6. Kutoka Katika Quran na Sunnah

Kutabasamu: Sunna iliyosahaulika!

Ndugu yetu mmoja alikwenda kumuona Sheikh kwa nia ya kumshutumu kwa sababu ya mitazamo yake. Akiwa amejawa na hasira, alimkemea vikali yule Sheikh, lakini ghafla alitulia na kuanza kutabasamu. Kitu gani hasa alichofanya Sheikh mpaka yule bwana aliyekuwa akimfokea vikali akaacha kufoka na kutabasamu? Sheikh yule alimpa tabasamu tu.

Tabasamu ni nyenzo yenye ufanisi mkubwa katika kulingania, kuondoa uhasama na kujenga udugu. Kwa bahati mbaya sana, neno Sunna linahusishwa na mavazi, kufuga ndevu, vyakula na kadhalika, lakini siyo vipengele vya kitabia kama kutabasamu.

Tabasamu huleta watu karibu

Kila Anas (Allah amridhie) alipomuona Mtume (rehema za Allah za amani zimshukie), uso wake mtukufu ulikuwa muangavu kama mwezi, na kila Mtume alipomuangalia Anas, alitabasamu. Kila walipokaribiana alikutana na tabasamu zito lililosababisha moyo wa Swahaba huyu mkubwa kuathiriwa kwa kiasi kikubwa kiasi kwamba alihisi yeye ndiye anayependwa zaidi na Mtume.

Swahaba huyu alitaka kuthibitisha hisia yake hii, hivyo akamuuliza Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) ni nani anayempenda zaidi miongoni mwa Maswahaba zake? Mtume alijibu: “Abubakr.”

 Akidhani kwamba yeye ndiye anayependwa zaidi na Mtume baada ya Abubakr (Allah amridhie), Anas alirudia tena swali lile, na kwa mshangao mkubwa, hakuwa yeye bali Umar (Allah amridhie)! Kutokana na kitendo hiki kidogo tu, Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie), aliweza kumfanya Anas (Allah amridhie) adhani kwamba yeye ndiye anayempenda zaidi.

Ilikuwa ni vitendo hivi vidogo lakini vyenye athari kubwa na visivyohitaji nguvu, ndivyo vilivyomfanya Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) awe kipenzi cha watu wote wakati wa zama zake. Abdullah bin Harith (Allah amridhie) amesema:

“Sijapata kumuona mtu yeyote aliyetabasamu zaidi kuliko Mtume wa Mwenyezi Mungu (rehema za Allah na amani zimshukie).” (Shamaíil Tirmidhi).

Tabasamu ni sadaka

Katika utafiti uliofanywa na Wamarekani wawili, iligundulika kuwa binadamu hawezi kuishi bila tabasamu. Katika jaribio lao hilo la kisayansi Wamarekani waliwaambia washiriki wasitabasamu kwa siku tatu, jambo ambalo hawakuweza kulifanya. Kutabasamu ni matokeo ya hisia ya ndani na vile vile ni njia ya kuonyesha mtu huyu anajisikiaje.

Mtu anapojawa na furaha au kuridhika, hutabasamu. Pia, mtu anapogeuka pembeni na kuwaona wenzake, anatabasamu zaidi ili kuwashirikisha katika furaha yake.

Hata hivyo, sababu za Kiislamu za kutabasamu zinazidi hapo. Kutabasamu siyo tu ni upole, lakini pia ni kuonyesha mapenzi na upendo – ambapo vyote hivyo vimekusanywa katika hadithi hii.

“Kutabasamu mbele ya ndugu yako ni sadaka.” [Tirmidhi].

Mtu anaweza kuuliza, ikiwa msingi wa sadaka ni kutoa, je kutabasamu kunahusika vipi na sadaka? Unapotabasamu unatoa baadhi ya tabia zako njema au ukarimu kwa mtu mwingine.

Maana finyu ya sadaka inatokana na tabia ya kugawanya watu katika kundi la matajiri ambao wanaweza kutoa na maskini yaani wale wanaopokea. Kutabasamu ni sadaka isiyokomea kwenye utajiri, daraja, au hadhi. Kutabasamu hakuna gharama na kunaweza kufanywa na mtu yeyote.

