6. Kutoka Katika Quran na Sunnah

Mgawanyo wa maudhui ya Qur’an

Ubora wa umma huu ukitofautisha na umma zilizopita unaelezewa katika Qur’an: “Nyinyi mmekuwa bora ya umma waliotolewa watu, kwa kuwa mnaamrisha mema na mnakataza maovu, na mna muamini Mwenyezi Mungu…. [Qur’an, 3:110]

Historia inatuonesha kuwa, Mtume wa Allah pamoja na wale waliomfuata baada yake walilazimiana na kazi ya ulinganiaji mpaka mwisho wa maisha yao; hivyo tuachane na nadharia kuwa kazi hii ni ya watu fulani tu. Tukumbuke maneno ya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie): “Kila mtu ni mchunga na ataulizwa juu ya kile alichokichunga.” [Bukhari na Muslim]. Kila mtu, katika nafasi aliyo nayo,katika aidha ngazi ya familia,jamii, taifa na kuendelea, ataulizwa.

Na katika Hadithi nyingine: “Nifikishie mimi walau Aya moja.” [Bukhari]. Ndani ya Hadithi hii, yanapatikana mambo matatu ya kuzingatia, kwanza, amri kutoka kwa Mtume wa Allah akituachia jukumu la kufikisha da’wa kwa chochote mtu alichojifunza katika dini. Pili, Utukufu (tashrif), yaani unafikisha kutoka kwa Mtume wa Allah. Huo ni uzuri ulioje? Na tatu, takhfif, yaani tukapunguziwa, hata ikiwa ni Aya, Hadithi au jambo moja katika sira na mfano wa hayo.

Mamabo haya yote yanafungamana na himizo la kuwa na mwenendo na kauli nzuri katika kuyaendea mambo. Allah anasema: “Na ni nani mbora wa kusema kuliko aitaye kwa Mwenyezi Mungu na akatenda mema, na akasema,‘Hakika mimi ni katika Waislamu?’ [Qur’an, 41:33].

Siku zote, ili ufanisi upatikane katika kazi,yapaswa kuwa na vitendea kazi, ambavyo katika muktadha huu ni Qur’an na Sunna. Tuungane pamoja ndani ya makala hii kuangalia mtazamo wa ujumla wa Qur’an.

Qur’an ni nini?
Qur’an ni maneno ya Allah aliyoshushiwa Mtume kupitia Jibriil (amani ya Allah imshukie) ikikusudiwa kuwa ukumbusho kwa umma huu. Allah anasema: “Na hakika haya ni ukumbusho kwako na kwa kaumu yako. Na mtakuja ulizwa.” [43:44].

Wanawachuoni wamegawanya mtazamo wa jumla katika Qur’an, kuna baadhi wameigawanya sehemu tatu na wengine nne. Hebu tuone mgawanyo huo.

Tauhid (Aqida).
Tauhidi ninamna ya kumpwekesha Allah katika ulezi, majina, sifa zake, na vilevile ibada ili kuepuka kumuabudu asiye Allah. Na hii hasa ndiyo sababu ya kutumwa Mitume. Na kinyume cha Tauhid ni shirki. Kadhalika inaingia ndani ya Tauhid imani juu ya Allah na vyote alivyoviumba, tunavyoviona na tusivyoviona.Mifano ya hili ipo mingi katika Qur’an. Mwenyezi Mungu Aliyetukuka anasema: “Na kwa hakika, kwa kila umma tuliutumia Mtume kwamba,‘Muabuduni Mwenyezi Mungu, na muepukeni Shetani.’” [Quran, 16:36].

Akhlaaq na Muamalaat.
Sehemu kubwa ya maisha ni namna tunavyoamiliana na watu katika nyanja tofauti. Katika Hadithi aliyoipokea Tirmidhiy, Mtume wa Allah amefunganisha kumcha Allah na tabia njema, kukaa na watu kwa wema na kujitahidi kufanya mema kwani mema yanafuta yale maovu. Wasifu mzuri ndani ya Qur’an ni uliotajwa kumhusu Mtume wa Allah: “Na hakika wewe una tabia tukufu.” [68:4]. Tabia na muamala mzuri wa Mtume uliwavutia washikirina na kupelekea kusilimu; hivyo nasi tujipambe na tabia njema ili mambo yaende sawa.

