6. Kutoka Katika Quran na Sunnah

Madhara ya chumo la haramu

Amru bin Asw (Allah amridhie) amehadithia kwamba, Mtume (rehema na amani ya Allah zimshukie) alimtumia ujumbe akimtaka achukue nguo zake pamoja na silaha kisha amfuate (aende nyumbani kwa Mtume). Amru alifika nyumbani kwa Mtume akiwa ametawadha, Mtume akamtazama kisha akainamisha kichwa chake chini akasema: “Ewe Amru! Nataka kutuma jeshi nawe uwe kiongozi wa jeshi hilo. Nakuombea kwa Allah akupe ngawira nyingi (ushinde vita) kisha uje kwangu nikupe mgao wa ngawira.” Amru akamwambia Mtume: “Mimi sikusilimu kwa sababu ya kutaka mali bali nimependezwa na dini ya Uislamu na napenda niwe pamoja na Mjumbe wa Allah.” Mtume akasema: “Ewe Amru! Mali bora ni ile anayoimiliki mtu mwema.” [Bukhari/ Adabul–Mufrad].

Mafunzo ya tukio hili:

Allah ‘Azza Wajallah’ amewaumba wanadamu na kuwafanya wapende mali zaidi kwa kuwa ndiyo mhimili wa maisha yao hapa duniani. Kwa hali hiyo, ni wajibu kwa Muislamu kutafuta mali kwa njia anayoiridhia Allah. Mwanadamu anawajibika kutafuta mali ili kuepukana na udhalili wa kuombaomba na kukodolea macho mali za watu.

Kutafuta mali ya halali ni jambo la wajibu kwa kila Muislamu. Allah humuondoshea madhila muumini mwenye kutafuta mali kwa njia ya halali na kumuwezesha kutoa zaka, sadaka na kuwahudumia watu hasa wenye mahitaji wakiwamo yatima na wajane.

Mtume (rehema za Allah na amani imshukie) alikuwa akiwausia Maswahaba zake (Allah awaridhie) kufanya kazi kwa bidii ili kuiimarisha dunia yao sambamba na kuipigania dini ya Mwenyezi Mungu kwa mali zao na nafsi zao. Kwa nyakati mbalimbali katika mji wa Madina, Mtume na Maswahaba zake walikuwa wakigawana ngawira (mali zilizopatikana kwenye vita vya Jihad) na kuzitumia katika mambo mengine ya kheri.

Mali bora ni ile inayotokana na chumo halali

Moja ya sababu ya kukubaliwa kwa matendo yako mema ni kula riziki ya halali. Kwa hiyo, unapaswa kuitakasa nafsi yako kutokana na chumo la haramu kwa sababu Mwenyezi Mungu amekataza kuchuma mali kwa njia ya riba, unyang’anyi, uongo, kula rushwa, kudhulumu na kadhalika. Licha ya katazo hilo, wapo baadhi ya ndugu zetu Waislamu ambao hutafuta mali (fedha) kwa njia za haramu ili wapate utajiri wa haraka.

Madhara ya chumo la haramu

Chumo la haramu lina athari mbaya kwa mhusika na jamii nzima. Miongoni mwa athari hizo ni; mosi, kukosekana baraka na kuzidi ukame katika ardhi; pili, kukithiri kwa magonjwa mbalimbali; tatu, kuenea machafu katika ardhi na nne dua kutojibiwa.

Kwa kuchelea hayo, Uislamu umeamrisha watu kufanya kazi ya halali na umekemea tabia ya uvivu, uzembe na kuombaomba. Qur’an Tukufu na Hadith za Mtume zimeweka wazi umuhimu na fadhila za kuchuma mali ya halali na kuwatahadharisha watu juu ya chumo la haramu.

