6. Kutoka Katika Quran na Sunnah

Kirusi cha corona – kupitia lenzi ya Qur’an!

Qur’an ni kitabu kilichofunuliwa kwetu na Muumba wetu ili kutuongoza wanadamu katika kile kilicho sawa na bora kwetu. Qur’an inatufundisha kutofautisha kati ya mema na maovu, kumtegemea na kumuabudu Mwenyezi Mungu peke yake, na kuyaangalia maisha yetu ya duniani kama maandalizi tu ya maisha ya milele Akhera.

Allah ‘Azza wa Jalla’ ameweka misemo na mifano mingi ndani ya Qur’an Tukufu kwa ajili yetu kutafakari na kuakisi. Misemo na mifano hii mara nyingi imeletwa kwetu kwa ajili ya kulinganisha hali moja na nyingine. Mwenyezi Mungu Mtukufu anawasilisha aya nyingi ndani ya Qur’an kwa utaratibu huu ili kuleta uwazi na ufahamu wa ndani, wakati anapofafanua mambo kwa wanadamu.

Aya hizi zinataka akili za wanadamu kuzihoji na kuzihamasisha ili kuzielewa kikamilifu na kutafakari ujumbe wa Mwenyezi Mungu uliobebwa na aya hizo. Ndani ya Qur’an, Allah ‘Azza wa Jalla’ anasema:

“Hakika mfano wa maisha ya dunia ni kama maji tuliyoyateremsha kutoka mbinguni, kisha yakachanganyika na mimea ya ardhi wanayoila watu na wanyama. Mpaka ardhi ilipokamilika uzuri wake, na ikapambika, na wenyewe wakadhani wameshaiweza, iliifikia amri yetu usiku au mchana, tukaifan ya kama iliyofyekwa – kama kwamba haikuwapo jana. Namna hivi tunazipambanua Ishara zetu kwa watu wanaofikiri.” [Qur’an,10:24].

Katika aya hii nzuri, Allah ‘Azza wa Jalla’ analeta mfano wa ardhi iliyonyeshewa mvua ambayo ikapelekea mimea kuchipua na kufikia ukamilifu na kupendeza machoni mwa anayeiangalia. Wale wanaoidhibiti bustani hii wanafurahishwa mno kiasi kwamba wanadanganyika na kudhani kuwa wana mamlaka kamili na umiliki usio shaka wa bustani hii.

Kisha amri ya Mwenyezi Mungu inashuka kwenye bustani hii na ghafla janga linakuja. Katika muda ambao ameuchagua Yeye Mwenyezi Mungu, akaigeuza ardhi hii ambayo awali ilikuwa nzuri na kuwa kame kabisa – kama vile hakuna kitu kilichomea kabla ya uharibifu huu.

Mfano huu unalinganishwa na maisha yetu ya duniani, maisha ambayo yanapendeza mbele ya macho ya mtazamaji, yakishangaza na kung’aa kwa mapambo yake na kuwafanya wanadamu wayapende sana na kuyatamani.

Lakini hamu hii inapelekea kwenye kudanganywa, ambapo mwanadamu anafikia hatua ya kudhani anayamiliki maisha haya na ana utawala huria juu yake. Ghafla, hata hivyo, ananyang’anywa ulimwengu huu wakati akiuhitaji zaidi. Hapo, kizuizi kinawekwa baina yake na ulimwengu ambao anautamani mno.

Uzuri wa Qur’an ni kwamba, msemo/mifano kama huu na mingine, inaweza kutumika kwenye dhiki na majaribu mengi ambayo Waislamu wamepitia katika kipindi cha miaka 1441 tangu kufunuliwa kwa Kitabu hiki kitukufu. Kwa hakika ni kitabu cha muongozo kisichopitwa na wakati na kinachohamasisha.

Dunia na janga la corona

Dunia imetekwa na adui asiyeonekana, akimuathiri tajiri na masikini, vijana na wazee, weupe na weusi. Amejichimbia mbele kabisa ya akili zetu. COVID-19 imechukua maisha ya maelfu ya watu. Imeporomosha uchumi wa nchi nyingi, imesitisha ghafla utalii wa dunia, na imeacha maelfu ya watu bila kazi na wakihangaika kifedha.

Huo ndiyo udhaifu wa ulimwengu ambao tunaung’ang’ania sana na kuupenda. Adui ambaye amekuwepo kwa takriban miezi minne tu, ameipigisha magoti mifumo mikubwa ya ulimwengu iliyodhaniwa kuwa isingeweza kuharibika.

Wamekuwa wanyenyekevu mno kwa kirusi hiki wale ambao wamekuwa wakitenda dhambi na kupuuza maisha ya Akhera, ambao wamekuwa hawajali kiasi cha kuhisi kwamba janga lile halitawapiga.

Kama vile wamiliki wa ardhi waliotajwa kwenye aya ya Qur’an hapo juu, amri ya Mwenyezi Mungu imekuja na hakika bustani ambayo awali ilikuwa ikistawi; kufumba na kufumbua, imesambaratika kiasi cha kushindwa hata kutambuliwa!

Mlinganisho huo wa kusikitisha unatupa mtazamo ambao tunapaswa kuutumia kuuangalia huu mtihani uliotukabili sasa, maradhi ya corona. Huu ulimwengu ni wa muda mfupi. Kwa asili, umaarufu, uzuri, na utajiri ulimwengu ni mambo ya muda mfupi na yanaweza kuchukuliwa kutoka mikononi mwetu – kufumba na kufumbua tu. Wiki chache zilizopita zimetufundisha somo hili kwa uwazi kabisa. Kuiambatanisha mioyo yetu kwa dunia ni kosa lililowazi kabisa kwa kuwa huu ulimwengu kwa asili yake huwa unakabiliwa na majanga yakiwemo vita, mlipuko wa magonjwa, matetemeko ya ardhi. Kwa hivyo, ulimwengu huu utaendelea kuwa dhaifu na ulio hatarini kwa muda wote utakapokuwepo (mpaka Kiyama).

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close