Visa (Qasas)
Qasas, ama visa, vimechukua takriban theluthi nzima ya Qur’an ikiwa pia imekusanya mambo mawili yaliyopita. Visa hivyo vinajumuisha vya Mitume na Manabii na pia visivyokuwa vyao. Tufahamu ya kuwa, visa hivi ni uhakika na uthibitisho wa matukio yaliyotokea zama zilizopita na inatosha jambo hili kuliita ‘ghaibu’ kwani Allah anasema: “Hizi ni katika habari za ghaibu tunazokufunulia. Hukuwa ukizijua wewe, wala watu wako, kabla ya hii. Basi subiri! Hakika Mwisho ni wa wachamungu.” [Qur’an, 11:49].

Asili ya neno ‘qasas’ limetokana na neno ‘qaswa’ lenye maana mfatilizo au mfululizo wa athari ya kitu fulani. Allah anasema: “Naye akamwambia dada yake Musa, ‘Mfuatie. Basi naye akawa anamuangalia kwa mbali bila ya wao kujua.” [Quran, 28:11]. Vipi tutatafautisha visa hivi na vile vya kutungwa na watu?Tofauti ipo katika irabu ya neno. Visa hivi vilivyotungwa vinaitwa ‘qaswas’, tofauti na lile neno la kwanza. Hivyo maneno haya ni tofauti.

Visa vizuri
Allah anatukhabarisha wasifu na uzuri wa visa hivi pale aliposema: “Sisi tunasimulia simulizi nzuri kwa kukufunulia Qur’an hii. Na ijapo kuwa kabla ya haya ulikuwa miongoni mwa wasiyojua.” [Qur’an, 12:3]. Wasifu na uzuri huu unaelezeka kwa mambo kadhaa. Kwanza, lugha, inayotumika ya Kiarabu ni yenye kufahamika na balagha ya hali ya juu kabisa. Pili, maudhui, katika visa hivyo ni ya kipekee. Tatu, mazingatio na mafunzo yanayopatikana ndani ya visa hivyo ili tupate mifano halisi kama ilivyopata kutokea zama zilizopita. Lengo ni kwamba, mafunzo hayo yatusaidie katika zama zetu za sasa, tusirejee makosa ya wenzetu na tuige mazuri.

Hekima na faida ya visa
Usimulizi wa visa hivi una hekima na faida ndani yake na siyo kusoma na kutuacha bila ya mazingatio. Tutazame faida chache za kusoma simulizi hizi zilizomo ndani ya Qur’an. Faida mojawapo ni kutufanya tuwe wenye kutafakari vizuri. Tafakuri za watu zinatofautiana; baadhi hutafakari mazuri na wengine mabaya.

Tufahamu ya kuwa, wapo viumbe waliishi kabla yetu, waliokuwa kama sisi na sisi tutakuwa kama wao,walipitia misukosuko na furaha katika mambo kadhaa. Hivyo basi, yafaa tutafakari na kuchukua hatua kwa yale waliyoyafanya ili tujifunze au tuyaache. Allah anasema: “…. Basi simulia hadithi, huenda wakatafakari.” [Quran, 7:176].

Suala zima la kutafakari linaenda sambamba na hekima ya pili ambayo ni kuzingatia. Baada ya kutafakari kwa kina na kujifunza wapi wenzetu walipatia na wapi walikosea au kitu gani kilipelekea kuangamizwa umma zilizopita, ndipo mazingatio yanapatikana. Mazingatio yamebeba mawaidha yanamsaidia mtu kubadilika kutoka hali moja kwenda hali nyingine. Allah anasema: “Kwa hakika katika Hadithi zao yamo mazingatio kwa wenye akili. Si maneno yaliyozuliwa, bali ni ya kusadikisha yaliyo kabla yake, na ufafanuzi wa kila kitu, na ni uongofu na rehema kwa kaumu yenye kuamini.” [Qur’an, 12:111].

Faida ya tatu ni kuwa na msimamo thabiti katika haki kwa sababu usomaji wa visa hivi unatupa picha halisi ya hali katika da’wa ilivyokuwa na hivyo mazingatio yanayopatikana yanatupa uthabiti na msimamo (istiqamah) katika dini. Watu wanaofanya kazi ya da’wa wanapaswa kuchukua na kuiga mifano hii kwani wanakumbana na maudhi mengi; na kuwa wanahitaji msimamo imara ili wasitetereke.Allah anasema: “Na yote tunayokusimulia katika habari za Mitume ni ya kukupa nguvu moyo wako. Na katika haya imekujia haki na mawaidha na ukumbusho kwa Waumini.” [Qur’an, 11:120].

Nimalize kwa kusema, hakika ni mengi ya kujifunza katika visa hivi, hivyo tunamuomba Allah atujaalie kujifunza juu ya visa hivi vyenye kuakisi maisha yetu

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close