madhara ya zinaa yakiwemo ya kiafya na kifamilia yamechambuliwa kwa kina na wasomi, waandishi na watafiti wengi katika vitabu na machapisho mbalimbali.

Pili: Haki ya kutubu

Haki hii imeporwa kutoka mifumo mingine ya sheria isiyokuwa ya Kiislamu. Imethibiti katika mapokezi sahihi kuwa mwanamke mmoja alimwendea Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) akitaka ahukumiwe kupigwa mawe kutokana na kosa la uzinifu.

Mtume alipomuona aligeuza uso wake kwa kuwa jambo alilolifanya ni la siri, na anayepaswa kulijua ni mhusika mwenyewe na Allah ‘Azza Wajallah’. Hazikupita siku nyingi mwanamke yule alirejea kwa Mtume akitaka ahukumiwe kupigwa mawe ili ithibiti toba ya kweli juu yake. Mtume alipomuona aligeza uso wake kwa mara ya pili.

Kwa kutambua kuwa adhabu ya Allah siku ya Kiyama ni kubwa ukilinganisha na kupigwa mawe, mwanamke yule aliamua kurejea tena kwa Mtume akitaka ahukumiwe kupigwa mawe. Mtume alipomuona aligeuza uso wake kama alivyofanya mara ya kwanza na ya pili.

Aliporudi kwa mara ya nne, Mtume aligeuza tena uso wake kisha akamuuliza: “Wewe una wazimu, umekumbwa na pepo mbaya au umelewa?” Mwanamke yule akajibu: “Hapana ewe Mjumbe wa Allah! Mimi nina akili timamu.”

Mtume hakuwa tayari kumhukumu mwanamke yule wala kumsikiliza kwa sababu alitaka kujiridhisha kama kweli amefanya kosa au anadanganya. Lakini mwanamke yule alishikilia msimamo wake wa kutaka kupigwa mawe kutokana na kosa la kuzini. Hivyo Mtume akaamuru akamatwe na kupigwe mawe.

Mwanamke yule aliposikia agizo hilo, alijuta sana na baada ya sekunde chache alinyanyuka na kukimbia. Maswahaba (Allah awaridhie) walimkimbiza na walipomkamata walimpiga hadi kumuua. Mtume alipojulishwa juu ya tukio hilo alisema: “Kwanini hamkumuacha alete toba!” [Bukhari].

Katika zama za Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) wale waliofanya zinaa walijipeleka wenyewe mbele ya Mtume na baada ya kufanyika michakato ya kisharia, Mtume alitangaza hadd (adhabu) juu yao.

Watu wengi waliotenda kosa la zinaa walijisalimisha kwa Mtume ili kujiokoa na adhabu ya Allah Siku ya Kiyama. Uhai, mali na heshima za watu vinalindwa ili kuilinda jamii na uhalifu unaoweza kufanywa na watu waovu.

Tatu: Haki ya kuishi

Haki hii inajumuisha kulinda mwili na nafsi dhidi ya hatari za viumbe. Uislamu ambao ni mfumo kamili wa maisha ya mwanadamu unauzingatia uhai kama msingi muhimu katika ukuaji na ustawi wa mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla.

Kwa kuzingatia msingi huu, Uislamu unawataka wafuasi wake kuchunga na kulinda dini, nafsi, akili, heshima na mali za watu. Kuangamiza nafsi za watu wasio na hatia ni uhalifu mkubwa katika ulimwengu uliostaraabika. Allah anasema:

“Tuliwaandikia wana wa Israili ya kwamba aliyemuua mtu bila ya yeye kuua, au kufanya uharibifu katika nchi, basi ni kama amewaua watu wote. Na mwenye kumuokoa mtu na kifo ni kama amewaokoa watu wote….” [Qur’an, 5:32].

Kupitia aya hii tunajifunza kuwa haki ya kuishi inafungamana na jukumu la kutekeleza ibada na kusimamia sharia za Allah. Uislamu unatukataza kuangamiza au kuhujumu nafsi ambayo Allah ameharamisha kuiangamiza isipokuwa kwa makusudio ya kisharia kama vile kupigana Jihad, kulinda uhai au kukata kiungo kimoja kwa kuhofia maradhi kusambaa mwili mzima.