Mtu anayekula mali za haramu, kamwe hawezi kupata radhi za Allah na baraka zake. Vilevile, umma hauwezi kufanikiwa ikiwa watu wake wanakula mali za haramu. Wanadamu tutambue kuwa tutaulizwa na Allah siku ya Kiyama juu ya mali tulizozichuma hapa duniani. Je, tulizichuma kwa njia ya halali au ya haramu? Anayetambua hilo aandae majibu.

Allah hajibu dua ya mtu anayekula haramu

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Hakika Allah ni mzuri na hakubali ila mazuri. Na hakika Allah amewaamrisha Waislamu yale aliyowaamrisha Mitume pale alipowaambia: ‘Enyi Mitume! Kuleni vizuri na fanyeni mema.’ [Qur’an, 23:51].

Akasema tena Mwenyezi Mungu: ‘Enyi mlioamini! Kuleni vizuri tulivyowaruzuku na mumshukuru Mwenyezi Mungu ikiwa kweli mna muabudu yeye tu.” [Qur’an , 2:172].

Kisha Mtume akatoa mfano wa mtu anayesafiri safari ndefu hali akiwa amechoka, nywele zake zimejaa vumbi, anainua mikono yake na kuomba:

“Ewe Mola wangu, ewe Mola wangu ilihali chakula chake ni cha haramu na kinywaji chake ni cha haramu, na mavazi yake ni haramu na amel- ishwa vya haramu. Vipi mtu huyu atajibiwa dua yake.” [Muslim].

Hadith hii Tukufu inaonesha kuwa, chumo la haramu ni kizuizi kikubwa cha kukubaliwa dua. Na kama tujuavyo, ibada anazofanya mja kwa lengo la kujikurubisha kwa Allah ni sehemu ya dua.

Kwa muktadha huo, ni wazi kuwa amali yoyote atakayoifanya mtu anayechuma mali kwa njia za haramu haiwezi kukubaliwa. Zaidi ya hivyo, chumo la haramu huufanya moyo kuwa mgumu, hivyo kupelekea viungo vingine kufanya maovu mengi.

Wapo baadhi ya watu wanaochuma mali kwa njia ya haramu na kwenda kuitoa sadaka wakiamini kuwa kufanya hivyo kunasafisha mali na kuifanya kuwa halali.

Lakini Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) amesema: “Mwenye kutoa sadaka kiasi cha tende moja katika chumo la halali, Allah hapokei ila vilivyo vizuri. Hakika Allah anazikubali sadaka na anazipokea kwa mkono wake wa kuume na anazilea kama mmoja wenu anavyomlea ndama wake, mpaka tonge (anayoitoa sadaka) inafikia ukubwa wa jabali Uhud.” [Bukhari na Muslim].

Allah ‘Azza Wajallah’ ameitenganisha haki na batili kwa kuwa viwili hivyo haviwezi kukaa sehemu moja. Anasema Mwenyezi Mungu:

“Haviwi sawa viovu na vyema japokuwa wingi wa viovu vitakupendeza. Basi mcheni Allah enyi wenye akili ili mpate kufanikiwa.” [Qur’an, 5:100].

Matendo ya mtu hayatakasiki isipokuwa kwa kula, kunywa na kuvaa mavazi ya halali, ndiyo maana Maswahaba (Allah awaridhie) walijitenga na vitu/ mambo ya haramu.

Mama wa waumini, Aisha (Allah amridhie) amesema, siku moja Abubakr (Allah amridhie) aliletewa kitu na mfanyakazi wake kisha akakila. Baada ya kula, yule mfanyakazi akamuuliza:

“Je, wajua nimekipata wapi (hicho ulichokula?) Abubakr akajibu: “Sijui.” Yule mfanyakazi akasema: “Nilimtabiria mtu siku za jahiliya (zama za ujinga), nikamfanyia uganga. Kisha akanipa hicho kitu ulicho kula kama zawadi.” Baada ya kusikia hivyo, Abubakr akaingiza mkono wake mdomoni akajitapisha vitu vyote vilivyokuwa tumboni, [Bukhari].

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close