6. Kutoka Katika Quran na Sunnah

Itikadi yetu na mlipuko wa virusi vya corona!

“Msitumie dini yenu kuficha upumbavu wenu.”

Hayo ni maoni yaliyokuwa yakizunguka nchini Singapore kwenye mitandao ya kijamii kufuatia maandamano makubwa ya Waislamu yaliyofanywa nchini Indonesia hivi karibuni ambapo waandamanaji walikuwa wanapinga kufutwa kwa tukio moja kubwa la kidini ambalo huwa linakusanya maelfu ya Waislamu nchini humo.

Kufutwa kwa tukio hilo kulitokana na tishio la maambukizi ya virusi hatari vya corona vinavyosababIsha homa kali ya mapafu (Covid-19).

Mdahalo kuhusu jinsi ya kushughulikia janga la virusi vya corona umewasili mlango wa mbele wa imani ya Waislamu. Wanaoamini usekula, kama jamii ya Singapore iliyotajwa hapo juu, mara zote wanafanya hila za kuleta taswira hasi kwamba kipengele cha imani ni karibu sana na ujinga na uchawi.

Wanaoamini usekula, hususani katika ulimwengu wa Magharibi na nchi zilizoendelea huabudu ‘reason’ (yaani fikiri, elewa, na unda hitimisho kwa mchakato wa mantiki) na ‘empiricism’ (nadharia kwamba elimu yote inatoka kwenye uzoefu wa akili). Misingi ya Kiislamu iko kinyume kabisa na usekula. Kwa kifupi, imani madhubuti ya Kiislamu ndiyo inayopaswa kubaki na kuathiri namna tunavyofikiri na kuyaangalia mambo.

Hata hivyo, kushika imani sawa sawa au kuwa Muumini, haimaanshi kwamba tumepoteza akili zetu. Kushika Imani sawasawa kunatufanya tubebe matokeo ya kuambatanisha Sharia ya Allah kwenye mwenendo wetu.

Kipengele hiki cha imani kinamfanya Muislamu awe bora zaidi kuliko watu wengine. Na Ubora wa imani madhubuti yenye tija ni kichocheo cha ufanisi kwa watu katika kukabiliana na shida na majanga mbalimbali.

Vipi tuweke imani yetu katikati ya janga hili la dunia? Kuna dondoo mbili muhimu ambazo zinahitaji kujadiliwa kuhusiana na kadhia hii.

Imani kwa njia ya tafakuri

Kwanza, umuhimu wa kusimamisha imani kupitia njia ya tafakuri (aqliyah). Mara nyingi masheikh na wanazuoni wa Kiislamu wamekuwa wakionya kuhusu jambo hili. Kwamba, itakuwa hatari iwapo mtu atakuwa na imani kutokana na hisia tu (wijdan) kwa kuwa hii inaweza kumuondoa kwenye imani sahihi na kumpeleka kwenye ukafiri na ujinga.

Mgongano wowote kati ya namna tunavyofikiri, imani, na mwenendo kama Waislamu, unaonyesha kwamba bado hatujaikumbatia kikamilifu imani. Kuiogopa corona, ambayo ni kiumbe cha Allah, haina maana kwamba hatuna imani na Allah .

Kanuni za kupambana na mlipuko

Pili, Sharia ya Kiislamu ina kanuni za jinsi ya kujipanga pale unapotokea mlipuko wa magonjwa. Mlipuko wa magonjwa haukuwahi kutokea wakati wa Mtume Muhammad (rehema za Allah na amani zimshukie), lakini aliufundisha umma wake namna ya kukabiliana nao iwapo utatokea.

Mtume alisema: “Mkisikia mlipuko wa ugonjwa katika mji, msiingie kwenye mji huo, lakini kama mlipuko ukitokea wakati mpo katika mji huo, basi msiondoke mahali hapo.” [Bukhari].

Hadithi hii inafafanua katazo la kuingia kwenye eneo lenye mlipuko wa ugonjwa ili mtu asiambukizwe. Vile vile, wale walio ndani ya eneo hilo hawawezi kuondoka, ili wasiwaambukize wengine isipokuwa pale yanapotafutwa matibabu zaidi.

Katika historia yetu, mlipuko wa ugonjwa ulitokea wakati wa zama za Khalifa Umar al-Khattwab (Allah amridhie) katika eneo la Amawash, jirani na Palestina, mkoa wa Sham. Umar pia alitii sharia kwa kutekeleza msingi wa hadithi hii, kwa kufuta kuondoka kwake kwenye eneo la mlipuko.

Hitimisho

Kwa kuhitimisha, dondoo hizi mbili zinaweza kuimarisha imani yetu na kuifanya iwe na tija, bila ya kupoteza uwezo wetu wa kufikiri kimantiki, ikiwa ni pamoja na kutopoteza ujasiri wa kuuthibitishia ulimwengu, kwamba Waislamu wana nguvu za kutosha kukabiliana na kirusi hiki cha corona, kwa kutumia imani yao!

Uislamu umekuja na seti kamili ya sheria na kanuni zinazoshughulikia kila tatizo linalotokea kwa wanadamu, wakati wowote na mahali popote. Ukamilifu huu wa Sharia ya Kiislamu unathibitishwa na Yule ambaye ni mkamilifu, Allah ‘Azza wa Jalla’. Kwa hiyo, haiwezekani kukuta dosari yoyote ndani yake, hata ikiwa ndogo kiasi gani.

Allah anasema: “Leo nimekukamilishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe ndiyo Dini. Na mwenye kushurutishwa na njaa, bila ya kupendelea dhambi, basi hakika Allah ni Msamehevu na Mwenye kurehemu.” [Qur’an, 5:3].

Show More

Related Articles

Back to top button
Close
Close