6. Kutoka Katika Quran na Sunnah

Miamala ya kifedha iliyoruhusiwa katika Uislamu

Uislamu ni dini iliyokamilika na muongozo kamili wa maisha ya mwanadamu. Mwenyezi Mungu, kupitia Qur’an na Sunna ametoa muongozo wa kisiasa, kijamii na hata kiuchumi juu ya namna ya kuishi duniani.

Kwa upande wa uchumi, kuna miamala ya kifedha ambayo Mwenyezi Mungu ameiridhia na ambayo ameiharamisha. Katika makala hii, tunataja miamala inayokubalika katika Uislamu.

Murabaha:

Huu ni muamala wa kiuchumi unaowapa wateja mbadala wa miamala ya mikopo ya riba. Katika murabaha,benki inakuwa ni mtu wa kati baina ya mwenye mali na mteja.

Benki itanunua bidhaa kutoka kwa mwenye mali na kuiuza kwa mteja kwa bei watakayokubaliana kwa mkataba maalumu. Hapa benki inaweza kuweka ada (tozo) wakati wa kusaini mkataba kama dhamana ya kuilinda benki pindi bei za vitu inavyoviuza zikiongezeka ghafla au mteja akiamua kuvunja mkataba.

Nyongeza itakayopatikana juu ya bei ya kununulia vitu hivyo haitahesabiwa kuwa riba bali ni gharama za huduma ya benki kwa mteja.

Mudharaba

Katika muamala huu wa pili, wajasiriamali hushirikiana na wawekezaji ili mipango ya kibiashara itekelezeke kwa ufanisi. Wawekezaji hubeba jukumu la kutoa mtaji na wajasiriamali watatoa nguvu kazi na mazingira ya kufanyia kazi. Ikiwa biashara itafanikiwa, faida itagawanywa kufuatana na makubaliano ya asilimia zilizowekwa kati ya wawekezaji, wajasiriamali na waliotoa nguvukazi.

Sukuk

Muamala huu hujulikana kama uwekaji bondi wa Kiislamu bila ya kuwa na mfumo wa deni ambao hutumika katika bondi ya kawaida.

Muamala huu hutumika katika miradi mikubwa kama vile mradi wa upanuzi wa kiwanja cha ndege, ambapo rasilimali kubwa huhitajika. Kwa kutumia muamala huu, fedha za mradi hukusanywa kutoka kwa watu mbalimbali kisha pesa hizo huundiwa kampuni itakayosimamia mradi wenyewe. Waliotoa pesa (yaani wawekezaji) watasaini mkataba na kampuni hiyo na faida itakayopatikana itagawiwa kwa wawekezaji na kampuni ile kwa viwango vya asilimia vilivyowekwa.

Mfumo kama huu hutumiwa sana na Jumuiya ya Umoja wa Nchi za Kiislamu (OIC) ambapo husaidia kujenga mradi fulani kisha hugawana faida na serikali husika.

Tofauti yake na misaada inayotoka katika nchi nyingine za kimagharibi ni kuwa, hawakupi pesa kukukopesha ili uje uwalipe zaidi, yaani pamoja na riba.

Misingi ya uchumi wa Kiislamu

 1. Kila mtu apewe fursa sawa
 2. Njia za uchumi zisihodhiwe na watu wachache katika jamii
 3. Mali isiwe ya wachache bali isambazwe katika jamii ili kuleta manufaa na kuondoa umaskini. Hii ni ili kuepuka matajiri kuhodhi uchumi.
 4. Kila mwenye uwezo wa kufanya kazi afanye. Uislamu unapiga vita uvivu. Uislamu vile vile hauruhusu kuombaomba.

Njia za uchumi zilizoharamishwa na Uislamu

 • Riba: Hiki ni kiwango cha ziada ambacho mdai analipwa au kupokea kutokana na mkopo alioutoa kwa mdaiwa.
 • Ulevi: Pombe zote ziwe za kiwandani au kienyeji pamoja na bangi, shisha, madawa ya kulevya na mirungi.
 • Nyamafu: Mnyama aliyekufa bila kuchinjwa yaani kibudu isipokuwa samaki. Vievile biashara ya nguruwe. Katika kundi hili pia kuna vinyago, sanamu na kuchora picha za viumbe hai.
 • Dhuluma: Wizi, unyang’anyi, rushwa, utapeli na udanganyifu (uchumi wa dhuluma haukubaliki kabisa).
 • Kamari na aina zake zote – ikiwemo bahati nasibu
 • Mapato yatokanayo na ushirikina
 • Mapato yatokanayo na uzinzi
 • Kupiga ramli na aina zake zote
 • Mapato ya biashara zote haramu
Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close