Huu ni mfano hai kwamba sadaka ni utambulisho wa yale yote ambayo ni mema. Isitoshe, sadaka inawaleta watu pamoja na matokeo na kuimarisha mshikamano wa jamii. Hii inang’arisha nyoyo za roho zilizofungwa. Athari za tabasamu zinapenya kwa kina sana ndani ya hisia za mtu, na kulazimisha wengine kufanya kitendo hiki cha kutabasamu na hivyo tabasamu inaambukiza. Tabasamu ni lugha ya ulimwengu ambayo inawakusanya pamoja watu wote.

Tabasamu inasaidia kubadili mtazamo

Tabasamu ina athari kubwa katika mazingira ya mtu. Kwa hiyo, wakati mambo yanapokuwa hayaendi sawa, tunapaswa kujaribu kutabasamu badala ya kuruhusu shida inayotukabili kutuchanganya. Tukifanya hivi tutakuwa tumeonresha kuridhika zaidi na Qadari ya Mwenyezi Mungu.

Halikadhalika, tabasamu ina athari kubwa katika mtazamo wako kwa sababu inakufanya uyashughulikie mambo kwa utulivu zaidi na bila ya kuwa na msongo (stress). Si hivyo tu, tabaamu inazalisha hisia chanya ambazo zinaruhusu mtazamo wa mtu kubadilika ndani ya muda mfupi tu.

Kutabasamu siyo tu kunasaidia kubadilisha mtazamo wako, bali pia mtazamo wa watu wengine, kama inavyoakisiwa katika kisa cha yule ndugu yetu aliyekasirika na sheikh anayetabasamu tulichokitaja awali.

Pia, Malik El-Shabbaz, ambaye anajulikana kama Malcolm X ametaja tukio moja la kuvutia ambapo alisema iwapo mtu atakutana na mtu aliyekasirika sana, na yeye akampa tabasamu tu, baada ya makabiliano machache, bila ya kujali kiasi cha hasira aliyokuwa nayo, hatimaye na yeye atatabasamu tu.

Hiyo ndiyo sunna ya kutabasamu ambayo kwa bahati mbaya sana haitekelezwi miongoni mwa Waislamu wengi leo. Uhalisia wa leo ni kwamba ukimuona mtu anatabasamu, basi aghlabu atakuwa anataka kitu. Kwa kuifanya tabasamu kuwa tabia, tutaona mabadiliko katika tabia za watu wanaotuzunguka. Hata hivyo, huku kutabasamu hakupaswi kufanywa tu kwa jinsia tofauti, kwa sababu kitendo hiki, ambacho ni aina ya sadaka kinabadilika na kuwa ukosefu wa maadili.

Kwa kitendo kidogo tu cha hisani kama kutabasamu, tunaweza kuichangamsha siku ya mtu. Kuna hadith ngapi tulizosikia ambazo Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alitabasamu mpaka meno yake yote yaliweza kuonekana? Matukio kama hayo tunayoyasoma katika vitabu vya hadith yanapaswa kutuhimiza nasi kutabasamu. Waislamu tunahitaji kutabasamu hata tukiwa katika hali ngumu kiasi gani au huzuni.

Tabasamu ni dhihirisho la upendo na udugu, na moja ya masharti ya kuingia Peponi. Tabasamu itatupa mtazamo chanya wa maisha, mtazamo wa kuyafurahia maisha. Kwa nini iwe mtu wakati wote umekunja ndita utadhani nyati!

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alikaripiwa na Mwenyezi Mungu Aliyetukuka kwa kukunja uso katika Sura ya Abasa. Mtume alifanya kitendo hicho kwa Ibn Umm Maktum ambaye alikuwa kipofu. Hakumwambia Ibn Umm Maktum aje baadae wala hakumwambia neno lolote baya, isipokuwa Mtume alikaripiwa alishughulishwa zaidi na kuzungumza na wakuu wa Makuraish.

Ajabu ni kuwa, Mtume alifanya kitendo ambacho hata Ibn Umm Maktum mwenyewe hakuweza kukiona, lakini Allah ‘Azza wa Jalla’, Mjuzi wa kila kitu, aliona kitendo hicho na akamkaripia Mtume. Kama Mwenyezi Mungu amekirekodi kitendo hiki kidogo ndani ya Qur’an mpaka ambamo kitadumu hadi Siku ya Kiyama, basi kwa hakika tunapaswa kujitahidi kuwapa tabasamu kaka zetu na dada zetu.

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close