Allah anatuambia: “Enyi mlioamini, msiliane mali zenu kwa batili, isipokuwa iwe biashara kwa kuridhiana baina yenu. Wala msijiue (wala msiue wenzenu). Hakika Allah ni mwenye kukuhurumieni. Na atakayefanya haya kwa uadui na dhuluma, basi huyo tutamuingiza motoni, na hayo ni rahisi kwa Allah.” [Qur’an, 4:29–30]. Pia amesema: “… wala msijitie kwa mikono yenu katika maangamizo.” [Qur’an, 2:195].

Na katika hadith iliyosimuliwa na Abu Huraira (Allah amridhie), Mtume (rehema na amani ziwe juu yake) amesema:

“Yeyote atakayejirusha kutoka mlimani na kujiua atatupwa motoni akae humo milele, na atakayekunywa sumu na kujiua atatupwa motoni na atakunywa sumu hiyo milele, na atakayejiua kwa kipande cha chuma ataingizwa motoni akiwa na kipande hicho cha chuma na atajichoma nacho milele.” [Bukhari na Muslim].

Nne: Haki ya kuabudu

Haki ya kuabudu ni msingi muhimu miongoni mwa misingi ya dini ya Kiislamu kwa mujibu wa kauli yake Allah Aliyetukuka:

“Hapana kulazimisha katika Dini. Kwani Uongofu umekwishapambanuka dhidi ya upotofu. Basi anayemkataa shetani na akamuamini Allah bila ya shaka amekamata kishikio madhubuti, kisichovunjika. Na Allah ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.” [Qur’an, 2:256].

Na katika aya nyingine Allah anasema: “Je, wewe utawalazimisha watu kwa nguvu mpaka wawe Waumini?” [Qur’an, 10:99]. Haki ya kuabudu katika Uislamu inazingatiwa na kuheshimiwa kwa sababu inafungamana na tauhidi (Kumpwekesha Allah).

Uadilifu kama mhimili wa haki

Allah anayo majina mengi mazuri, na miongoni mwa hayo ni Al–Adli, yani Muadilifu. Kupitia jina lake hili (Al–Adli), Allah Aliyetukuka amewapa watu uhuru wa kuchagua dini na kufuata sheria ambayo wataridhika nayo kwani masuala ya itikadi yanafungamana na uelewa wa mtu mwenyewe na imani yake.

Mwenyezi Mungu anasema: “Na sema, ‘Hii ni kweli itokayo kwa Mola wako Mlezi. Basi atakayeamini. Na atakayekataa. Hakika Sisi tumewaandalia wenye kudhulumu moto ambao utawazunguka kama hema.” [Qur’an, 18:29].

Katika aya hiyo tukufu, Mwenyezi Mungu anamwambia Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie) kwamba hana mamlaka ya kuwalazimisha watu kuamini ujumbe wake kwani jukumu lake linaishia katika kuwalingania na kuwaita kwenye njia ya Mwenyezi Mungu.

Kama wanaolinganiwa watakubali, ni vema. Ama wakikataa, basi hakuna mamlaka ya kuwalazimisha kufuata Uislamu.

Ufafanuzi zaidi wa jambo hili unapatikana katika kauli ya Mwenyezi Mungu Aliyetukuka:

“Angelitaka Mola wako Mlezi wangeliamini wote waliomo katika ardhi.” [Qur’an, 10:99]; na katika kauli yake nyingine: “Basi kumbusha! Hakika wewe ni Mkumbushaji tu. Wewe si mwenye kuwatawalia.” [Qu’ran, 88:21–22].

Zaidi ya hayo, Mtume aliamrishwa katika Qur’an aachane na wale waliotangaza kukufuru. Amri hiyo imerudiwarudiwa mara kadhaa, ikiwemo katika Suratul Kaafirun.

Katika Sura hiyo, Mwenyezi Mungu anasema: “Sema: Enyi makafiri! Siabudu mnachokiabudu. Wala nyinyi hamuabudu ninayemuabudu. Wala Sitaabudu mnachoabudu. Wala nyinyi hamuabudu ninayemuabudu. Nyinyi mna dini yenu, nami nina Dini yangu.” [Qur’an, 109: 1–6].

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close