6. Kutoka Katika Quran na Sunnah

Maajabu ya Bismillah

Bismillah’ ni kalima (tamko) maarufu kwa kila Muislamu. Ni tamko la ufunguo ambalo hutumika kabla ya kuanza kufanya jambo lolote. ‘Bismillah’ ni neno la ajabu kwa kuwa limepenya na kutumika katika maeneo mengi sana.

Jambo la kushangaza na pengine la kufurahisha ni kuwa, wapo Waislamu wengi ambao wameutupa mbali Uislamu wao, lakini, utawasikia kabla ya kula, au kuanza safari kwa kipando au kufanya kitu kingine chochote, wanakumbuka kusema Bismillah.

Kwangu mimi naona haya ni maajabu yenye kuleta tafakuri kubwa. Kwanza, ni bishara kuwa, pamoja na kutoutekeleza Uislamu kwa asilimia 100 bado katika nyoyo zao wanazo chembe za imani. Huenda wakilinganiwa, na iwapo Allah akitia Taufiq, watarejea katika mstari.

Pia, kuanza kufanya mambo yao kwa Bismillah, pamoja na kuitupa imani yao kwa kiasi fulani, inaonesha wanamtegemea Allah katika mambo yao. Kumtaja Allah wanapoanza mambo yao ni kumuomba awape kinga na hifadhi.

Muhimu zaidi ni kuwa, mwanadamu kwa namna yoyote ile ni kiumbe tegemezi. Pia, ni wazi kuwa, utegemezi wa mwanadamu kwa Allah upo wakati wote, na ndiyo maana hata anapoamua kujitenga na dini yake upo wakati asili inamlazimu kumhimidi na kumuomba Allah ampe kinga na msaada.

Kwa Masheikh na walinganiaji wote, tumieni maajabu ya Bismillah kuwazindua Waislamu. Tumieni fursa ya kuwepo chembe za Imani katika mioyo ya vijana kuwarudisha misikitini.

Hawa watu bado wana imani na wanamtegemea Allah katika mambo yao hata kama hawafiki misikitini.
Kwa kusema hivi simaanishi kuwa nakubaliana na hali ilivyo ya watu kuitelekeza dini, laa hasha! Dini inapaswa kutunzwa na haipaswi kuchezewa hata kidogo.

Bali ninachosema hapa ni kuwa, lipo kundi kubwa, hasa la vijana, limeiacha misikiti, na kupitia maajabu ya Bismillah bado tuna fursa ya kufufua na kuziimarisha imani zao kwa manufaa ya dini yetu na jamii kwa jumla.

Tags
Show More

Related Articles

Back to top button
Close