6. Kutoka Katika Quran na Sunnah

Kinga dhidi ya corona ilishatajwa katika uislamu

Mwenyezi Mungu anasema katika Qur’an: “Tutawaonesha (ukweli) wa ishara zetu katika nchi za mbali na katika nafsi zao wenyewe mpaka iwathibitikie kwamba haya ni kweli. Je haitoshi kwa Mola wako yeye kuwa ni Mjuzi wa kila kitu? Jueni kwamba wao, wako katika shaka (tu) juu ya kukutana na Mola wao. Jueni kwamba hakika yeye (Mola wako) amekizunguka kila kitu.” [Qur’an, 41:53-54].

Mara kwa mara, kumekuwa na matukio makubwa ambayo hudhihirishia ulimwengu ukweli wa dini ya Kiislamu; na laiti isingekuwa ukaidi na ubishi wa binadamu, kwa ishara hizo wangepaswa kusilimu.

Hivi sasa, dunia nzima imejaa hofu na simanzi kutokana na balaa la virusi vya corona vinavyosambaa kwa kasi ya ajabu na kuathiri zaidi nchi tajiri zaidi duniani zenye uwezo mkubwa (kibinadamu) wa sio tu kuyagundua magonjwa mapya bali pia kutumia nguvu za fedha na utaalamu mkubwa katika kuyakomesha.

Kinga yake

Dunia imejikuta inalazimika kukubaliana na mafunzo ya dini tukufu ya Uislamu kupambana na ugonjwa huu unaoenezwa kupitia hewa. Madaktari wanashauri watu wawe na tahadhari ili wasipate maradhi haya, ikiwemo kuepuka kugusana na mgonjwa, kukaa naye, kugusa vitu anavyovitu
mia au kuvuta hewa yake.

Pia, watu wametakiwa kuweka vikinga mdomo na pua (mask) ili kuzuia hewa yenye virusi kupita. Pia, watu wameshauriwa kunawa mara kwa mara kwa sabuni. Kwa upande wa mgonjwa, ameshauriwa kuziba kinywa chake anapokohoa, anapopiga chafya au anapopiga mwao ili kuepusha kuzagaa hewa.

Jambo ambalo watu wengi hawalijui ni kuwa, maelekezo hayo yalishatanguliwa na mafunzo matakatifu ya Uislamu. Mathalan suala la kuziba kinywa mtu anapokohoa, tunaambiwa:

“Mtume alipokuwa akipiga chafya hufunika uso wake kwa mkono au nguo yake na hushusha sauti yake.” [Mustadrak Alhakim].

Kuhusu suala la kunawa vilevile, maelekezo yanayotolewa yanakubaliana na mafunzo ya Uislamu yanayoagiza mtu kunawa, tena kwa maji ya kutiririka katika hali mbalimbali, ikiwemo kabla na baada ya kula na pia anapotoka chooni.

Uislamu unafundisha, mtu akiingia chooni avae viatu, ajikinge na chechezi za mikojo na akimaliza ajisafishe kwa kutumia mkono wa kushoto. Pia, asitumie mkono wa kushoto kwa kula ama kunywa. Kadhalika baada ya kutoka msalani lazima anawe mikono yake vyema.

Aidha, Uislamu umeagiza vitu vyote vichafu vishikwe kwa mkono wa kushoto. Mtume mwenyewe alionekana akishika sikio la mzoga wa mbuzi kwa vidole vyake viwili vya mkono wa kushoto katika soko la Madina akiwaonesha watu kwamba, dunia ni dhaifu zaidi kuliko mzoga.

Uislamu umekataza kufanya haja ndogo au kubwa katika maji yaliyotuama (yaliyotulia), kisha kuoga kwenye maji hayo. Abu Huraira (Allah amridhie) amemnukuu Mtume akisema:

“Usifanye haja ndogo katika maji yaliyotulia kisha ukaoga ndani yake.” [Bukhari na Muslim].

Licha ya hekima nyengine, lakini iliyo wazi ni kumtaka binadamu achukue tahadhari dhidi ya uwezekano wa kujiambukiza yeye mwenyewe.

Katika hadithi nyingine iliyosimuliwa na Abi Qatada, amesema Mtume: “Mmoja wenu anapokunywa asipulizie kwenye chombo, na anapokwenda msalani asiguse uchi wake kwa mkono wa kulia, na asijisafishe kwa mkono wa kulia.” [Ahmad].

Kutoka kwa Umar bin Abi Salama amesema kwamba, Mtume alimuambia:

“Ewe kijana, mtaje Mwenyezi Mungu, na kula kwa mkono wako wa kulia na kula (chakula) kilicho mbele yako.” [Ahmad].

Dhana ya karantini

Katika kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona, watu duniani wanashauriwa kubaki katika miji na nchi ambako maradhi yalishaingia; na kwa upande wa pili, walio nje ya miji iliyoathirika wasiingie. Kwa hiyo, nchi zimefunga mipaka yake na kuzuia mikusanyiko ili waliokwishaathirika wasiwaambukize wengine. Njia hii ambayo kwa kiasi kikubwa husaidia kunusuru wazima, tayari imeshatanguliwa na mafunzo ya Uislamu kupitia hadithi za Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie).

Mtume (rehema za Allah na amani zimshukie) alikataza kuingia ama kutoka katika mji au nchi iliyokumbwa na tauni (maradhi ya kuambukiza) ili maradhi hayo yabaki sehemu moja na kuwa rahisi kupambana nayo. Na amesema kwamba, watakaobaki watapata ujira mkubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.

Imamu Tirmidhy amepokea kutoka kwa Usama bin Zaid (Allah amridhie), kwamba Mtume alitaja tauni akasema:

“Hii ni mabaki ya adhabu iliyoshushwa kwa Wana wa Israil lakini Allah akaijaalia kuwa rehema. Basi, mkisikia imeingia katika nchi fulani, msiingie. Na yakitokea katika ardhi ambayo mpo, msitoke.”

Katika kupambana na janga hili, walimwengu wamesisitizwa kudumisha usafi, jambo ambalo ni moja ya kauli mbiu muhimu za Uislamu: “Uislamu ni msafi basi jisafisheni.” Vilevile, Uislamu umeifanya tohara (unadhifu) kuwa sharti kuu la kusihi ibada zote ikiwemo sala.

Katika hadithi iliyosimuliwa na Abu Malik Ash-ary, Mtume amesema: “Tohara ni nusu ya imani.” Pia, tusisahau hadithi iliyosimuliwa na Ibn Umar kwamba, Mtume amesema: “Allah hakubali sala bila ya tohara, wala sadaka ya mali ya kupora.” (Taz: ‘Attwahara’ cha Alqasim bin Salam)

Amesema kweli Allah katika neno lake: “Basi uelekeze uso wako sawasawa kwenye Dini – ndilo umbile la Mwenyezi Mungu alilo waumbia watu. Hapana mabadiliko katika uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Hiyo ndiyo Dini iliyo nyooka sawa. Lakini watu wengi hawajui.” [Qur’an 30: 30].

Show More

Related Articles

Back to top button
Close